Wednesday, September 18, 2013

SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA BALOZI WA CHINA ALIYEHUDHURIA MKUTANO NA WA CCM

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imehadharisha mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, kuepuka kujihusisha na mambo ya ndani.

Hadhari hiyo imetolewa jana katika taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari, baada ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Lu Younqing, kuonekana katika mkutano wa hadhara wa CCM, akiwa amevalia kofia yenye nembo ya chama hicho.

“Wizara inaelekeza kwamba kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa, sio sahihi na kinakiuka Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa 
kidiplomasia.

“Mkataba huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi, ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao katika nchi za uwakilishi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo, Mkubwa Ally.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa hata Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986, ambayo ni zao la Mkataba wa Vienna, pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi, kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi.

“Itakumbukwa kwamba, Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa tukio hili Wizara itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,”

“Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha Balozi yoyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia,” alisema Membe katika taarifa taarifa hiyo.

Lu alikuwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM na alikwenda Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba, vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina, Tahong na viwanda hivyo vita kuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.

Balozi huyo amenukuliwa na vyambo vya habari wakati akihutubia mkutano wa hadhara akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kujitahidi kuwasalimia wananchi hao kwa lugha ya kabila la Wasukuma kwa kusema mwadila.

Alisema pamoja na Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, anaamini kuwa CCM bado iko imara na inaweza kuendelea kuongoza kwa muda mrefu.

“Kwa hili inadhihirisha kuwa hakuna chama kama CCM kutokana na uimara wake na hili wanalofanya sasa la kuja kuimarisha chama nasi kule China kupitia chama chetu tawala cha CPC (Chama Cha Kikomunisti cha China), tunafanya kama hivi pia. Mwadila, Shinyanga, CCM Oyeeeeee asanteni sana,” alikaririwa akisema.

Taarifa hiyo ilisema kuwa Balozi huyo alikwenda wilayani humo kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imeelezea kutambua uhusiano mzuri uliopo kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na vilevile inatambua kazi nzuri ambayo BaloziLu Younqing amekuwa akiifanya tangu alipowasili nchini Tanzania.

--- via HabariLeo na NIPASHE

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...