Dar
es Salaam. Licha ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama
kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo
atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa
tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni
pamoja na kutumia maji ya bomba.
Mbali na tahadhari hiyo,
ziara hiyo ya Obama itakuwa na ulinzi mkubwa ambao pengine haujawahi
kutokea katika historia ya viongozi wa nje wanaotembelea Tanzania kwani
utahusisha idadi kubwa ya magari, ndege za kijeshi na meli kubwa ya
kivita ambazo zitakuwa zikifanya doria karibu na pwani ya Tanzania.
Tahadhari
za matumizi ya chakula, maji na nyinginezo zimetolewa katika nchi zote
tatu za Afrika ambazo Obama atatembelea, kila moja kwa jinsi
Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi
Vyombo
vya usalama vya Marekani vimejipanga kuhakikisha ziara ya kiongozi
huyo haivurugwi kwa namna yoyote ile. Tayari ndege za jeshi zilizobeba
magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’ maalumu kwa
ajili ya kiongozi huyo, yamewasili katika nchi hizo tatu za Afrika
atakazotembelea.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post la
Marekani, ndege hizo pia zimebeba malori matatu ambayo yamesheheni
karatasi maalumu za kuzuia risasi kupenya kwenye vioo, zitakazobandikwa
kwenye madirisha ya hoteli ambazo Rais Obama na ujumbe wake watafikia.
Kwa
mujibu wa gazeti hilo, mamia ya mashushushu wa Marekani tayari wako
katika nchi hizo. Meli maalumu za kubeba ndege za kivita, maarufu kwa
jina la ‘amphibious ship,’ ikiwa na hospitali maalumu na yenye vifaa
vyote itaweka nanga baharini, jirani na nchi atakayokuwa Rais Obama,
tayari kukabiliana na dharura yoyote itakayotokea. Gazeti hilo
liliandika kuwa ndege za kivita za Marekani zitakuwa zikipeana zamu
kufanya doria kwa saa 24, katika anga la nchi ambayo Rais Obama
atakuwepo, iwapo ndege za ‘adui’ zitakaribia eneo linaloitwa ‘anga ya
rais.’ Kwa mujibu wa gazeti hilo, ziara ya Rais Obama aliyoifanya hivi
karibuni katika nchi za Ujerumani na Ireland Kaskazini, japo kulikuwa
na gharama kwa walinzi, lakini safari za nchi za Afrika zimeelezwa kuwa
na gharama kubwa zaidi.
Tahadhari
Kwa mujibu wa
taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya Marekani, ambayo Mwananchi imepata
nakala yake, watu watakaokuwa kwenye msafara wa Obama wametakiwa
kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia maji ya chupa zaidi.
“Kutokana
na mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu wetu kutumia maji ya chupa
zaidi kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa
kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa malaria nchini, ujumbe wa Obama
umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.
Deet
ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya
kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye
vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia
mwaka 1957.
ATM nazo noma
Pia watu watakaokuwa
kwenye msafara wa Rais Obama wametakiwa kuhakikisha wanatumia mashine
za kutolea fedha (ATM) zilizoko karibu na hoteli watakazofikia.
“Kuna
tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri kutumia ATM ambazo ziko katika
sehemu zisizo salama. Pia katika kipindi watakachokuwa Tanzania watu
wanapaswa kutumia teksi ambazo zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia
siyo vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye vyumba mtakavyolala. Pia
kina mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa
wanapita mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment