Ndugu Wananchi;
Naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa
fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila
mwisho wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo
la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013.
Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo
kati ya China na Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru
wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake.
Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.
Kwa
niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping
akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba
tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine
mashuhuri watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami
pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu
na kufanya ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi
yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu
isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika
kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi
yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini
kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi
wake.
Tumefarijika
sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na
viongozi wapya wa China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na
uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa
nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi
zetu mbili zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja
mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya kipaumbele nayo
imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais
Xi Jinping alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama
cha Kikomunisti cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo
kati ya Tanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka
1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa
Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai.
Rais
wa China aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania
katika medani ya kimataifa na kuchangia katika jitihada zetu za
kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya maendeleo. Katika miaka 49
ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya
maendeleo ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere
ambao ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna
miradi kadhaa mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na
Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya China. Wakati wa ziara yake, Rais
Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo
kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa
saini siku ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la
ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la Dar es Salaam. Ajali
hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi
kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17
waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa.
Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia
ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi
na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la
ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata
hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa
zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika
binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake
madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi,
na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova
pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na
wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza
pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na
hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya
waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na
jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote
tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.
Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno
mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana
dhana yake. Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo
kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika
kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa
Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za
ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la
kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima
zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza
ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na
wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao. Watimize
wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili
wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane.
Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la
Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na
hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha
ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo
la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na
Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za
nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa.
Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa
mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya.
Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na
Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana
itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika
orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka
na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na
Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo
zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu,
kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya
dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi
vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani
achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa
mifano.
Na,
pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande
mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo
inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na
viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa
ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.
Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu
nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu,
kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na
Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa
katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba
Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa
Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi
kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za
kujenga Makanisa na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki
maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu
hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo
wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza,
hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu
kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya
Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa
mashtaka kwa nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua wajibu
wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu
wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali.
Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na
wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao
kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi
binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila
ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya
shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W.,
safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi.
Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu
mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo sikushiriki mazishi ya
Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine
ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa
upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa
kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu
ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine
siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri
hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia
wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo,
tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa
nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi
sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya
kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri
Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili
Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na
kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni
kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.
Kila
tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali
kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa
hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua
viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo
cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu
zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale
kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu.
Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote
walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza
kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale Buseresere na
limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu
zao.
Hivi
kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile
kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na
Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi
kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku
kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia
tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji
Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na
Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta
njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze,
waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo
wa kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu
hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo
na Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa
kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina
uhusiano kabisa na lile la Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu
nani achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya
upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya
hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya
kabla yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose
Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh
Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na bado
tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa
moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu?
Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo.
Kuna
watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni
dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya
uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu
wakishirikiana na wenzao wa nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno
kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika
mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika
usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali
kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa,
kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo
lina mazingira yake maalum. Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio
la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha
Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi
wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha
Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu
wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana
wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya
waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao
walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma
moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali
popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio
lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya
vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za
mkononi. Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya
usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa
lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya
ukweli. Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza
ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa
Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao
Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa
Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba
mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa
kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu
wanazozijua wao na kwa faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la
kutaka Wakristo na Waislamu wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya
Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali
imewatelekeza raia wake. Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma
tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini
kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na Waislamu na
kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali
haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa
kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha
Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa
tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila,
watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na
kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo
walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta
watu wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande
wa Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi
zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma
Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika
pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu
uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika
ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa
makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa
na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua.
Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo
mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea
chuki na vurugu za kidini. Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine
ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia
nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa,
yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili
vya radio yaani Kwa Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro
vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya
Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza
haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia
wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa
kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na
yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote,
makabila yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako salama.
Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na
mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona
Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale
yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari
za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie
sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha
yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe,
harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa
Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo
pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa
Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu
na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine
yenye huduma ya chakula.
Ndugu
zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya
namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa
kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo
hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike,
na wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini
wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado
narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili
kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko
mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala
yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi
wao kwa jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi
yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha
uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni
viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana
na viongozi kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na
Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona kuwa
wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya
viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.
Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na
Watanzania. Kuna upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini
wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha
nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea. Maisha ambayo
waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano
na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri
Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya
kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini
yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi. Lazima
tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na
kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia
katika vita vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na
kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari
za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza. Wawe makini na
maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie
kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa
dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa
ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba
wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha
vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya
Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba
kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na
mshikamano wetu. Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano
bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu.
Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi,
kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali
haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza
dini yo yote au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama
itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama
inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali
zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo
zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment