Wednesday, May 15, 2013

Kuziona Simba, Yanga Sh.5,000

Wachezaji wa Yanga wakijifua kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba jana kwa ajili ya mechi yao kukamilisha ratiba dhidi ya Simba.
Wakati kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi kimetajwa kuwa ni Sh.5,000, makocha wa timu hizo walioko kambini Zanzibar wamezidi kutambiana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka nchini (TFF) jana, kiingilio hicho cha chini kitakuwa ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo idadi yake ni 19,648.

Taarifa hiyo ilitaja viingilio vingine kuwa Sh. 7,000 kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, Sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, VIP C kiingilio ni Sh. 15,000, VIP B itakuwa Sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa Sh. 30,000. 

"Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni," ilisema taarifa hiyo na kuongeza kwamba mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Martin Saanya kutoka Morogoro ambapo atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha, na Jesse Erasmo kutoka Morogoro. Mwamuzi wa akiba atakuwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.


Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Leslie Liunda.

Kocha wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alisema jana kuwa ni lazima Yanga wafungwe katika mechi hiyo ya kukamilisha ratiba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga na Simba zinapambana Jumamosi katika mechi ya kutafuta heshima zaidi kwa vile tayari Yanga imeshatwaa ubingwa wa Bara na Azam imeshika nafasi ya pili na hivyo kuwa timu zitakazocheza michuano ya kimataifa mwakani.

“Vijana wangu wako imara na fiti kupambana na Yanga, hatuna hofu yoyote tunasubiri tu muda ufike,” alisema kocha huyo baada ya mazoezi ya jana ya Simba kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung mjini hapa.

Simba iliwasili hapa Jumapili kujinoa kwa mechi hiyo na imepiga kambi Mbweni pembeni kidogo ya mji na imekuwa inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Mao uliopo Kikwajuni.
Wapinzani wao, Yanga, wako kisiwani Pemba ambapo kocha wao Mholanzi Ernie Brandts amesema anataka kuimaliza mechi hiyo katika kipindi cha kwanza.

"Mipango yangu ni kumaliza mechi katika kipindi cha kwanza. Ingawa mchezo wa soka una dakika 90, ukifanya vizuri mwanzoni, dakika 45 za mwisho zinakuwa ni za kutulia, si kucheza kwa 'presha'," alisema kocha huyo wa zamani wa APR inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Rwanda.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa wachezaji wao wote wako katika hali nzuri na wamefanya mazoezi jana asubuhi wakiwa na morali ya juu.

SOURCE: NIPASHE

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...