Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtuhumu Waziri wa Uchukuzi,
Dk Harrison Mwakyembe kwamba alitoa zabuni ya ujenzi wa bandari ya
nchikavu kwa kampuni inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinyume
cha sheria za ununuzi. Chadema
walisema jana kwamba, kampuni hiyo ni Jitegemee Trading Company ambayo
ilipewa zabuni ya ujenzi wa bandari katika Viwanja vya Sukita pasipokuwa
na mchakato wa kushindanisha kampuni nyingine.
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema:
“Mwakyembe aseme alitoa zabuni hiyo kwa Jitegemee kwa kuzingatia vigezo
gani? Kampuni ngapi zilishindanishwa katika mchakato huo na asipofanya
hivyo hastahili kukaa wizarani hapo bali alipelekwa Segerea gerezani
kwani ni kosa kubwa kutoa zabuni kinyemela.”
Kigaila
alituhumu mradi huo ulitakiwa kujengwa ndani ya Halmashauri ya Temeke,
lakini katika hali ya kushangaza CCM waliamua kuhamishia Bonde la
Msimbazi.
“Kampuni
hiyo tayari imetengewa Sh10 bilioni katika bajeti ya 2013/14
itakayosomwa bungeni, itakuaje Serikali inawafukuza watu kuishi
mabondeni, lakini wao wanapeleka mradi huo bondeni?
Kigaila
alidai kumshangaa Dk Mwakyembe kwa kubadilika na kutoa zabuni kwa
kampuni, ambayo haijafanyiwa upembuzi yakinifu wakati waziri huyo
aliwahi kuibeza Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond wakati akiwa
Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge 2007.
“Mnakumbuka
Dk Mwakyembe alidai Richmond haikufanyiwa upembuzi yakinifu na kutaka
ipokonywe tenda, kwa nini leo hii anatoa zabuni kwa kampuni ya chama
chake bila kuitangaza?”alihoji.
Alipotafutwa
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM
watafuatilia ukweli wa jambo hilo. “Nipe muda nifuatilie huko Jitegemee
ili kujua tenda ilivyotolewa ilikwenda wapi,” alisema Nape.
Naye
Meneja wa Kampuni ya Jitegemee, Esther Nyawazwa alisema wizara ilileta
maombi ofisini kwao na baada ya hapo mawasiliano yaliendelea kupitia kwa
Mwenyekiti wa Bodi, Peter Machunde.
“Wizara
ilileta `application’ (maombi) ya zabuni ofisini kwetu ya kuomba
kujenga mradi wa kituo pale kwenye Bonde la Msimbazi na baada ya hapo
mawasiliano yaliendelea kati ya wizara na mwenyekiti wa bodi, kwa hiyo
sasa sifahamu maendeleo ya mradi,” alisema Nyawazwa na kuongeza:“Mimi
jukumu langu ni kutekeleza niliyoagizwa, hivyo ninashauri uwasiliane na
mwenyekiti wa bodi kwa ufafanuzi zaidi.” Alipotafutwa kupitia simu yake
ya kiganjani, Machunde hakupatikana kwani ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Habari na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Chanzo - Mtanzania
No comments:
Post a Comment