Baraza la Wanawake
wa Chadema (Bawacha) limetangaza maandamano kwenda Ikulu kumuomba Rais
Jakaya Kikwete asikubali kutia saini Rasimu ya Katiba inayopendekezwa
iwapo itapitishwa na Bunge.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee alisema jana
kwamba maandamano hayo yatafanyika mwishoni mwa wiki ijayo, baada ya
maandalizi yatakayofanyika kwa siku saba kuanzia jana kukamilika.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, alisema baraza
hilo limeamua kuitisha maandamano hayo ili kuwakilisha kilio cha
wanawake ambao ndiyo waathirika wa kwanza pale nchi inapokuwa katika
mfumo usio wa haki.
Alivitaka vyombo vya dola hasa polisi kujitokeza
kuwasindikiza na kuandamana nao kwa kuwa nao ni miongoni mwa Watanzania
ambao wataathiriwa na uamuzi usiolenga kujenga umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Polisi imetahadharisha kuwa itaendelea
kuwachukulia hatua za kisheria wanachama wa Chadema watakaojiingiza
katika maandamano yaliyopigwa marufuku nchini. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alisema, “Kauli
yetu haijabadilika, maandamano ya Chadema ni batili. Yeyote
atakayeandamana atakuwa anakiuka utii wa sheria bila shuruti. “Jukumu
letu ni kuwalazimisha wote wasiotaka kufanya hivyo, kuitii kwa shuruti.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum
amewataka Watanzania kutokuwa na papara ya kupata Katiba Mpya kwani
mwisho wa siku wenye uamuzi wa kutaka iwe ya namna gani ni wao.
“Ni vyema na busara Watanzania wakasubiri na
kuliachia kazi Bunge hilo Maalumu ambalo linamaliza kazi hivi karibuni
na wao kubaki na kazi ya kuchagua wanachokitaka kiwemo kwenye katiba
hiyo.
Maandamano yazimwa
Polisi wamedhibiti wafuasi wa Chadema maeneo
mbalimbali waliokuwa wamejipanga kufanya maandamano na wengine
wamefikishwa kortini.
Wanachama zaidi ya 40 wa Chadema eneo la Mbalizi,
Mbeya Vijijini walikumbana na virungu vya polisi muda mfupi baada ya
kuanza maandamano katika Mtaa wa Z.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi alisema hakuwa na taarifa yoyote lakini angependa wakazi wa
Mbeya wafikirie zaidi masuala ya elimu, biashara na kilimo kuliko siasa.
Katavi
Viongozi watatu na wafuasi 14 wa Chadema Mkoa wa Katavi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
Wanachama hao walikamatwa jana saa nne asubuhi
eneo la Zahanati ya Kasimba katika Mtaa wa Majengo A, wakiwa
wanaandamana kwenda Viwanja vya Hoteli ya Mpanda walikopanga kufanya
mkutano.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri
Kidavashari alisema wanaoshikiliwa ni: Katibu wa Chadema wa Mkoa,
Almasi Ntije, Mwenyekiti Wilaya ya Mpanda, Abraham Mapunda na Katibu wa
Jimbo la Mpanda Mjini, Cretus Nkumba.
13 wanaswa Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino
Mlowola amesema wanawashikilia watu sita baada ya kukutwa wamejikusanya
katika makundi jambo lilioashiria walitaka kuandamana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza,
Adrian Tizeba alisema wanaoshikiliwa ni wanachama 13 na viongozi wao.
Aliwataja baadhi ya viongozi wanaoshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa
Chadema Vijana Mkoa, Joseph Idd, Mwenyekiti Wilaya ya Nyamagana,
Josephat Nungwana na Katibu wa Vijana Wilaya ya Ilemela ambaye
hakumtaja.
Dar es Salaam
Wafuasi 12 Chadema wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio
halali kwa nia ya kuandamana.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola aliwataja
washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi kuwa ni Paulo Stanley
‘Ndege’, Joseph Michael, Ajenta Emmanuel na Waziri Saidy ‘Mahunzi’.
Wengine ni Oldgard Lerio, Sifa Majura, Magreth
Mapunda, Remina Peter, Stella Masanja, Mwanahamisi Hassani, Vaileth
Seka na Sina Manzi.
Kongola alidai mahakamani kuwa juzi katika maeneo
ya Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ilala Boma walifanya
mkusanyiko usio halali kwa nia ya kuandamana kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, washtakiwa wote
walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umekamilika.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 8. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment