Tuesday, August 12, 2014

UCHAWI WASHIKA KASI, ALBINO WAANGAMIA


Vifaa vinavyodaiwa kuwa ni vya kishirikina

Jana tulichapisha habari za kusikitisha kutoka wilayani Urambo, mkoani Tabora kuhusu Pendo Sengerema, msichana wa miaka 15 mwenye ulemavu wa ngozi (albino), ambaye watu wenye imani za kishirikina wamemkata mkono wa kulia na kuondoka nao.

Huu ni uthibitisho kwamba Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi wanaendelea kupoteza maisha au kupata vilema vya kudumu kutokana na sehemu ya jamii yetu kukumbwa na imani potofu za kishirikina kwamba viungo vya watu hao vinaleta utajiri mkubwa na wa haraka.

Hatuna maneno stahiki ya kuelezea tukio hilo, isipokuwa tu kusema kwamba linasikitisha na kufadhaisha.

Kama msichana mdogo hivyo anaweza kufanyiwa ukatili wa kiwango kikubwa kiasi cha kupoteza kiungo muhimu kama mkono, ambao ungekuwa tegemeo kubwa kwake katika kufanya shughuli za kumwezesha kujitegemea kimaisha, basi tukubaliane kwamba ushirikina umeigeuza jamii yetu kuwa sawa na jamii ya wanyamapori.

Ni imani hizo potofu ambazo zimeikumba jamii yetu tangu mwaka 2000 wakati nchi yetu ilipoanza kushuhudia mauaji ya kinyama dhidi ya ndugu zetu hao wenye ulemavu wa ngozi.

Miaka 14 imepita sasa na vitendo hivyo vinaendelea. Bahati mbaya Serikali imeshindwa kuonyesha dhamira ya kutokomeza uovu huo, bali imebakia kutoa machozi ya mamba. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Tulitarajia Serikali na Bunge viweke mkakati wa kupambana na watu wanaofanya uovu huo, angalau kwa kutunga sheria kali dhidi yao na kuwatia mbaroni waganga wanaoendelea kuchochea vitendo hivyo. Kesi nyingi za watuhumiwa wa vitendo hivyo zinasuasua mahakamani, huku Serikali ikifumbia macho waganga wa kienyeji wanaopiga ramli.

Mfano ni wale wanaopiga ramli eti kuwawezesha watu kupata utajiri, mvuto, vyeo, kufuta kesi mahakamani, kurudisha wapenzi, kutibu ukimwi, kupata madaraka na kadhalika. Serikali inashindwaje kuwabaini wakati wanaweka wazi anwani na namba zao za simu katika matangazo wanayobandika barabarani na mitaani?

Jambo la ajabu ni kwamba Serikali inaendelea kuikumbatia sheria dhaifu ya mwaka 1928. Hatuelewi sababu zinazoifanya Serikali kushindwa kupitia upya Sheria ya Tiba Mbadala pamoja na taratibu za usajili wa waganga wa kienyeji. Hii ni pamoja na udhibiti wa shughuli zao kwa kuhakikisha wapiga ramli wanafutiwa leseni zao.

Tumesema yote hayo kuonyesha udhaifu wa Serikali katika kusimamia na kuratibu vita dhidi ya mauaji ya albino. Sisi tunadhani tumerudi nyuma kama taifa katika vita ya kukomesha unyama huo. Kwa mfano, utafiti uliofanywa katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Rukwa na Tabora umebaini kwamba waathirika wa unyama huo sasa wanakatwa mikono.

Kwa muhtasari tu, tangu mwaka 2000 yamefanyika mashambulizi zaidi ya 153 ambapo watu 76 wamepoteza maisha. Kati ya watu 34 walionusurika, wengi wao walikatwa viungo au kuumizwa vibaya, huku makaburi 15 yakifukuliwa na viungo vya watu hao kuibwa. Ni majaribio manne tu ya kufukua makaburi ndiyo yaliyoshindwa.

Serikali inastahili lawama kwa kuendelea kuwapo kwa hali hiyo. Inakuwaje zaidi ya nusu ya waganga wa kienyeji bado hawajasajiliwa? Na inakuwaje wanaachwa waendeshe shughuli zao kwa kuegemea uchawi na ushirikina? Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
 Je, waganga wa kienyeji hawana maadili au miiko inayosimamia kazi zao? Tunasubiri sasa kuona jinsi Serikali ilivyoguswa na kukatwa mkono kwa msichana Pendo Sengerema ambaye amelazwa katika Hospitali ya Urambo, mkoani Tabora. 

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...