Lubumbashi,
DR Congo. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea TP Mazembe
ya DR Congo, Mbwana Samata amesema viongozi wa klabu za Tanzania hawana
malengo ya kutwaa ubingwa wa Afrika ila wanapigania kutwaa ubingwa wa
Ligi Kuu tu.
Samata
alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa mtandao wa
klabu ya TP Mazembe wakati timu hiyo ilipokuwa imeweka kambi mjini
Ndola, Zambia kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Alisema,”Viongozi
wa klabu kubwa za Tanzania, Simba na Yanga hawana malengo ya kutaka
kushinda ubingwa wa Afrika na kucheza mashindano ya FIFA ya klabu bingwa
ya dunia, viongozi wanapigania kushinda Ligi Kuu tu.”
Samata
alisema,”Viongozi wa TP Mazembe wana malengo ya juu, wapo tofauti na
viongozi wa klabu kubwa za Tanzania, ndiyo maana TP Mazembe inakuwa
klabu kubwa.
“TP
Mazembe haionei wivu klabu nyingine za Afrika, ila zipo klabu nyingi za
Afrika zinazoionea wivu, TP Mazembe ina vifaa vyote muhimu vya
kuwaandaa wachezaji, ina miundombinu ya soka, ina wafanyakazi wanaoijua
soka na ina wachezaji wenye kiwango cha juu,”alisema Samata.
Alisema,
“TP Mazembe ina wachezaji nyota kutoka DR Congo, Ghana, Zambia,
Tanzania na Uganda, naona faraja kuchezea klabu hii, nataka mwaka huu
nitwae ubingwa wa Afrika nikiwa na klabu yangu ya TP Mazembe.
Nataka nicheze mashindano ya FIFA ya Klabu Bingwa ya Dunia, ambapo naweza kucheza dhidi ya Barcelona na kuonyesha uwezo wangu.”
Mwanacnhi
No comments:
Post a Comment