IMEELEZWA
kuwa, mtuhumiwa Omar Mussa Makame (35) anayeshikiliwa na Jeshi la
Polisi kwa madai ya kumuua Padri Evaristus Mushi ni mwanachama wa CUF
ambaye aligombea nafasi ya uwakilishi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 katika Jimbo la Rahaleo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Kaimu
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud alithibitisha jana kuwa,
mtuhumiwa huyo ni mwanachama wao na alishiriki katika mchakato wa
uchaguzi mkuu na kusimamishwa na chama katika kampeni za Uwakilishi
Jimbo la Rahaleo.
“Ni
kweli mtuhumiwa anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji
ya Padri Mushi ni mwanachama wetu na alishiriki katika mchakato wa
kuwania Uwakilishi Jimbo la Rahaleo mwaka 2010.
Hata
hivyo, Hamad alisisitiza na kusema suala la Omar kamwe lisihusishwe na
CUF na kusema suala hilo watalitolea tamko baadaye.
Kwa
mujibu wa kumbukumbu za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ripoti ya
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Jimbo la Rahaleo, mgombea wa
CCM, Nassor Salim Ali maarufu kama Jazirra aliibuka na ushindi kwa
kupata kura 3,952 sawa na asilimia 63.10, wakati mgombea wa CUF, Omar
Mussa Makame alipata kura 2,310 sawa na asilimia 39.9 na kushika nafasi
ya pili.
Taarifa
iliyotolewa na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mussa Ali Mussa mtuhumiwa
anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kukamatwa
kwa Omar kunatokana na michoro ya teknolojia ya kisasa chini ya msaada
wa upelelezi wa makachero kutoka FBI ambayo iliweza kutambua sura
yake.
Uchunguzi
zaidi uliofanywa na gazeti hili umegundua kwamba mtuhumiwa huyo licha
ya kuwa mfuasi wa CUF, mama yake mzazi ni kada wa CCM.
Mama yake, Tatu Sheha mkazi wa Mkele, Unguja ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa CCM katika Jimbo la Kwamtipura.
Tangu
kuibuka kwa kadhia hiyo inayomhusu mtoto wake, mama mzazi amekosa raha
na faraja kiasi ya kushindwa kuhudhuria vikao vya chama kwa takribani
wiki mbili sasa.
Baadhi
ya wananchi Zanzibar wamepongeza juhudi za Jeshi la Polisi za
kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, wakisema ni dalili njema za
kutaka kukomesha matukio ya mauaji kisiwani Zanzibar.
No comments:
Post a Comment