Siku moja baada ya kuwasilisha maelezo yake ya utetezi baada ya
kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya Chadema, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Zitto Kabwe amekata rufaa Baraza Kuu kupinga hatua hiyo.
Zitto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila
Mkumbo walivuliwa nyadhifa zao na Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika
Novemba 20 na 21 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mwanasheria wa Zitto, Albert
Msando alitaja sababu mbili za kukata rufaa kuwa ni kukiukwa kwa
taratibu za kuchukua hatua za nidhamu na sababu zilizotolewa kutokuwa
sahihi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
Chadema, John Mnyika alisema mambo hayo yalishatolewa ufafanuzi na chama
na kwamba kukata rufaa ni haki ya kikatiba kwa mwanachama yeyote.
“Kukata rufaa ni haki ya kikatiba ya wanachama
yeyote. Rufaa ikatwe tu, itashughulikiwa kwa mujibu wa katiba, kanuni,
maadili na itifaki ya chama. Hata hivyo, ieleweke, rufani inahusu
kuvuliwa nafasi za uongozi, kusudio hilo haliwaondolei wajibu wa
kujieleza kwa maandishi mbele ya Kamati Kuu kwa nini wasifukuzwe
uanachama,” alisema Mnyika.