POLISI WADAIWA KUMFANYIA UNYAMA KADA WA CHADEMA
HATIMAYE
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba,
amekiri kuhusika na video inayomwonesha Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Nchemba
amekuwa akitajwa na viongozi wa CHADEMA kuwa anahusika kutengeneza
video hiyo, kwa kuwa aliwahi kutamba wakati akihojiwa na kituo kimoja
cha televisheni kuwa anayo video inayowaonesha viongozi wa chama hicho
wakipanga mauaji.
Hata
hivyo, tangu Nchemba atoe kauli hiyo Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi
lilikaa kimya hadi Machi 12 lilipomkamata na kumhoji Lwakatare, siku
moja baada ya video hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa You tube na mtu
anayejiita ‘Bukoba Boy’.
Akizungumza
na gazeti hili kwa simu jana, Nchemba alikiri kuwa ndiye aliyeipeleka
video ya Lwakatare polisi na kwamba alifanya hivyo baada ya kuripoti
kuandikiwa ujumbe wa simu wa kutishiwa maisha na baadhi ya viongozi wa
CHADEMA.
“Niliwapelekea
mimi hiyo video polisi na wakati nasema kwenye televisheni nilikuwa
tayari nimewapa. Na pale nilisema makusudi baada ya Zitto Kabwe kudai
kuwa mwaka jana kulitokea mauaji mengi, ndipo nikataka kumuonesha kuwa
chama chake kinahusika na mikakati hiyo,” alisema.
Alipoulizwa
aliipataje video hiyo na kwanini hajahojiwa polisi ili kutoa
uthibitisho wa uhalali wake, Nchemba alisema: “Kuna msamaria mwema
aliniletea.”
Nchemba
alipobanwa ana uhakika gani kama video hiyo ina ukweli, alijibu kuwa:
“Ile huhitaji akili kubwa kutambua uhalisia wake. Suala la Lwakatare
CHADEMA wakubali tu na wajitokeze hadharani kwenye makanisa na misikiti,
watubu na kuomba radhi kwa umma.”
Hata
hivyo katika kile kinachoweza kuongeza mashaka ya Nchemba kuhusishwa
kutengeneza video hiyo, alikwenda mbali zaidi akitoa hata siri za
polisi, akisimulia maelezo aliyodai kuwa ndiyo yalitolewa na Lwakatare
wakati akihojiwa na polisi.
“Pale
video inaonesha ni nyumbani kwake, tena jikoni na hilo amekiri katika
maelezo yake polisi. Pia amekubali kuwa siku hiyo alipiga chafya kama
inavyoonekana. Sasa wewe mwandishi unatetea nini wakati yeye amekiri
polisi kila kitu kilichomo mle,” alisema.
Maelezo
ya Nchemba yalionekana kumtia hofu mmoja wa mawakili wa Lwakatare,
ambaye alikuwepo wakati wote wa mahojiano polisi, Nyaronyo Kicheere,
akidai kuwa ni wazi jeshi hilo linafanya kazi ya propaganda za CCM.
“Nchemba
hakuwepo wakati Lwakatare akihojiwa na hata baadhi ya wanasheria katika
kesi yake ya ugaidi inayomkabili hawajui alichokisema polisi, sasa huyo
amepata wapi siri za polisi kama si mchezo unachezwa?” alihoji.
Kuhusu
mahusiano yake na mshtakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, Ludovick
Joseph, ambaye anadaiwa na baadhi ya watu kuwa ndiye aliyerekodi video
hiyo, Nchemba alisema walifahamiana kupitia mtandao wa kijamii wa
facebook.
Alipotakiwa
kufafanua ukaribu wao hadi kufikia hatua ya kumtumia fedha kwa njia ya
M-Pesa kupitia simu yake, Nchemba alisema: “Mimi nilimtumia kama
ninavyowapa watu wengine hata wa CHADEMA.
“Mimi
sijui kama Ludovick ndiye alirekodi video hiyo, wala sikuwahi kumtuma
kufanya hivyo na fedha niliyomtumia si kwamba nilikuwa nikimlipa ujira.
Kwani unaweza kumpa mtu sh 50,000 tu kwa kazi hiyo?” alihoji.
Tanzania
Daima lilipotaka kufahamu kama anahusika kushirikiana na vyombo vya
dola kuwarubuni baadhi ya vijana wa Makao Makuu CHADEMA kwa fedha ili
watumike kutoa ushahidi wa kumwangamiza Lwakatare mahakamani, Nchemba
alisema: “CHADEMA haijawahi kuongoza serikali, hivyo hawajui mikono ya
serikali.”
Alipotakiwa
kufafanua kikao baina yake na vijana hao kilichofanyika katika Hoteli
ya Sea Cliff ya jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita na
kisha kuwatumia fedha kwa njia ya M-Pesa, Nchemba aling’aka na kuuliza:
“Hiyo Hoteli ya Sea Cliff iko wapi? Maana sipajui na sijawahi kufika.”
Mwishoni
mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mambo ya Katiba wa CHADEMA, Tundu
Lissu, alifichua njama zinazofanywa ili kutengeneza ushahidi wa uongo
kwa ajili ya kuutumia katika kesi ya ugaidi inayomkabili Wilfred
Lwakatare.
Lissu
alidai kuwa njama hizo zinafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya usalama na ujasusi ili kutumia ushahidi huo
mahakamani dhidi ya Lwakatare.
Alisema
kuna baadhi ya vijana wa CHADEMA wa Idara ya Ulinzi na Usalama
wanaopewa fedha na kuahidiwa kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi
hiyo ya Lwakatare.
Lissu
alisema kuna baadhi ya vijana wakiongozwa na Saumu Mulugu, ambaye
alifukuzwa kazi CHADEMA mwanzoni mwa mwaka jana, wamepokea fedha kutoka
kwa kigogo mmoja wa CCM (jina linahifadhiwa) ili kufanikisha mpango huo.
Lissu
alisema hadi sasa vijana hao wameshapewa sh 400,000 ili wakubali kwenda
kufundishwa jinsi ya kuzungumza mahakamani kuwa CHADEMA ni chama cha
kigaidi, kwamba Lwakatare alipanga mikakati ya kigaidi.
“Awali
walipewa sh 400,000, wakapewa tena sh 300,000, pia wakapewa sh 35,000
mara mbili. Na fedha zote hizi walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,”
alisema Lissu.
Alidai kuwa Saumu ndiye anayeratibu mpango wote kati ya Jeshi la Polisi na vijana hao wa CHADEMA kwa kuwarubuni kwa fedha.
Alisema
vikao baina ya vijana hao wa CHADEMA na Saumu vimewahi kufanyika mara
kadhaa katika moja ya hoteli maarufu nchini juu ya mambo ya kwenda
kuzungumza kwenye vyombo vya habari au mahakamani kwenye kesi ya
Lwakatare.
Siku
moja baada ya madai ya Lissu, gazeti hili lilimnasa Saumu akiwa
anawasiliana na wenzake, huku akiwatuhumu baadhi yao kuwa ndio
waliovujisha siri kwa Lissu.
Vilevile
alionekana akiwasiliana na kigogo mmoja wa CCM ambaye alikuwa akimwita
‘mkuu’ huku akimsomea baadhi ya taarifa zilizoandikwa magazetini jana
yake kuhusu kuvuja kwa siri zao.
Saumu
akiwa katika grosari karibu na baa maarufu kwa jina la Kwa Kimaro,
jirani na eneo la Benki Kuu ya Damu Salama, Mchikichini jijini Dar es
Salaam, alisikika akiwalalamikia wenzake kwa kumsaliti na kuvujisha
mkakati wao kwa Lissu.
“Kwanini
mmelikisha siri zetu kwa Lissu hadi amejua tulikutana katika hoteli ya
kifahari na Mwigu…? Sasa nitawaonesha, maana laki tano zenu ninazo mimi.
Siwapi bali nitazitumia kujilinda,” alitamba.
Saumu
ambaye alikuwa akizungumza kwa sauti kubwa ya ghadhabu kupitia simu,
aling’aka: “Nyie kwanini mmeniuza kwenye ishu ambayo tumeipanga wote?”
Baada
ya kupokea maelekezo kutoka kwa ‘mkuu wake’ aliendelea kupiga simu
akimlalamikia mtu ambaye hakumtaja, kuwa alikuwa amezima simu yake
makusudi kwa kuwa ndiye alivujisha siri zao kwa CHADEMA.
“Mimi
sitakubali na nimehakikishiwa na bosi wetu kuwa huyo aliyetusaliti
tutatumia wale askari kumwekea hata unga. Haiwezekani fedha tumepokea za
kwanza, za pili na tatu kwanini tuuzane dakika za mwisho?” alidai Saumu
huku akiendelea kugida bia yake.
Huku
akihaha huku na kule, Saumu alikuwa akiwapigia simu baadhi ya madereva
wa CHADEMA makao makuu na kuwaomba simu za baadhi ya watu, na hata
wakati mwingine kuwafokea akidai ndio waliofichua siri hiyo.
Hata
hivyo, baada ya kutilia shaka nyendo za chanzo chetu kudaka siri zake,
ghafla alitokomea na kuzima simu zake mara moja kwani hata alipotafutwa
baadaye hakupatikana hadi leo.
Polisi wafanya unyama
Katika
hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limemkamata kada wa CHADEMA
mjini Bukoba, Evodius Justinian na kumshikilia kwa siku kadhaa kisha
kumsafirisha hadi jijini Dar es Salaam huku akipewa mateso makali ya
kulazimishwa akubali kutengeneza video ya Lwakatare.
Justinian
(30), ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA)
mjini Bukoba, alikamatwa Jumanne ya wiki iliyopita akidaiwa kukabiliwa
na makosa ya jinai.
Alishikiliwa
kwa siku mbili mfululizo kabla ya kumsafirisha kwenda wilayani Igunga,
Tabora ambako alidaiwa kuwa alitenda makosa hayo ya jinai lakini
alifichwa jijini Mwanza.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi hakutaka kulizungumzia kwa
undani suala hilo lakini aligusia kuwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka
ya kushambulia na kujeruhi mtu huko wilayani Igunga.
Hata
hivyo, kada huyo alisafirishwa hadi uwanja wa ndege wa jijini hapa
juzi, lakini akanyang’anywa simu na kukatazwa kuzungumza na ndugu zake.
Taarifa
za kada huyo kuletwa jijini hapa zilikuwa za kificho kwani wakili wake
Nyaronyo Kicheere akiongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walifika Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuelezwa kuwa amepelekwa makao makuu.
Walipofika
makao makuu kumwona na kumpatia chakula, polisi walisema hawana mtu
kama huyo, hivyo wakarudi tena Kanda Maalumu walipohakikishiwa kuwa yuko
makao makuu.
Akizungumza
mbele ya wakili wake, Kicheere, mtuhumiwa huyo alieleza unyama
aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na
jijini hapa.
Katika
maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate
Nyombi, Justinian alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri
bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila
kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Alieleza
kuwa wakati wote wa mahojiano hayo alikuwa akilazimishwa kukiri
kurekodi video ya Lwakatare inayoonesha mikakati ya ugaidi.
Alisema
alisafirishwa kwa siri kwa ndege hadi Dar es Salaam, akapelekwa chooni
na kumpiga, kutishiwa na kuteswa kwa nyaya za umeme na kumnyima fursa ya
kupewa chakula.
Justinian ambaye anaendelea kushikiliwa na polisi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Kabla
ya maelezo hayo, Kicheere akiwa na Uloleulole Juma Athumani, ambaye ni
ndugu wa Justinian, alijitambulisha kwa Nyombi akimweleza kuwa walikuja
kuonana na mteja wake pamoja na kumletea chakula.
Hata hivyo, Nyombi alisema hakuwa na habari za kukamatwa kwa kada huyo na kwamba angekuwa amelimaliza mapema suala hilo.
Kada
huyo alisimulia unyama aliofanyiwa akisema: “Nimepigwa na polisi nikiwa
Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa
huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini
Igunga.
“Nikiwa
Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia
pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa,
niliomba kuwa na wakili wakanikatalia,” alisema.
Aliongeza
kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya
Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick lakini akapigwa
makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama
kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video
ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa
nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera
tarehe 4 Aprili,” alisema.
Justinian
aliongeza kuwa hakula chakula chochote cha polisi kwa kuwa hawaamini,
ila kuhara kulipozidi alikubali kula chakula chao.
Wakili
Kicheere alisema ni makosa makubwa sana kumtesa mtu kwa kipigo na
vitisho vya umeme na kwamba hayakubaliki hata mahakamani.
“Polisi hawakutaka nionane naye kwa makusudi hadi walipomaliza kumhoji na kumtesa ndipo wakaniruhusu,” alisema.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment