IMEELEZWA
kuwa, mtuhumiwa Omar Mussa Makame (35) anayeshikiliwa na Jeshi la
Polisi kwa madai ya kumuua Padri Evaristus Mushi ni mwanachama wa CUF
ambaye aligombea nafasi ya uwakilishi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 katika Jimbo la Rahaleo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Kaimu
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud alithibitisha jana kuwa,
mtuhumiwa huyo ni mwanachama wao na alishiriki katika mchakato wa
uchaguzi mkuu na kusimamishwa na chama katika kampeni za Uwakilishi
Jimbo la Rahaleo.
“Ni
kweli mtuhumiwa anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji
ya Padri Mushi ni mwanachama wetu na alishiriki katika mchakato wa
kuwania Uwakilishi Jimbo la Rahaleo mwaka 2010.
Hata
hivyo, Hamad alisisitiza na kusema suala la Omar kamwe lisihusishwe na
CUF na kusema suala hilo watalitolea tamko baadaye.
Kwa
mujibu wa kumbukumbu za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ripoti ya
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Jimbo la Rahaleo, mgombea wa
CCM, Nassor Salim Ali maarufu kama Jazirra aliibuka na ushindi kwa
kupata kura 3,952 sawa na asilimia 63.10, wakati mgombea wa CUF, Omar
Mussa Makame alipata kura 2,310 sawa na asilimia 39.9 na kushika nafasi
ya pili.