Utata mpya
umeibuka kuhusu matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya
wagombea watatu waliotangazwa washindi kuwekwa kando ikidaiwa kuwa
badala yake walioshindwa waliapishwa kuchukua nafasi zao, hali iliyozua
vurugu kubwa zilizotulizwa na polisi kwa mabomu ya machozi Ubungo jana.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa CUF wanaodai
wagombea wa chama chao ndiyo walioshinda, waliibuka na kutanda nje ya
Hoteli ya Landmark kupinga kuapishwa kwa baadhi ya wenyeviti wa Serikali
za Mitaa wa CCM katika Wilaya ya Kinondoni, hatua iliyosababisha baadhi
ya wagombea na mashabiki kushushiwa kipigo hadi polisi walipoingilia
kati kwa kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Vurugu hizo zilizodumu kuanzia saa tatu hadi saa
tano asubuhi, zililenga kuzuia wateule watatu wa mitaa ya Ukwamani,
Pakacha na King’ong’o kuapishwa kwa madai kuwa siyo walioshinda.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa
Msisiri, Juma Mbena alivamia eneo hilo akidai kuwa Gasper Chambembe
(CUF), ambaye alishinda katika mtaa huo hakustahili kuapishwa, kitendo
kilichosababisha ashushiwe kipigo na wafuasi wa CUF. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Licha ya Mbena kupigwa na kuchaniwa nguo, pia
Sultan Jetta (CCM) ambaye alitangazwa kushinda katika Mtaa wa Ukwamani,
Kawe alizuiwa na wafuasi wa CUF kuapishwa, wakidai kuwa mgombea wao,
Nasri Mohammed Mashaka ndiye aliyestahili kuapishwa. Alipogoma,
walimkamata na kumshushia kipigo hadi alipookolewa na polisi.
Baadaye Jetta alirudishwa ukumbini chini ya ulinzi
wa polisi na kuapishwa pamoja na wenyeviti wenzake 153 kati ya 191 wa
Wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Pakacha Kata ya
Tandale, Hussein Juma Mpeka (CUF) alidai kuwa licha ya uchaguzi huo
kuvurugika, alipewa barua ya kuitwa kuapishwa lakini baada ya kufika
eneo hilo alikataliwa kuingia ukumbini, badala yake aliyeruhusiwa ni
Nassib Omary Kalenga wa CCM.
Hali ilivyokuwa
Shughuli ya kuapisha wenyeviti hao ilianza saa
mbili asubuhi na baada ya saa moja, wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya
manispaa hiyo walikusanyika eneo hilo ili kushuhudia uapishwaji huo.
Kati yao walikuwapo viongozi wa vyama vya CCM na
CUF wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na wagombea walioeleza kuwa walishinda
katika uchaguzi na matokeo yao kutangazwa lakini hawakupewa barua za
uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika.
Waendesha bodaboda na wananchi wanaofanya biashara
zao kando ya hoteli hiyo nao walikusanyika kwa lengo la kushuhudia
kinachoendelea hali iliyowafanya polisi waliokuwa katika magari mawili
aina ya Landrover Defender kuwataka wananchi hao kuwa watulivu.
Mmoja wa wakazi wa Kawe, Anna Cheupe aliyekuwa
eneo hilo alisema licha ya kuwa ni mwanachama wa CCM, hakufurahishwa na
kitendo cha matokeo ya Mtaa wa Ukwamani kubadilishwa, kauli ambayo
iliungwa mkono na watu waliokuwa karibu yake.
Wakati idadi ya watu ikizidi kuongezeka, polisi walisikika
wakiomba msaada kwa wenzao na ilipofika saa 3.55 asubuhi magari mengine
mawili yalifika na askari waliokuwamo kuanza kupiga mabomu ya machozi
mfululizo kwa nusu saa.
Mabomu hayo yalisababisha wananchi kukimbia ovyo
na wengine kunusurika kugongwa na magari yaliyokuwa yakipita katika
Barabara ya Mandela kabla ya kufungwa kwa muda.
Risasi zilipigwa hewani ili kuwaokoa watu
waliokuwa wakishambuliwa kwa kupigwa huku sauti zikisikika, “Piga hao
wezi…, mwizi, piga mwizi huyo. Tuuweni tumechoka kuonewa, Pigeni tena
nyingine hewani.”
Polisi waliwaokoa Mbena na Jetta na kuondoka nao
na baadhi ya wenyeviti waliokuwa wakisubiri kuapishwa walizirai. Askari
waliokuwa hawana vifaa vya kufunika uso, waandishi wa habari na wahudumu
wa hoteli walikimbia kutafuta maji ya kunawa uso.
Utata wa matokeo
Kutokana na utata, kila chama kilikuwa na matokeo
yake. Mwenyekiti wa CUF, Kata ya Kawe, Bakari Mozina alisema katika Mtaa
wa Ukwamani, mgombea wa chama hicho alipata kura 568 na CCM 560 lakini
matokeo yalibadilishwa.
“Tunashangaa kwa nini ameitwa kuapishwa mgombea wa CCM wakati sisi ndiyo tulioshinda?” alihoji. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Alisema licha ya utata wa matokeo, pia kulikuwa na
utata wa majina… “Katika karatasi ya kupigia kura kulikuwa na jina la
Seleman Mohammed Jetta, anayeapishwa leo (jana) ni Sultan Jetta ambaye
tunapinga asiapishwe.”
Wakati Mozina akieleza hayo, Jetta alisema yeye
ndiye mshindi katika mtaa huo kwa kuwa alipata kura 561 na CUF wa
alipata kura 548. Katika Mtaa wa King’ong’o, aliyekuwa mgombea wa CUF,
Abubakar Nyanguma aliyedai kuwa alishinda alisema: “Mimi nilipata kura
461 na mgombea wa CCM, Demetrius Mapesi alipata kura 450, cha ajabu
barua ya kuitwa kuapishwa amepewa mwenzagu badala ya mimi.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Wilaya ya
Kinondoni, Danstan Tido alisema washindi watatu katika wilaya yake
wamenyimwa barua za kuitwa kuapishwa na ndiyo chanzo cha wafuasi wa
chama hicho kujazana eneo hilo ili kushuhudia nani atakayeapishwa.
“Washindi wa mitaa ya King’ongo, Pakacha na
Ukwamani ndiyo waliostahili kuapishwa leo baada ya kutangazwa washindi
katika uchaguzi uliopita. Lakini tunashangaa kuona kuwa hawakupewa barua
za kuwatambua, hii siyo demokrasia tunayoitarajia katika mfumo huu wa
vyama vingi,” alisema Tido.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho kutoka Kawe,
Jafari Makonyola alisema walikwenda katika hoteli hiyo kuhakikisha kuwa
wanaostahili ndiyo wanaapishwa na si vinginevyo.
“Lengo letu ni kuona tuliyemchagua ndiye anayeapishwa na
ikishindikana basi asiapishwe yeyote. Matokeo ya uchaguzi ni lazima
yaheshimiwe kwa kuwa wanaochaguliwa wanakuja kufanya kazi na wananchi,
hivyo ni lazima tuwaridhie,” alisema Makonyola.
Mpeka alisema, “Ilinishangaza maana ofisa mtendaji
aliniita na kunipa barua ambayo inaonyesha kuwa mimi ni mshindi.
Niliipokea na kufika pale ukumbini na nilifanikiwa kuingia ndani ila
baada ya muda alinifuata na kuniambia kuna tatizo, alinitoa nje na
mgombea wa CCM akaingia ndani na kuapishwa. Sijaelewa nini kimetokea na
sijui nini nifanye.”
Kauli ya Jetta
“Baada ya kuondolewa hapa nilipelekwa Kituo cha
Polisi Urafiki ambako nilipewa PF 3 ili nikatibiwe na baadaye chini ya
ulinzi mkali kama nilivyoondoka nilirudishwa hapa na kuendelea na zoezi
hili. Hivi sasa mimi ni kiongozi halali kwa mujibu wa sheria,” alisema
Jetta.
Kauli ya mkurugenzi
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya
Kinondoni, Mussa Nati alisema wenyeviti walioapishwa jana ni 154 kati ya
191 lakini alipoulizwa sababu za wajumbe wengine kutohudhuria shughuli
hiyo aling’aka akisema, “Baadhi ni wagonjwa na wengine wana sababu zao…
nyingine ongeza wewe mwandishi, mimi nitajuaje kila sababu ya mshiriki
kutohudhuria?”
Alipotakiwa kufafanua sababu za kuvuruga matokeo
ya uchaguzi na kuathiri uapishwaji wa wenyeviti hao, mkurugenzi huyo
alikataa kuzungumza.
Awali, akizungumza na wenyeviti hao, Nati alisema
hakuna atakayedhulumiwa nafasi yake... “Ngoja niwape neno la uchokozi,
ikitokea mtu asiyehusika akasaini (fomu za kiapo), mfano mwandishi wa
habari au mhudumu wa hoteli, hatutamtambua kwa kuwa hausiki. Wenyeviti
wote tunawatambua hivyo kuweni na amani,” alisema Nati.
Lipumba akoleza
Katika hatua nyingine; Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba amewataka wananchi wa Kata ya Buguruni kujitokeza kwa
wingi kwenye shughuli ya kuapishwa kwa wenyeviti wa mitaa wa Manispaa ya
Ilala leo ili kudhibiti uchakachuaji unaofanywa dhidi ya vyama vya
upinzani.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara jana, Kata
ya Buguruni jana, Profesa Lipumba alisema ufisadi wa CCM umekithiri
mpaka kwenye matokeo ya uchaguzi ambayo tayari yanafahamika kwa
wananchi.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la wakazi wa kata hiyo
kutetea haki yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Aliwatahadharisha
wasikubali kumpokea mwenyekiti ambaye hawajamchagua katika mitaa yao.
“Ni jukumu lenu kulinda kura zenu, lakini ni muhimu zaidi
kulinda matokeo wakati wa kuapisha. Zoezi la kuapisha wenyeviti
limevurugika kule Kinondoni, sasa kesho ni zamu ya Ilala. Mjitokeze kwa
wingi ili wasifanye kama walivyofanya Kinondoni,” alisema.
Profesa Lipumba aliwashukuru wananchi wa Kata ya
Buguruni kwa kuwachagua wenyeviti wa mitaa kutoka CUF, hali aliyosema
inathibitisha kuwa wamechoshwa na ufisadi unaofanywa na Serikali ya CCM.
Kata ya Buguruni ina mitaa sita, kati ya hiyo, CUF imeshinda mitano, mmoja ukichukuliwa na CCM. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment