Tuesday, June 25, 2013

WABUNGE NA MASHOGA WATETA..... HOFU YA KUWA NA RAIS SHOGA TANZANIA YATANDA....!!!


WABUNGE wanachama wa Chama cha Kupambana na Ukimwi (TAPAC), wiki iliyopita walikutana na kujadiliana mambo mbalimbali na mashoga katika mkutano wa mwaka wa chama hicho uliofanyika kwa muda wa siku tatu mjini  Dodoma. Katika mkutano huo, baadhi ya wabunge walionyesha wasiwasi wa taifa kupata rais shoga katika miaka ijayo kutokana na ongezeko la mashoga hapa nchini.

Mbali na wasiwasi ulioonyeshwa na wabunge, mashoga waliokuwa wakihudhuria mkutano huo, walilalamikia vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na wanajamii wenzao na kudai watambulike na wapatiwe huduma za msingi za kibinadamu.


Akizungumza katika mkutano huo uliomalizika jana, Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM), alitahadharisha uwezekano wa nchi kupata rais shoga katika miaka ijayo, iwapo hatua za makusudi za kudhibiti hali hiyo hazitachukuliwa.


“Tabia ya kuwapeleka watoto kwenye shule za mabweni wangali wadogo wa umri wa miaka hadi miwili, itatuletea matatizo baadaye.

“Katika shule nyingi za bweni vitendo vichafu vinafanyika, vikiwamo vya ushoga. Katika vyuo vikuu hivi sasa kuna mashoga wasiopungua 40,000. Hii ni hatari, tusipojihadhari tutakuwa na rais shoga katika miaka ijayo,” alisema Kessy huku akishangiliwa na wabunge.

Mbunge huyo alitaka elimu dhidi ya ushoga na athari zake ienezwe nchini kupitia vyombo vya habari na nyumba za ibada.


Naye, mmoja wa mashoga waliohudhuria mkutano huo aliyejitambulisha kwa jina la Abdilah Ally, alieleza kuwa yeye ni shoga mwenye wanaume watatu lakini amekuwa akikutana na vitendo vya unyanyasaji kutoka ndani ya jamii inayomzunguka.

“Tunataka haki zetu. Tunanyanyaswa katika jamii hasa na polisi. Na sisi tunastahili huduma bora za afya na nyingine tuweze kujikinga na Ukimwi,”
alisema Ally, mkazi wa Dar es Salaam.

Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Mshauri wa Masuala ya Ufundi wa Kampuni ya Jhpiego, Dk. Augustine Hellar, ilieleza kuwa kuna wanaume 397,458 waliotahiriwa nchini hadi Mei, mwaka huu katika mpango maalumu wa tohara kwa ajili ya kupambana na maradhi ya Ukimwi.

Dk. Hellar alitoa takwimu hizo alipowasilisha mada kuhusu tohara ya hiari kwa wanaume katika kukabili maambukizi ya Ukimwi nchini.

Alisema lengo la mpango huo ulioanza kutekelezwa Oktoba, 2011 katika baadhi ya mikoa nchini ni kutoa tohara kwa wanaume milioni 2.8 kila mwaka mmoja.

Alisema mpango huo umekabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ya watu wazima ambao ndiyo walengwa kutojitokeza kwa wingi na baadhi ya watu kuhusisha hatua hiyo na upotevu wa nguvu za kiume.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...