Imeandikwa na Saleh Ally wa www.salehjembe.blogspot.com
MGOGORO
wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo
kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja
likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.
Kundi
ambalo linamuunga mkono Jaydee na kumuona ni mkombozi, anazungumza kwa
niaba yake na wasanii wengine, la pili ni lile linalobaki upande
unaoshambuliwa, linatetea ngome yake.
Jaydee
anashutumu kubaniwa nyimbo zake na kituo hicho ambacho kupitia mitandao
kadhaa ya kijamii ameeleza wazi kuwa wanambania, wanaziponda lakini
hata watangazaji wake wamekuwa wakionyesha chuki binafsi dhidi yake.
Jaydee
pia aliwaponda wasanii Ben Pol na Linah anayetokea THT kwamba
walishindwa kutokea kwenye uzinduzi wa video ya wimbo wake wa Joto
Hasira, kwa madai walizuiwa na bosi wao.
Ujasiri
huu wa Jaydee ndiyo kitu bora ambacho kimekuwa kikitakiwa kufanyika
kutoka kwa wasanii, yaani wapigane kutetea muziki wa Tanzania hasa kama
kuna watu au kundi la watu limejikita katika kuuangamiza.
Lakini
ni tofauti kidogo, kwani wasanii wengi wamekuwa imara na kuwa tayari
kujitetea wenyewe tu na si vingine. Nasisitiza mara nyingi, wao ndiyo
wahusika wa kwanza na wanapaswa kuanzisha mapinduzi kuanzia kwao, mfano
kusema naonewa si kitu kibaya lakini je, umewahi kupigania wanaoonewa?
Kujitetea
pekee unaweza kufanya, lakini vipi utafanikiwa kama asilimia kubwa ya
kundi la wanamuziki linaendelea kuonewa. Ukibaki hauonewi pekee na
asilimia kubwa ya wasanii au wanamuziki inaonewa, kunaweza kuwa na mapinduzi sahihi?
Ndiyo
maana nashangazwa kusikia Jaydee leo anaona ubovu wa kituo hicho,
anathubutu kusema hadharani akionyesha wazi ameumia. Lakini miaka 10 au
zaidi iliyopita, Jaydee alikuwa kimya na hakuwaza kusema kwamba kituo
hicho kinawabania wasanii wengine na ‘kumtukuza’ yeye hata kama muziki
wake haukuwa wa kiwango kilichokuwa kinazungumzwa.
Siwezi
kusema muziki wa Jaydee ni mbaya, nimekuwa kati ya mashabiki wake.
Lakini yoyote atanichekesha akisema nyimbo albamu zake zote alizotoa
zilikuwa katika kiwango cha juu sana na ndiyo maana leo ni maarufu.
Hakuna
asiyejua kwamba miaka nenda rudi, wasanii wamekuwa wanaongoza kwa
unafiki, kutopendana wenyewe, kugeukana na hata kujenga makundi lukuki,
ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakishambuliwa maana katika maisha yao
hawana umoja.
Jaydee
alianza kuwa mtangazaji katika kituo hicho baada ya kuacha kurap,
akaamua kuachana na kurap na mwisho kuwa msanii wa nyimbo za
kubembeleza, mara ya kwanza akianza kutikisa na albamu ya Machozi, Solo
Thang anaweza kuhadithia vizuri kuhusu hili.
Kuanzia
albamu ya Machozi, kituo hicho ndicho kilisimama kuhakikisha anakuwa
bora hata kama muziki wake haukuwa ukimzidi kila mwanadada wakati huo.
Angalia,
kulikuwa wasanii kama Stara Thomas, Carola Kinasha ambao kiuwezo
walikuwa juu kuliko Jaydee, lakini hawakupewa nafasi ya kutosha, badala
yake Jaydee ambaye hakuthubutu kuwatetea hata kidogo akaendelea
‘kubebwa’ na watu wakaamini ni bora kuliko yeyote kwa upande wa akina
dada au kina mama katika kuimba, haikuwa hivyo.
Angalia
albamu ya Binti, karibu nyimbo zote zilikuwa na ujumbe mmoja, ulikuwa
ukimshambulia mwanaume mmoja ambaye alikuwa amemuumiza Jaydee. Takribani
ujumbe wa nyimbo karibu zote ulikuwa ni mmoja, lakini ilibebwa na
kuonekana ni moja ya albamu bora kabisa kuwahi kuwepo katika muziki wa
Tanzania, kitu ambacho hakikuwa sahihi.
Wakati
huo wasanii lukuki walilia kubaniwa, mmoja wao alikuwa ni Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ndiye alimtambulisha mwanadada huyo
alipomshirikisha katika wimbo wa Mambo ya Fedha, kabla ya hapo hakuwa na
jina. Jaydee hakuwahi kuungana naye hata kidogo hata kwa mstari mmoja
wa kumtetea au kuunga mkono kutetea muziki wa Tanzania, kuonyesha
anapinga mwenendo wa wanaolazimisha kuwabagua wasanii au kufanya mambo
kwa mabavu kwa kuwa wameshika mpini.
Hakuna
aliyesikia kilio cha Sugu, wasanii wanaochipukia bila ya kujua
wasemacho, kisa nyimbo zao zinapigwa redioni, ili kuonyesha shukrani za
dhati wakaanza kutangaza Sugu anatapatapa na amekwisha kimuziki!
Ajabu,
asilimia kubwa ya maneno yake ndiyo yanayozungumzwa leo, ndiyo
yanatumiwa na kila msanii anayebanwa au kuhisi kaonewa. Angalia, hata
Jaydee naye ameingia huko! Swali langu hapa je, Jaydee na wengine
wanaolalamika, wamekwisha kisanii?
Ndiyo
maana nasema, tasnia ya muziki hasa muziki wa kizazi kipya umejaza watu
wavivu kufikiri, wenye mioyo ya ‘Kichina’, wasio na uwezo wa kuthubutu
hata kidogo ambao wanasubiri wayumbe au kuumizwa wao ili wamtafute wa
kumuangushia lawama.
Jiulize,
kama Jaydee alibebwa kwa miaka 10, halafu leo analalamika atakuwa
sahihi? Sitaki kumpinga kwa kuwa kuna kitu anakiona lakini ninaamini
alikiona tokea mapema, akauchuna.
Bado
nasisitiza, yeye na wengine wote wanaolia baada ya kuguswa wao nawaita
wanafiki, wanapigana kwa ajili yao na si kwa muziki wanaoutumikia. Iwapo
wangekuwa tayari kupambana kwa ajili ya muziki huo, msanii kama Jaydee
asingeanza vita leo.
NARUDI KWA JAYDEE
NARUDI KWA JAYDEE
Sijawahi
kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa
mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni
kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao
zaidi.
Picha
ya unafiki na kujiangalia mwenyewe inaonekana sasa ingawa takribani
miaka mitano iliyopita nilianza kuinusa. Leo analia, anabaniwa na
anauona moto unaounguza muziki wa Tanzania ulivyo mkali.
Naamini
aliuona miaka kibao nyuma, lakini kwa kuwa alikuwa akitetewa hakuweza
kuangalia kwamba rafiki zake, wasanii waliombeba kabla walikuwa
wakiungua. Akaendelea kuwapita kwa raha zake mustarehe.
Tungeweza
kumuita Jaydee ni mpambanaji kama angewakosoa hao anawakosoa sasa
katika kipindi walichokuwa wamempa mbeleko yeye, basi kweli ingeonekana
anapigania muziki wa Tanzania. Sasa anapigania chake tu!
Jaydee
amefika mbali kimuziki, alikuwa bora jukwaani na nyimbo kadhaa na
nyingi zikapewa ‘over promotion’ lakini bado ninaweza kumuita mkongwe.
Ajabu alibaki chipukizi hadi leo katika suala la kutetea haki za wasanii
na muziki wenyewe.
Sitaki
kumkatisha tamaa kwa mapambano aliyoyaanza, ninaamini ana nafasi ya
kuanza kuusaidia muziki ambao umemsaidia. Lakini ndiyo kipindi ambacho
anaweza kupata machungu waliyopata wasanii wenzake kunyeshewa mvua na
kuunguzwa na jua wakati akiwa kivulini kwa ‘msaada’.
Anachokifanya
leo Jaydee ni nyongeza tu ya walichokifanya Sugu au Afande Sele au
wasanii wachache walioamua kuwa wakweli au wale walioamua kuwa wabunifu
kama Ambwene Yessaya ‘AY’, aliyekimbia vita ya redio na kuingia katika
kurekodi video bora zilizoendelea kumng’arisha.
Simzuii, Jaydee kuendelea kupambana, lakini namuasa anachokifanya kama ni kwa ajili ya muziki akipozwa tena, asirudi nyuma.
Ninachomkumbusha,
hata yeye amekuwa kundi moja na analowalaumu ambao angeweza kuwashauri
mapema ‘ndani ya mjengo’ kama angekuwa na nia nzuri na muziki wa kizazi
kipya. Msisitizo ‘Joto Hasira’ liwe la kweli.
No comments:
Post a Comment