LICHA
ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume bado hali ya staa wa filamu za
Kibongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ ni tete ambapo Rais Mstaafu wa Awamu
ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’, amejitosa baada ya kumuona
alivyodhoofu kwa sasa.
JK na Mzee Majuto walikutana uso kwa
uso wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar ambako
kulikuwa na shughuli ya utoaji tuzo za filamu zilizojulikana kwa jina la
Tuzo za Kimataifa za Sinema Zetu ambapo walionekana wakiteta kwa dakika
kadhaa kabla ya kila mmoja akaenda kukaa kwenye siti yake.
Mzee Majuto alionekana akiwa amedhoofu
kwani aliingia ukumbini akitembea kwa msaada wa fimbo huku akionekana
kutokuwa mchangamfu kama ilivyo kawaida yake, hali iliyowahuzunisha
mashabiki wake waliokuwa ukumbini hapo.
Mwandishi wa habari hii alizungumza
na Mzee Majuto ili kujua hali yake na kile alichokuwa akiteta na JK
ambapo alisema kuwa, kutokana na hali yake kutokuwa nzuri licha ya
kufanyiwa upasuaji, rais huyo alimuahidi kwamba watajadili na
watampeleka India kwa matibabu zaidi kwani tiba za hapa hajaridhishwa
nazo.
“JK ameniahidi kwamba watanipeleka
India kwa ajili ya matibabu ikiwa ni baada ya kwenda na kujadili na rais
aliyeko madarakani Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ ili nikapate matibabu
zaidi maana tiba nilizopatiwa hapa bado sijakaa sawa.
“Kwanza kwa sasa nimepatwa ugonjwa mpya
tena ambapo mkono unaniuma mno, ninashindwa hata kushika chochote ndiyo
nataka nirudi tena hospitalini nikawaeleze kuhusu hilo maana hali siyo
nzuri kabisa,” alisema Mzee Majuto.
Hata hivyo, Mzee Majuto alisema kuwa,
pamoja na hilo, JK alimuahidi kwamba atamnunulia trekta kwa ajili ya
kulima kwenye mashamba yake ambako atapanda minazi huko Tanga ili aweze
kuendesha maisha.
Na GPL
No comments:
Post a Comment