Monday, December 29, 2014

MTOTO WA MIEZI MITATU MWATHIRIKA DAWA ZA KULEVYA

 
Zena akiwa na mtoto wake. Mwanamke huyo na wataalamu wa tiba wanathibitisha kuwa mama mwenye uraibu anayenyonyesha anaweza kumwathiri mtoto.

Mtoto mwenye umri wa miezi mitatu, mkazi wa Buza, Dar es Salaam amebainika kuwa mwathirika wa dawa za kulevya.
Damu na mkojo vya mtoto huyo (jina tunalihifadhi) vilichukuliwa na kupimwa katika maabara ya Hospitali ya Mwananyamala na baada ya saa mbili, majibu yalitoka na kuthibitisha kwamba alikuwa na chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini.
Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa kuwapo kwa heroini mwilini mwa mtu, huweza kuonekana katika mkojo ndani ya siku mbili hadi nne iwapo dawa hizo zilitumiwa na mhusika kwa kati ya saa mbili hadi tano.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.

Hatua ya kumfanyia vipimo mtoto huyo wa kiume, inatokana na jitihada za gazeti hili kutaka kufahamu jinsi utumiaji wa dawa za kulevya kwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha unavyoweza kumwathiri mtoto akiwa tumboni au anayenyonya maziwa ya mama mwathirika.
Mtaalamu wa tiba katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Elifasi Mritu anasema: “Ni kweli ukitumia dawa za kulevya wakati unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye huathirika.”
Kauli ya Dk Mritu ambaye ni daktari katika kitengo cha tiba ya methadone hospitalini hapo, inaungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Frank Mushi ambaye anasema mama anayetumia dawa za kulevya akiwa mjamzito humwathiri pia mtoto.

Mama wa mtoto azungumza
Mama wa mtoto, Zena maarufu Zerish, mkazi wa Yombo Buza alikiri kwamba alipata ujauzito wakati akitumia dawa za kulevya na kwamba hadi sasa anavuta dawa hizo huku akiendelea kumnyonyesha mtoto huyo.
Anasema baada ya kujifungua hakukaa ndani kwa siku 40 kama wafanyavyo wanawake wengi wa Kitanzania, kwa sababu mwili wake ulikuwa unahitaji ‘unga’ vinginevyo hali yake huwa mbaya.
Anasema baada ya kujifungua alianza kuzunguka huku na kule akiwa na mtoto mgongoni, huku akiwa amebeba mfuko wake wa plastiki wenye mahitaji muhimu ya mtoto kama nepi na nguo.
Anasema anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake pia hupata ‘stimu’ kwa sababu hupata dawa hizo za kulevya kupitia maziwa anayonyonya na hivyo wote wawili kulala fofofo sehemu yoyote ile.
Hata hivyo, kwa Zerish na mwanaye, anapofikia hali ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya zinapoisha mwilini na hivyo kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali mno.
Anasema dawa zinapoisha mwilini na mtoto naye huwa katika hali hiyo na hivyo hulia sana. Hali hiyo humfanya akimbie kutafuta dawa ili ‘kujinusuru’ yeye na mwanaye.

Uwezekano wa tiba
Dk Mushi anasema watoto wanaoathirika kwa dawa kupitia mama zao, hulia sana na kujinyonganyonga hali inayoashiria wanapata maumivu ya tumbo.
“Lakini tumaini lipo kwa watoto hao, kwani hupewa dawa aina ya morphin ambayo hukata ulevi huo taratibu. Baada ya muda hupona kabisa,” anasema.
Hata hivyo, alisema iwapo mtoto ataendelea kunyonya maziwa bila kupata tiba huku mama naye akitumia dawa hizo, huweza kuwa mtumiaji wa dawa hadi anapokuwa mkubwa.
Katika hospitali za Muhimbili na Mwananyamala, wanawake wenye watoto walio na uraibu wa dawa za kulevya hutakiwa kuhudhuria kliniki kila siku bila kukosa.
Mwanamke anayetumia dawa za kulevya hutibiwa kwa dawa aina ya methadone na mtoto hupewa morphin. Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...