Serikali
imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi ikieleza
kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia nguvu za kadiri hata
kiasi cha kusababisha madhara au kifo.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa
bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote
wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.
Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha
18(B) na 18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa
kutumia nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au
kifo katika mazingira ya kisheria.
Aliyataja
mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa uhai wa mtu mwingine, kuzuia
madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au kwa mtu mwingine na kumzuia
mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au kunajisi mtoto au kufanya vitendo
kinyume na maumbile.
Pia
kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au unyang’anyi wa kutumia silaha au
kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo chochote kinachohatarisha uhai
wa mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu
cha 18 na 18(A) cha Sheria ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio
mwaka 2002, kinampa haki mtu yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda
mtu mwingine, kulinda mali yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya
Serikali na taasisi zake, ambayo iko chini ya uangalizi wake kisheria.
Kauli
hiyo ya Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi, ilitolewa
ikiwa ni ufafanuzi wa jibu la swali la nyongeza lililoulizwa bungeni Mei
28,2013 na Rashir Ally Abdalah (Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji yanayofanywa na askari polisi ni mauaji ya kisheria.
Kutokana
na kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa
spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo, na jana Silima kutoa kauli ya
Serikali kujibu mwongozo huo.
“Ikumbukwe
pia kuwa, kifungu cha 29 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi
wasaidizi Sura322, pamoja na Kanuni za Kudumu za Utendaji za Jeshi la
Polisi Na274, vinampa haki ya kisheria askari polisi kubeba na kutumia
silaha za moto ikiwamo bunduki na mabomu katika utekelezaji wa majukumu
yake ya kila siku..,”alisema Silima.
Alifafanua
kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ikiwamo
alizozitaja, mahakama katika nyakati tofauti imetoa msimamo wa kisheria
juu ya suala hilo.
Akitoa
mfano alisema: “Mathalan katika kesi ya Seif Mohamed Senzagala dhidi ya
Jamhuri ya mwaka 1994 kama ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report
ukurasa wa 122, ambapo mshitakiwa (mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga
mlalamikaji ambaye alimfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”
Alisema
katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja na kuridhia uamuzi wa
mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia nguvu kupita kiasi,
ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani alitenda kosa lile
wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa mlalamikaji.
“Kwa
msingi huo, tarehe 28 Mei, 2013 wakati nikijibu swali Na 290, nilitumia
maneno ‘mauaji yanayofanywa kisheria’ nikimaanisha mauaji yanayotokea
katika mazingira niliyoeleza..,”alisema Silima.
Hata
hivyo alisema siyo nia ya Serikali kuhalalisha vitendo vya matumizi
mabaya ya silaha ambavyo vinaweza kufanywa na askari wasio waadilifu.
Alibainisha
kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
sheria, kuheshimu haki za raia na kutumia busara kutatua migogoro.
Hata
hivyo, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imelaani kauli ya Serikali
kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi iliyoitoa jana na kueleza kuwa
haikubaliani nayo kwa kuwa inatoa baraka kwa polisi kuendeleza mauaji
ya raia.
Akizungumza
na mwandishi wetu baada ya kikao cha bunge kuahirishwa, Waziri Kivuli
wa Mambo ya Ndani wa kambi hiyo rasmi, Vicent Nyerere alisema kauli hiyo
ingekuwa na uthabiti kama askari polisi wangekuwa waadilifu.
“Kauli
ingekuwa thabiti kama polisi wangekuwa waadilifu. kabla ya kutoa kauli
hiyo, Serikali ilitakiwa kuchuja miongoni mwa askari wa jeshi la polisi,
wa ngazi zote na kuwaondoa wasio waaadilifu ndipo wakatoa kauli hiyo
wananchi wataielewa Serikali,”alisema Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa
Musoma Mjini(Chadema).
Kwa
upande wake, Mbunge wa Ole, (CUF) Rajab Mbarouk Mohammed akizungumzia
kauli hiyo ya Serikali alisema kuwa majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Pereira Ame Silima ni ya kisiasa.
Alisema
kwamba kauli hiyo ni mwendelezo wa kauli iliyotolewa Alhamisi iliyopita
na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiwataka pilisi kuwashughulikia kwa
kuwapiga watu wote watakaokaidi kutii sheria.
“Hakuna
mwenye haki ya kuua, kuua ni kuua tu. Mahakama pekee ndiyo ina haki ya
kuhukumu kifo baada ya kumtia hatiani mshtakiwa husika. Lakini kuwa
polisi wanafundishwa utii, siyo kuua,”alisema Rajab.
Alifafanua kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na kwamba kuruhusiwa kujihami haimaanishi kuua raia.
Nao
Wabunge Aeshi Hilaly na Aly Keissy walisema ni vizuri raia wakatii
mamlaka iliyopo na kutekeleza utii wa sheria bila shuruti.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema: “Maoni yangu haki za watuhumiwa lazima ziheshimiwe.”
Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS), Francis Stola alisema hakuna
sheria inayompa mamlaka askari polisi kutumia nguvu za ziada ikiwemo
kupiga raia pindi anapotekeleza majukumu yake,isipokuwa tu anaweza
kutumia nguvu kiasi iwapo raia anayekabiliana naye anaonyesha vitendo
vya kukaidi amri ama kuhatarisha usalama
Stola
ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kauli bungeni
alisema kuwa kwa kufuata sheria polisi haruhusiwi kupiga raia. “ Ukisoma
sheria hakuna mahala utakuta kuna neno limeandika piga…. Askari polisi
anachoweza kufanya ni arrest(kamata) na siyo vinginevyo, hana mamlaka
kabisa ya kupiga raia”
Alisema
sheria imetamka wazi kuwa kunapojitokeza hali yoyote inayopaswa
kdhibitiwa na vikosi vya ulinzi, nguvu inayopaswa kutumika ni ile ya
kawaida na kwamba kitendo cha kutumia risasi za moto ama kupiga raia ni
ukiukwaji wa sheria za nchi.
Alisema
polisi anapaswa kutoa mwongozo kwa raia kumwelekeza jambo la kufanya
iwapo kunajitokeza hali ya sintofahamu,lakini hapaswi kutumia nguvu
kupita kiasi ikiwemo kuwapiga raia
“
Sheria inasema wazi kwamba panapojitokeza hali yoyote korofi, polisi
wanatakiwa kutumia nguvu ya kawaida tu kukabiliana na hali hiyo na wala
siyo kutumia silaha za moto… silaha za moto zinaweza kutumika tu iwapo
kunajitokeza tukio ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa maisha ama
mali isipotee” alisema
Kuhusu
wananchi kufanya maandamano, rais huyo alisema maandamano ni haki ya
msingi ya kila raia,lakini yanafanyika katika utaratibu maalumu. “
maandamano ni haki ya kila raia lakini panapaswa kuwa na utaratibu
maalumu…. Kama kunajitokeza maandamano ambayo hayana utaratibu polisi
wanapaswa kutumia reasonable force (nguvu ya kawaida) kudhibiti
maandamano hayo na wala siyo kutumia nguvu za ziada.
Mwananchi:
No comments:
Post a Comment