WAZIRI
Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema anashangazwa na baadhi ya
viongozi wa dini kutoa sifa nzuri kwa watu wanaochanga fedha na si
kuzingatia uadilifu na wema walionao.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana katika sherehe za kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), zilizofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira mkoani Arusha.
Sumaye
alihoji kuwa inakuwaje wema wa baadhi ya watu unajitokeza zaidi
wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi unaotegemewa kufanyika mwaka
2015.
Sherehe
hizo za kutimiza miaka 50 zilifanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira
na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa KKKT kutoka sehemu mbalimbali
duniani pamoja na maaskofu wote wa dayosisi 20 zilizopo nchini.
Ingawa
Sumaye hakumtaja anayemlenga, lakini inaonekana kumlenga Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye katika siku za hivi karibuni
amekuwa akimiminiwa sifa kuwa ni mpambanaji wa umasikini na mtu mzuri
katika kuendesha harambee makanisani zinazowezesha kupatikana
mamilioni ya fedha.
Hivi
sasa, Lowassa anaonekana ndiye ‘mtaji’ mkubwa kwa viongozi wa
makanisa yanayohitaji kuendeleza miradi mbalimbali ambapo wamekuwa
wakimualika kwenye harambee zao.
Lowassa
mwenyewe alikaririwa hivi karibuni mkoani Dodoma akisema kuwa yeye
hana mamilioni ya fedha kama baadhi ya watu wanavyomhusisha
anaposhiriki harambee, bali ana watu wenye ushawishi katika jamii.
Kauli ya Sumaye
Sumaye
alisema ni jambo la kutia aibu na kushtua kuona watu wakipewa sifa za
kuvutia kwa sababu ya kuchangia mamilioni kwenye shughuli za kanisa
au binafsi na si kwa sababu ya uadilifu au wema wao.
Alisema
katika siku za hivi karibuni kumeibuka mambo mengi machafu
yaliyokithiri katika jamii na watu wanyonge kukosa haki zao za msingi
hadi watoe hongo au rushwa.
“Nafasi
katika nchi zimekuwa za biashara, watu hawaangalii tena uwezo au
uadilifu wa mtu anayeutaka uongozi bali wanaangalia ametoa fedha kiasi
gani za kuwahonga wapiga kura.
“Hata
katika baadhi ya dayosisi zetu na sharika zetu watu wakipewa sifa za
ajabu si kwa sababu ya uadilifu wao au wema wao, bali kwa sababu tu
wamechangia fedha kwa shughuli zetu za kanisa au hata binafsi.
“Hatujiulizi
kuwa mbona wema huu unajitokeza zaidi wakati kama kuna uchaguzi
unaotegemewa? Je, hapo hatusatahili kutupwa nje na kukanyagwa kanyagwa
kwa sababu chumvi imepotea utamu wake?
“Je, haya ni mafanikio ya miaka 50 ya kanisa au ni maeneo ambayo inabidi tujitazame na tujirekebishe?” alihoji.
Kuhusu
kanisa hususani masuala ya kijamii, Sumaye alisema pamoja
kushughulikia masuala ya kiroho, bado linapaswa kushughulikia masuala
ya mwili ambao ni hekalu la Mungu, hivyo kanisa lina jukumu kujenga
jamii yenye maadili mema na kukemea maadili mabaya.
“Yesu
alisema; ‘nyinyi ni chumvi ya ulimwengu’, lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena ni ya kutupwa nje
ikinyagwe na watu.
“Lakini nasema nyinyi ni nuru ya ulimwengu, hivyo ni wajibu wenu
kutoa nuru kwa wengine maana yake ni kutoa malezi mema kwa jamii. Je,
kanisa letu limefanikiwa kwa kiasi gani katika eneo hili?
“Je,
tumekuwa na ujasiri wa kukemea mabaya hata kama kukemea huko
kunawaudhi au kuwakera wenye mamlaka au na wenye nguvu za fedha? Je,
tuna ujasiri kama wa Nabii Mikaya mwana Imla, aliyemwambia mfalme wake
nitasema yake bwana aliyoniambia na kumwambia mfalme kuwa ukienda
kupigana vita vya kuteka Tamoth Gileadi hutarudi hai?” alihoji Sumaye.
Sumaye
pia alizungumzia matukio yaliyoanza kujitokeza katika siku za hivi
karibuni akisema hivi sasa taifa limekuwa na matatizo mengi ya watu
kuchukiana kwa sababu ya imani zao, mabomu kulipuliwa katika
mikusanyiko ya jamii na kuteketeza watu wasio na hatia.
“Leo
Watanzania wanabaguana kwa maeneo wanakotoka na sababu nyingine
zisizo na msingi, matukio ya viongozi wa dini kuuawa, uchomaji moto wa
makanisa, mapigano ya nani achinje mnyama, haya yote ni mambo mageni
nchini mwetu, tuendelee kuimboea nchi yetu amani, lakini wakati maombi
yakiendelea Watanzania tujue tunajichimbia kaburi letu wenyewe kama
hatutapiga vita maovu haya,” alisema Sumaye.
Naye
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini, Askofu Dk. Alex
Malasusa, alisema kanisa halitaogopa hujuma au kusema ukweli na
wataendelea kujenga marafiki wema bila kujali itikadi za marafiki wao.
Katika
hatua nyingine, Askofu Malasusa alibainisha kuwa kitendo cha viongozi
dini ya Kiislamu kuhudhuria sherehe hizo za miaka 50 kimeonyesha sura
mpya.
“Kuwapo kwa viongozi wa dini ya Kiislamu kumedhihirisha kuwa yanayozungumzwa nje si halisi,” alisema Dk. Malasusa.
Katika sherehe hizo maaskofu wa kanisa hilo walihudhuria ikiwamo pia viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Via Tanzania daima
No comments:
Post a Comment