Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.
Padri
Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa
kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini
hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili
katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada
ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha
maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa
mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar
Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi
wa NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa
mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea
kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa mujibu wa
uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa
juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa
dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la
Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa
ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba
mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo cha
habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na
uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa
watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman
aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba 17, mwaka
jana.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa
Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada la
mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari kumtafuta DPP
azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na uchunguzi wa
Polisi.
Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la Polisi
bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa kushirikiana na FBI hauna
shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na
wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu
wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni kuchunguza kesi na ofisi ya
DPP jukumu lake ni kufungua hati ya mashtaka na kutetea kesi mahakamani.
Hata
hivyo, NIPASHE ilipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake
alisema amepokea maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote wa
habari wanaofuatilia suala hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile
kazi aliyopewa ya kupitia jalada la uchunguzi kabla ya kufungua kesi
ameikamilisha.
“Kamishna ndiye aliyeitisha mkutano
na waandishi wa habari kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na kukamatwa
kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua
iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi kurejesha jalada la mauaji,” alisema
Katibu muhtasi huyo.
Katika hatua nyingine, Naibu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Yusuph Ilembo, jana alifika
katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia ombi lililofunguliwa
mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa wa mauaji, Abdallah Juma
Mohamed.
Abdallah Juma amefungua ombi katika
Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha sheria 390 cha sheria namba 7 ya
mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004, akitaka Jeshi la Polisi litoe
maelezo kwa nini mteja wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24
tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu.
Wakili
Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na Shaibu
Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa mteja
wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Ilembo alisema kuwa
kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa kutayarisha
majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha kwa upande wa
utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo kuanza kusikilizwa
na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa
upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema baada ya
kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa maandishi
hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo
Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji alisema wakati
wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo afikishwe
mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea kutaka
dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa tuhuma
za mauaji.
Kutupwa kwa uchunguzi wa jalada la
mauaji hayo pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya Polisi
kunadhihirisha kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi
Zanzibar na ofisi ya DPP.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment