Godfrey Mosha |
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Principal Ltd, Godfrey Mosha amesimulia jinsi Benki ya
Akiba Commercial (DCB), tawi la Kariakoo, ilivyoidhinisha malipo ya
fedha kwa mtu mwingine kutoka akaunti yake ndani bila yeye kujua.
Mosha
ni mmoja wa washtakiwa katika kesi ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya
Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Pamoja na
wenzake, Bahati Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu na Eda Makale,
wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh1.86 bilioni za EPA, katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuipitia Kampuni ya Changanyikeni Residential
Complex.
Katika
kesi hiyo dhidi ya DCB, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema, Mosha anaidai benki hiyo Sh46.8
milioni, zilizolipwa kwa mtu asiyemfahamu kwa kutumia hundi nne tofauti
na tarehe tofautitofauti.
Alidai
kuwa baada ya kubaini uhamisho huo, alikwenda makao makuu ya benki hiyo
ambako alimuona Meneja wa Fedha, Vicent Anthony na kumweleza kuhusu
tukio hilo wakati yeye hajawahi kuidhinisha uhamisho huo.
“Vicent
aliniambia kuwa siyo transfer (uhamisho), bali ni malipo yaliyofanyika
kwa kutumia cheque (hundi). Aliniambia namba za hundi hizo na ikaonekana
kuwa zililipwa kwa Rafael John Mkwabi, mwenye namba ya akaunti
11000787541,” alidai Mosha na kuongeza:
“Huyo John sijawahi kumwandikia hundi, wala sijawahi kufanya naye biashara, sijawahi kukutanana naye, wala simfahamu.”
Mosha
alidai kuwa hundi hizo zilikuwa zimesainiwa na Vicent na Meneja Mkuu,
Salehe Ramadhan, huku akidai kuwa saini inayoonekana katika hundi hizo
siyo yake.
Alizitaja
hundi hizo kuwa ni hundi namba 083722, ya Sh11.6 milioni iliyolipwa
Novemba 11, 2011 na hundi namba 083723 ya Sh9 milioni, iliyolipwa
tarehe hiyo.
Nyingine
ni hundi namba 083724 ya Sh14.4 milioni iliyolipwa Desemba 2011, hundi
namba 083725 ya Sh11.8 milioni iliyolipwa Desemba 3, 2011.
Aliziwasilisha
mahakamani hundi hizo na nyaraka mbalimbali zinazoonyesha saini yake
halisi, mahakama ilizipokea kama vielelezo vya ushahidi.
Baada
ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili Ngalo alifunga ushahidi na
mahakama ilipanga kuendelea na usikilizaji kesi hiyo Julai 8, wadaiwa
wataanza kujitetea.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment