Tuesday, August 12, 2014

BUNGE MAALUMU LA KATIBA MTEGONI TENA LEO

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta. PICHA |MAKTABA

Mjadala kuhusu masuala ya Muungano unatarajiwa kurejea upya katika kamati za Bunge Maalumu leo, wakati zitakapoanza kujadili sura za saba, nane, kumi na moja, 18 na 15 za Rasimu ya Katiba.
Kamati zimepewa siku sita kujadili sura hizo tano ambazo zina jumla ya ibara 79, huku miongoni mwake zikigusa masuala mengi ambayo msingi wake umejengwa juu ya mfumo wa serikali tatu.
Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na baraza la mawaziri, tume ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika (Tanganyika na Zanzibar), Sekretarieti ya Tume ya Uhusiano na Uratibu, Masuala yanayohusu Benki Kuu na Fedha pamoja na uteuzi wa watumishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Suala la aina ya muungano lilianza kujadiliwa katika sura ya kwanza na ya sita katika awamu ya kwanza ya Bunge iliyomalizika mwishoni mwa Aprili mwaka huu na kuzua mvutano mkali ambao hatimaye ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kususia mchakato huo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Wajumbe hao ni wale wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wanataka mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ya kuwapo kwa muundo wa serikali tatu yabaki kama yalivyo na upande mwingine unaowajumuisha wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee.
Kutokana na mvutano huo, Bunge Maalumu liliahirisha upigaji kura kuamua aina ya muundo unaofaa, lakini hata liliporejea Agosti 5, mwaka huu halikuweza kupiga kura, badala yake lilibadilisha kanuni ili kuwezesha upigaji kura kufanyika baada ya kumaliza mjadala wa sura zote ndani ya kamati. 
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hakuna maelekezo yoyote yaliyotolewa kwa wajumbe kuhusu jinsi ya kujadili masuala yanayohusu muungano na kwamba wajumbe watazingatia mapendekezo waliyoyatoa katika rasimu ya kwanza na ya sita.
“Sidhani kama ni wajibu wetu kutoa maelekezo yoyote, kinachoweza kutokea ni wajumbe kuzingatia kila walichokijadili na kukubaliana katika sura zile za awali, kama walikubali serikali ya shirikisho watazingatia hilo, kama walikubaliana serikali mbili watazingatia hilo pia,” alisema Hamad.
Itakumbukwa kwamba idadi kubwa ya kamati baada ya kujadili sura ya kwanza na ya sita zinazohusu aina ya muungano, zilipendekeza kuachana na muundo wa shirikisho na kuwasilisha maoni yanayotaka kuendelea kwa mfumo wa Serikali mbili. 

Kamati nyingi zilipata idadi ya kura za kutosha kuunga mkono mapendekezo hayo na chache zilikosa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ikiwa kamati hizo zitazingatia uamuzi wake wa awali, basi masuala yote yanayogusa serikali tatu yatafutwa, hivyo zitakuwa na kazi kubwa ya kuandika upya ibara nyingi zinazozingatia utekelezaji wa mfumo serikali mbili. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Maudhui ya Ibara
Ibara ya 98 ya Rasimu pamoja na mambo mengine, inazungumzia idadi ya mawaziri ambao idadi yao hawapaswi kuzidi 15, huku uteuzi wao ukipendekezwa uthibitishwe na Bunge.
Ibara ya 99 inazungumzia uwepo wa Waziri Mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge, wakati Ibara ya 100 (1) inasomeka kuwa: “Waziri Mwandamizi atakuwa na madaraka ya udhibiti na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za serikali za siku hadi siku.” Katika sura ya nane inayozungumzia uhusiano na uratibu wa serikali, Rasimu inapendekeza kuanzishwa kwa tume ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi washirika.
Tume hiyo iliyopewa jina la “Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali”, wajumbe wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mwenyekiti, Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakazi wanaoziwakilisha nchi washirika katika Serikali ya Muungano na waziri mwenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Ibara ya 110 inabainisha kazi za tume hiyo, utaratibu bora na endelevu wa kushauriana na kushirikiana baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika pamoja na kukuza na kuwezesha uratibu na ushirikiano miongoni mwa nchi washirika kuhusu mambo yasiyo ya Muungano. 

Ibara ya 229 inazungumzia masuala ya fedha na jinsi nchi washirika wa muungano zinavyoweza kukopa fedha kutoka ndani na nje ya nchi wakati Ibara ya 234 inapendekeza Serikali za Nchi Washirika kuwa na Benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za serikali ya nchi mshirika husika na kusimamia sera za kifedha.
Ibara ya 237 iliyopo katika Sura ya 15 inazungumzia uwapo wa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa litakalokuwa na wajumbe kadhaa wakiwamo Makamu wa Rais, Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar na Waziri mwenye dhamana ya ulinzi.
Akizungumzia sura hiyo mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema Watanzania wasitarajie miujiza katika mijadala inayogusia muundo wa Serikali.
“Wakati wakijadili sura ya kwanza na ya sita zilizokuwa zikigusia masuala ya muungano wajumbe walikubaliana juu ya muundo wa serikali mbili, licha ya kuwa hawakupiga kura ya pamoja kuamua jambo hilo,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo katika sura hii ya nane, mtizamo wao utakuwa uleule kama ilivyokuwa sura mbili zilizopita. Hakutakuwa na mvutano mkubwa kwa sababu awali walishakubaliana kuhusu muundo wa serikali mbili. Watanzania wategemee hivyo.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) ambalo limeweka kambi Dodoma kushinikiza Bunge hilo kusitishwa, Deus Kibamba alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilishatoa mwelekeo wa kuijadili rasimu hiyo lakini haufuatwi.
“Tume ilisema sura ya sita, nane, 10 na 12 zinazungumzia muundo wa Serikali na zijadiliwe kwa pamoja ili upatikane mwafaka, ushauri ambao haukufuatwa. Kesho (leo) mvutano utakuwa mkubwa kutokana na hali halisi iliyopo juu ya muundo wa serikali,” alisema. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...