Monday, April 01, 2013

SIMULIZI YA ALIYENUSURIKA KIFO KUTOKA GHOROFA YA 15.


Fundi ujenzi, Yusuph Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Ijumaa iliyopita.
 

Rais Kikwete na Mkewe, Mama Salma Kikwete wakimpa pole Yusuph Abdallah katika Hospitali ya Muhimbili walipotembelea majeruhi wa ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa 16. Picha na Muhidin Michuzi. 


FUNDI ujenzi, Yusuph Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Ijumaa iliyopita.


Yusuph aliliambia Mwananchi akiwa wodini kwamba kilichomponya ni neema za Mungu kwani kabla jengo hilo kuporomoka yeye alikuwa ghorofa ya 15 kwenye jengo hilo katika Mtaa wa Indira Gandhi akiendelea na ujenzi.

Alieleza kuwa hakuwa anafahamu kinachoendelea, bali aliona ghafla jengo linaaanza kuporomoka, na baada ya hapo hakufahamu zaidi kilichotokea hadi alipojikuta yuko hospitalini.

“Kweli jengo lilipoanza kuporomoka sikutambua nini kinachoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo hapa Muhimbili,” anasimulia Abdallah.

Alisema anahisi alipoanguka alifunikwa na kifusi kilichomponda na kuvunja miguu yote.

Fundi huyo ambaye amefungwa plasta gumu (P.O.P) miguu yote, alisema hakuweza kuona watu waliomwokoa.

Mwingine aokolewa na mkewe.

Mkazi wa Ubungo, Ally Mlela ambaye ni fundi madirisha anasimulia jinsi mke wake alivyomwokoa katika ajali hiyo baada ya kumtaka asiende kufanya kazi siku hiyo.

Akisimulia jinsi ilivyokuwa Mlela anasema siku ya tukio aliwasiliana na rafiki yake ambaye amepoteza maisha katika ajali hiyo na kumtaka aende akaonane na mkandarasi wa jengo hilo, ili ampe kazi ya kuweka madirisha.

“Majira ya asubuhi kati ya saa mbili na saa tatu hivi nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu jina maarufu anajulikana kama Tafu, ambapo alinitaka niende nikaonane na mkandarasi wa jengo hilo ili anipe kazi ya kuweka madirisha,” anasema Mlela.

Anasema wakati akijiandaa kutoka mke wake alimwambia siku hiyo apumzike asiende kufanya kazi naye akakubali, lakini haikupita muda mrefu mke wake alimfuata na kumuuliza amesikia taarifa kwamba kuna jengo limedondoka ?.

“Niliamua kwenda katika eneo la tukio na ndipo alipogundua kwamba eneo hilo ndiyo alipotakiwa kwenda kufanya kazi.

Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea nilijaribu tena kumpigia simu rafiki yangu.

Nikiwa bado kwenye eneo la tukio ghafla nikaona mguu ukitolewa kwenye mchanga na nilitambua ulikuwa mguu wa rafiki yangu baada ya kuona kiatu chake.”
Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...