Wednesday, September 18, 2013

MADEREVA WA BODABODA DAR WAUA JAMBAZI

MAJAMBAZI wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti Dar es Salaam akiwamo mmoja aliyeuawa na madereva wa pikipiki katika eneo la Vingunguti karibu na kituo cha mafuta. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa majambazi wapatao wanne walimvamia mfanyabiashara Abas Mussa (47) wa Vingunguti wakiwa na bunduki na mapanga.

Alisema mfanyabiashara huyo akiwa dukani kwake, ghafla walifika vijana wawili, mmoja akiwa na bunduki fupi na mwingine akiwa na panga na kumpora mwenye duka Sh 1,400,000.

Pia walimpora simu moja ya Nokia na ufunguo wa gari na alipotoka nje ya duka alisikia mlio wa bunduki na kumuona mfanyakazi wake Ally akiwa chini na watu wengi wakiwa wamejikusanya.

Alisema baada ya tukio hilo kutokea madereva wa pikipiki waliwaona majambazi hao na kuwafukuza na walipofika njia panda ya Tabata Relini walimkamata jambazi mmoja na kuwashambulia hadi kumjeruhi.

Kamanda alisema polisi walipata taarifa na walipofika eneo la tukio walimkuta jambazi huyo akiwa na hali mbaya. Walimchukua na kumpeleka hospitali lakini alifariki dunia akiwa njiani.

Alisema jambazi mmoja alikimbia baada ya kuacha pikipiki ya Sunlag na polisi waliweza kuwakamata waliokimbia baada ya tukio hilo.

Katika tukio jingine, jambazi mmoja aliuawa na polisi wakati majambazi sita walipojaribu kupora mamilioni ya fedha katika mtaa wa Jamhuri Kitumbini.



Alisema watuhumiwa hao walikuwa na pikipiki ya Boxer na wakiwa katika jaribio hilo waligundua kuwapo polisi katika eneo hilo.

Kamanda alisema walipojaribu kutoroka kuelekea mtaa wa Jamhuri waligonga ubavuni mwa gari ya Noah na kuanguka chini na kila mmoja akawa anakimbia kwa miguu huku wakiwafyatulia askari risasi.

Alisema katika majibiziano ya risasi kati ya polisi na majambazi hao askari mmoja, Daud alijeruhiwa kidole gumba cha mguu wa kushoto wakati jambazi mmoja alijeruhiwa ubavuni upande wa kushoto na alikufa wakati anapelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Maiti ya jambazi huyo ilipopekuliwa ilikutwa na pochi iliyokuwa na kitambulisho cha FINCA chenye jina la Saidi Lukulingwa na nakala ya liseni namba 4000801703 yenye jina hilo iliyotolewa Agosti 31 mwaka 2012, alisema.

Alisema inayoonyesha mmiliki wa vitambulisho hivyo alizaliwa Machi 17 mwaka 1989.

Kamanda alisema pochi hiyo ilikutwa na hirizi tano, karatasi tatu zenye maandishi ya kiarabu, fedha ya shaba yenye tundu katikati inayodaiwa kutumiwa kuleta miujiza ili wasikamatwe na kadi tatu za simu .

Alisema majambazi wengine watano, mmoja kati yao akiwa na bastola, walikimbia huku wakifyatua risasi ovyo na kutoweka kusikojulikana.

Juhudi za kuwasaka majambazi hao zinaendelea, alisema.
MTANZANIA

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...