Ujumbe
wa amani na tahadhari ya umakini kwenye utoaji maoni kwenye Katiba
ndiyo vilitawala wakati wa misa za Sikukuu ya Pasaka zilizofanyika
sehemu mbalimbali nchini jana na juzi.
Miongoni mwa waliotoa hotuba wakati wa sikukuu hiyo ni
pamoja
na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alikuwa mkoani
Mtwara; na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyekuwa jijini Dar es
Salaam.
Mkapa akataa udini
Rais mstaafu Mkapa alitumia fursa ya kutoa salamu katika Kanisa
Katoliki mjini Masasi kuliasa taifa kujiepusha na utoaji wa maoni ya
Katiba kwa misingi ya dini.
“Wapo watakaopata uwakilishi kupitia rasimu ya Katiba ya nchi.
Namwomba Mwenyezi Mungu awape mwanga, muhakikishe jambo moja tu ambalo
litakuwa msingi mkubwa wa amani na maendeleo na umoja wa taifa letu.
Watupatie Katiba ambayo inatoa fursa kamilifu ya kila mtu kuwa na imani yake.
“Katiba inayoheshimu imani ya kikatiba na imani zote zinazofanywa na
wananchi wa Kitanzania…Vilevile ihakikishe kwamba dola au nchi yetu
haina imani rasmi kama vile nchi yetu isivyo ya kabila moja, hivyo
haiwezekani kuwa na Katiba ambayo inatambua kwa dhana au maandalizi ya
vipengele mbalimbali kwamba kuna udini, haiwezekani.”
Askofu na Muungano
Watanzania wametakiwa kuwapuuza watu wanaohubiri kuuvunja Muungano
kwani watu hao wana agenda binafsi ambazo si kwa faida au masilahi ya
nchi, bali wao na baadhi ya mataifa yanawafanya vibaraka wa kuvuruga
amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa
Jimbo Katoliki la Dodoma wakati wa misa ya Pasaka ambayo iliyofanyika
kitaifa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mt. Paulo wa Msalaba mjini
humo.
Askofu Nyaisonga alisema hata kama kuna baadhi ya matatizo katika
Muungano, yanapaswa kuboreshwa badala ya kuuvunja kabisa Muungano ambao
kimantiki umeijengea nchi heshima.
“Muungano ni heshima ya taifa, tusiuvunje, tutumie Katiba Mpya
kuboresha pale tunapoona kuna upungufu na tujiepushe na hoja za watu
wenye masilahi binafsi ambao wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya mataifa
kutaka kutuvuruga kwa kusema Muungano hauna faida, hao wana masilahi
binafsi tuwapuuze,” alisema Askofu Nyaisonga.
Pengo ataka mafundisho
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo, aliwaambia waumini wa kanisa hilo, “Tutafute ufumbuzi
wa matatizo yetu kwa njia ya imani.”
Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati wa misa ya mkesha wa Sikukuu ya
Pasaka iliyofanyika juzi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar
es Salaam.
Ulinzi uliendelea kuimarishwa ndani na nje ya kanisa hilo kwa waumini
waliofika kukaguliwa na polisi mlangoni kabla ya kuingia kanisani,
kitendo ambacho pia kilifanyika siku ya Alhamisi Kuu.
Pia Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro jana liliimarisha ulinzi
katika makanisa mbalimbali mjini Moshi wakati wa ibada ya Pasaka
kutokana na vitisho vya kuhujumiwa kwa baadhi ya makanisa.
Katika milango ya makanisa, walionekana askari kanzu, wenye sare na
kuruta kutoka Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA-zamani CCP),
wakishika doria.
Akataza visasi
Waumini wa dini nchini wametakiwa kutolipiza visasi kwa sababu
vinaweza kusababisha chuki, mfarakano na hatimaye machafuko kwa watu
wasio na hatia. Hayo yalisemwa na Paroko Msaidizi wa Kanisa la Mtakatifu
Petro, Osterbay jijini Dar es Salaam, Padre Gerald Kamina kwenye misa
ya Sikukuu ya Pasaka jana.
SOURCE::MWANANCHI:
No comments:
Post a Comment