Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu wametua Dar es Salaam jana (Mei 17 mwaka huu) mchana, na
kujiunga moja kwa moja kwenye kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya michuano
ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo itafanyika leo (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Washambuliaji hao wa Taifa Stars
wamewasili saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea
Khartoum, Sudan ambapo juzi (Mei 16 mwaka huu) timu yao ya TP Mazembe
ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya huko.
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani kimepata
mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyoanzia Tukuyu
mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Naye Kocha Msaidizi wa Zimbabwe,
Kalisto Pasuwa amesema hawaifahamu vizuri Taifa Stars lakini wamekuja
kwenye mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni kwa ajili ya kushinda, na
kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona kiwango cha timu yake.
Milango kwa ajili ya mechi hiyo
itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei
Lamptey itakuwa wazi kuanzia saa 6 kamili mchana, na tiketi zitapatikana
katika magari maalumu uwanjani hapo.
Viingilio katika mechi hiyo ni
sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu, sh. 10,000 kwa
VIP C na B, na sh. 20,000 kwa VIP A. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz