Baada
ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa mwongozo na kuunga mkono uamuzi
wa Naibu wake, Job Ndugai kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema, wasomi,
wanasiasa na wanaharakati wamesema Kiti cha Spika ndiyo chanzo cha
mvutano bungeni kwa kuwa kinapendelea wabunge wa chama tawala (CCM).
Wamesema
licha ya Bunge kuongozwa na kanuni, wakati mwingine viongozi hao wa
Bunge wanatumia kanuni hizo kuwapendelea wabunge wa CCM, huku wakieleza
kuwa licha ya wabunge wa chama hicho kutukana, hawakupewa adhabu yoyote.
Jumatano
ya wiki hii, Ndugai aliwasimamisha Tundu Lissu (Singida Mashariki),
Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini),
Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa
Arusha Mjini kutohudhuria Bunge kwa siku tano kutokana na alichokiita
kufanya vurugu ndani ya Bunge.
Uamuzi
huo wa Spika Makinda ulikuja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kumtaka Ndugai aeleze alitumia kanuni
gani kuwasimamisha wabunge hao.
Licha
ya wabunge hao kupewa adhabu hiyo baada ya kuomba mwongozo wa Spika na
baada ya kupinga mwenzao kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, wapo wabunge
wa
CCM waliotukana na kutoa lugha za kukera lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote.
Wabunge
hao ni Peter Serukamba ambaye alitukana tusi zito la nguoni kwa lugha
ya kimombo wakati ulipozuka mzozo wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa
Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Profesa Kulikoyela Kahigi.
Wengine ni mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera).
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa
Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Bunge la
sasa linakabiliwa na mambo mawili makubwa; la kwanza ni udhaifu wa kiti
cha Spika na pili ni wabunge wa CCM kuamini kuwa Chadema ni maadui
wakati katika hali ya kawaida siasa ni ushindani na ndiyo demokrasia kwa
kuwa sasa tuko katika mfumo wa vyama vingi.”
Alisema kuwa Spika na Naibu wake wameshindwa kudhibiti vurugu bungeni kwa sababu ya kuendekeza itikadi za vyama.
“Kushindwa
huko ndiyo kunachangia vurugu kwa sababu wote wanaegemea upande mmoja,
wabunge wengine wa upinzani hawawezi kukubaliana na hali hiyo na huo
ndiyo mwanzo wa malumbano,” alisema Profesa Mpangala.
Alisema
tatizo jingine ni kitendo cha wabunge wa CCM na chama chao kudhani kuwa
upinzani ni uadui, “Hayo ndiyo matunda ya mfumo wa vyama vingi. Mfumo
huu ni wa ushindani na kuna mambo ya msingi yanayotolewa na wapinzani na
mengine hayana ubaya wowote.”
Mhadhiri
mwingine wa Chuo hicho, Bashiru Ally alisema Spika anaongoza Bunge kwa
ushabiki wa vyama; “Hatuwezi kutenganisha tabia za wabunge ndani na nje
ya Bunge, ila pamoja na hilo bungeni sasa kuna ushabiki wa vyama.”
Alisema
hali hiyo inasikitisha kwani licha ya kuongezewa posho wabunge sasa
wamegeukia malumbano badala ya kujadili mambo ya msingi.
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholas
Mgaya alisema kuwa viongozi hao wa Bunge wanafanya uamuzi bila kufuata
kanuni za Bunge.
“Hatuwezi
kuwalaumu wabunge kwa sababu wanaowaongoza wameshindwa kusimamia kanuni
hivyo wanajua wazi kuwa hata wakifanya ndivyo sivyo hakuna hatua zozote
watakazochukuliwa,” alisema Mgaya.
Kaimu
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila
alisema Bunge limekosa usimamizi mzuri, huku akifafanua kuwa limeshindwa
kuwachukulia hatua wabunge wa CCM ambao wanatumia chombo hicho cha
kutunga sheria kujizolea umaarufu.
“Wabunge
watatu wa CCM walitukana, lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote ila
wabunge wa upinzani walioomba miongozo wamechukuliwa hatua ikiwa ni
pamoja na kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, hii si sawa” alisema.
Mwenyekiti
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen-Kijo Bisimba
alisema; “Inaonekana wabunge hawajui cha kufanya wala kilichowapeleka
bungeni.”
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alisema
kuwa moja ya mambo yaliyotakiwa kujadiliwa na wabunge hao ni pamoja na
madai ya walimu ya muda mrefu.
“Walimu
wanaidai Serikali Sh25 bilioni, kuna suala la kutokuwapo kwa mitalaa,
haya yote hawayaoni wanaishia kutupiana vijembe tu,” alisema Oluoch.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema wabunge
wanatakiwa kutambua kuwa wapo bungeni kwa fedha za wananchi, hivyo
wanatakiwa kulipa fadhila.
“Wananchi
wanawategemea wabunge wasimamie haki na usawa na kujenga hoja za
kutetea masilahi yao, naona 2015 ndiyo uwe muda wa wananchi kuchagua
anayewafaa,” alisema Profesa Ngowi.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amekitaka kiti
cha Spika wa Bunge kufuata sheria, haki, kanuni na miongozo ya kibunge
na si kuegemea upande mmoja kwa mustakabali wa kulinda heshima ya
taasisi hiyo nyeti kwa taifa.
Pia
amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwakutanisha viongozi wote wa
Bunge kutoka pande zote ili kutafuta mwarobaini wa kile kinachoendelea
hivi sasa bungeni.
Profesa
Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema kinachoendelea
bungeni kinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
“Kinachotokea
bungeni ni matokeo ya kiti cha Spika kutokutenda haki na wakati
mwingine kimekuwa kikiegemea upande mmoja jambo ambalo linafanya
kipoteze mwelekeo,” alisema Profesa Lipumba
Alisema
kiti hicho kinatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Bunge na
kutokufuatwa kwa vitu hivi, matokeo yake ndiyo haya tunayoyashuhudia
sasa, lugha chafu zinazodhalilisha utu wa binadamu.
Mwenyekiti
huyo alisema wabunge wanatakiwa kuwawakilisha wananchi wao ipasavyo na
kuepuka kujiingiza katika mambo yasiyokuwa na tija kwa wapiga kura wao.
Makinda
juzi alilazimika kutoa mwongozo baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kumtaka aeleze, Ndugai alitumia kanuni
gani kuwasimamisha wabunge hao.
Baada
ya kipindi cha maswali na majibu, Alhamisi iliyopita, Mbowe alisimama
na kuomba mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 68(7) .
SOURCE::MWANANCHI::
No comments:
Post a Comment