Wednesday, December 17, 2014

AJALI ZAUA WATU 8 TABORA NA MOROGORO

Kamanda wa Polisi Tabora, Suzan Kaganda


 Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda. PICHA|MAKTABA

WATU wanane wamekufa papo hapo, huku wengine 50 wakijeruhiwa vibaya katika ajali mbili tofauti zilizotokea Tabora na Morogoro jana.

Katika ajali ya Tabora, basi la Kampuni ya Mohammed Trans likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam lilipinduka mara nne katika kijiji cha Makomero, kata na wilaya ya Igunga na kuua watu 5 na kujeruhi 50.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Suzan Kaganda alikiri kutokea kwa ajili hiyo na kusema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi wa kujua chanzo cha ajili hiyo iliyotokea majira ya saa 5:30 asubuhi.

Alilitaja basi hilo kuwa ni aina ya Scania lenye namba za usajili T 738 AAP ambalo lilikuwa na zaidi ya abiria 55. Akizungumza katika eneo la tukio, mmoja wa majeruhi, Maimuna Mussa (27) aliyekuwa akielekea Dodoma na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili, alisema walikuwa kwenye mwendo kasi na alishitukia gari likiacha njia na kupinduka mara nne.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.  
 

“Kwa kweli Mungu ni mkubwa nimeshuhudia mwenyewe gari likipinduka mara nne, lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mimi na mwanangu tumetoka salama,” alisema na kudai kuwa, gari hilo lilikuwa bovu, licha ya mwonekano wa nje kwa maana ya rangi kuvutia.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk Fedilis Mabula alisema alipokea maiti watano, wakiwamo wanawake wawili na wanaume watatu, ilhali majeruhi ni 50, kati yao wanawake wakiwa 23 na wanaume 27.

Wote wamelazwa wodi namba 8 katika Hospitali ya wilaya ya Igunga na kwamba hali zao bado ni mbaya. Naye Agnes Haule anaripoti kutoka Morogoro kuwa, watu watatu wamekufa katika ajali iliyotokea eneo la Ruhindo Sokoine baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuhama upande wake na kugongana uso kwa uso na lori kwenye barabara kuu ya Morogoro - Dodoma.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo ajali hiyo ilitokea alfajiri ya kuamkia jana katika eneo la Ruhindo likihusisha gari ya Totoya Noah lenye namba za usajili T 311 BLM lililokuwa likiendeshwa na Sembuli Nasibu (30) likitokea Gairo kuelekea mjini.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Rusian Protas (44), Charles Marwa (35) na Warioba Makoba (22) wote wakiwa ni wakazi wa Gairo. Kamanda huyo alisema kuwa gari hilo (Noah) lilikuwa likipishana na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 774 BUW lililokuwa na tela lenye namba za usajili T146 AKJ lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Zambia.

Wakati hayo yakitokea Tabora na Morogoro, kutoka Mbeya Joachim Nyambo anaripoti kuwa, milii ya watu watano waliokufa juzi katika ajali ya lori lililobeba maiti mkoani Mbeya, imetambuliwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ahmed Msangi waliokufa katika ajali hili kuwa ni Sophia Omar (50) na Susan Melele (31) wakazi wa Mbalizi wilayani Mbeya na Stella Mwaluswaswa (38) mkazi wa Tunduma wilayani Momba.

Wengine ni Bulele Mwaipaja (48) mkazi wa Uyole jijini Mbeya na Jacob Nyaluke (17) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Mbozi Misheni na mkazi wa wilayani Mbozi.

Katika ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Kantela Ntokela wilayani Tukuyu, watu 36 walijeruhiwa baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 143 AJR lililokuwa linasafirisha maiti kutoka kijiji cha Ilemi jijini Mbeya kwenda Tukuyu, Rungwe kutumbukia korongoni.

Kamanda Msangi alisema waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni wanaume 16 na wanawake 16 ambao alisema hali zao zinaendelea vizuri.

Jeshi la Polisi linamsaka dereva wa lori hilo aliyetajwa kwa jina la Robert Mwakibibi (37) mkazi wa Uyole aliyekimbia mara baada ya ajali kutokea.

Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year. 

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...