Serikali
imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi ikieleza
kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia nguvu za kadiri hata
kiasi cha kusababisha madhara au kifo.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa
bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote
wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.
Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha
18(B) na 18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa
kutumia nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au
kifo katika mazingira ya kisheria.
Aliyataja
mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa uhai wa mtu mwingine, kuzuia
madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au kwa mtu mwingine na kumzuia
mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au kunajisi mtoto au kufanya vitendo
kinyume na maumbile.
Pia
kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au unyang’anyi wa kutumia silaha au
kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo chochote kinachohatarisha uhai
wa mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu
cha 18 na 18(A) cha Sheria ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio
mwaka 2002, kinampa haki mtu yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda
mtu mwingine, kulinda mali yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya
Serikali na taasisi zake, ambayo iko chini ya uangalizi wake kisheria.