Serikali
imesema itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga
nidhamu na kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua
tovuti ya www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa
njia ya mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo
Mulugo ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya
wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo
kienyeji.
“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa na wageni waalikwa.
Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika masomo yao... “Tovuti kama hiyo ingewasaidia kwa masomo, lakini wao wanakimbilia kwenye facebook na mambo mengine yasiyofaa.”
Aliyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali na haki za binadamu ambayo yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
“Simu tunazipiga marufuku, mwalimu akimkuta mwanafunzi na simu amnyang’anye ndizo zinatuharibia taifa letu.” Aliwapongeza wabunifu wa mtandao huo akisema ni wazalendo kwani wamekuwa msaada katika jitihada za Serikali kukuza elimu nchini.
“Watu wanapiga kelele Mulugo na Kawambwa wajiuzulu, hata tukijiuzulu haitasaidia, bali kila Mtanzania atoe mchango wake katika elimu ili kuweza kuiendeleza.”
Mwanzilishi wa tovuti hiyo, Faraja Nyalandu alisema itakuwa na manufaa kwa wanafunzi wa Tanzania kwani masomo yanayotolewa yanaandaliwa na walimu wazoefu wenye shahada hivyo wanafunzi watakapoitumia watapata manufaa makubwa.
Maoni ya wadau
Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Waziri Kivuli wa Elimu Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo aliitaka iache kuangalia mambo madogo ambayo yanachangia kwa kiasi kidogo tu kudorora kwa elimu na kuacha mambo makubwa.
“Kuna
mambo makubwa zaidi yaliyotufikisha hapa tulipo, hii ni sawa na
kushughulika na matawi na kuacha mizizi. Lazima tuangalie suala hili
kwa upana zaidi, kuna ripoti nyingi na nzito hazijafanyiwa kazi mpaka
sasa badala yake Serikali inaibuka na kuanza kutangaza vitu vidogo kama
hivyo, wafanyie kazi kwanza ripoti ambazo zilitumia pesa nyingi za
walipakodi kwani nyingi zina mapendekezo mazuri.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa, Rukonge Mwero alisema uzuri wa adhabu ya viboko ni kwamba haipotezi muda”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema adhabu ya viboko haina maana katika kipindi hiki akisema wanafunzi wanapaswa kupewa adhabu ambazo zinawafundisha kama zile za kufanya usafi na kazi mbalimbali.
“Viboko havifundishi zaidi ya kumpatia mwanafunzi maumivu na kusababisha aichukie shule. Waelimishwe kwa kuelekezwa lakini wakiendelea kukiuka, wapewe adhabu za kufanya kazi mbalimbali.
Rais
wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema walimu
hawapati faida yoyote kuwachapa au kutowachapa viboko wanafunzi.“Hawa
viongozi kila kukicha wanazungumza mambo yasiyo na maana, badala ya
kuzungumzia masilahi ya walimu wanazungumza kuhusu viboko, hatuelewi
wakiamka kesho watasema nini,” alisema Mukoba.
Na MWananchi
No comments:
Post a Comment