Wednesday, September 18, 2013

TANZANIA YAMEGWA EAC

*Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi zaungana kuunda Shirikisho la Kisiasa
*Waziri Sitta asema zina ajenda ya siri, ashangaa marais kuwaburuza wananchi wao

HATIMAYE Tanzania imewekwa kando rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza nchi hizo.

Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.

Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda, James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo jipya.

Gazeti la The Sunday Times la Rwanda, limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.

Musoni ambaye alikiri kushiriki katika mkutano wa marais hao ulioshirikisha pia maofisa waandamizi wa nchi hizo isipokuwa Tanzania, alisema uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ambao ni wa pili kufanyika, ni moja ya maagizo ya uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika pia mjini Kampala.

“Tumekubaliana juu ya kanuni za kisheria na mpango mzima utakaotuongoza ili kupata Rasimu ya Katiba itakayoliongoza shirikisho hilo la kisiasa,” alikaririwa Musoni.

Alieleza kuundwa kwa kikosi kazi maalumu kitakachojulikana kwa jina la High Level Task Force (HLTF), ambacho kitajumuisha wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaoandika Rasimu hiyo kwa namna ile ile ya ulivyoandaliwa mpango wa Itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Musoni alisema mawaziri wa nchi wanachama waliopangiwa kushughulikia shirikisho hilo, wanatarajiwa kuelezea mwelekeo wa mafanikio ya mpango huo katika mkutano mwingine uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba huko Kigali Rwanda.

Kwa mara ya kwanza, marais Kagame, Museveni na Kenyatta walikutana kufikia makubaliano ya kuharakisha uundwaji wa shirikisho la kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya kiuchumi na kuweka hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa kibiashara sambamba na kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya Mombasa.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...