Na: Godfrey Kahango, Mbeya
Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Mbeya imewanasa walimu
wawili wa Shule ya Sekondari ya Forest kwa tuhuma za kushawishi na
kupokea rushwa ya kati ya Sh500 na Sh1,000 kwa wanafunzi wanaochelewa
asubuhi. Imeelezwa kwamba kutokana na mtindo huo, walimu hao wamekuwa
wakijikusanyia wastani wa Sh150,000 kwa siku. Walimu hao walikamatwa saa
8.30 mchana jana shuleni hapo baada ya baadhi ya wanafunzi kutoa
taarifa Takukuru za kuwapo kwa tabia hiyo ya kulazimishwa kutoa fedha
wanapokuwa wamechelewa kufika shuleni asubuhi. Kamanda wa Takukuru wa
Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka, aliwaambia waandishi wa habari ofisini
kwake kwamba walimu hao
(majina tunayo), walitiwa mbaroni wakati wakiwatoza wanafunzi hao fedha hizo.
Hadi
wanakamatwa, walimu hao walikutwa na kiasi cha Sh64,000 walizokuwa
wamezikusanya kutoka kwa wanafunzi hao, huku pembeni kukiwa na rundo la
fimbo lililokuwa likitumika kuwachapa.
Mtuka
alisema waligundua kuwa walimu hao walikuwa wanatengeneza kiasi cha
150,000 kwa siku kutokana na wastani wa wanafunzi 300 waliokuwa
wanawachapa. Shule hiyo ina wanafunzi 900.
“Walimu hao
wamekuwa na mradi huo wa kuwalipisha wanafunzi na wanaoshindwa kulipa
walikuwa wanachapwa viboko visivyokuwa na idadi,” alisema na kuongeza:
“Kwanza
walimu hao walikuwa wanachukua majina ya wanafunzi waliochelewa kutoka
kwa walimu walioko zamu na kuanza kuwaita kwenye chumba walichokuwa
wanakiita ‘Gwantanamo’ na kutoza fedha hizo.”
Walimu hao
walichukua jina hilo kutoka Kambi ya Guantanamo Bay iliyoko karibu na
Kisiwa cha Cuba, ambako Marekani imeweka kambi ya kijeshi.
Kambi
hiyo ilianzishwa Januari, 2002 wakati Marekani ikiwa chini ya George
Bush kwa ajili ya kuhifadhi mateka wa kivita kutoka Afghanistan na Iraq.
Kwa nyakati tofauti, wanafunzi walisimulia vituko vya walimu hao.
Mwanafunzi
wa kidato cha kwanza, (jina tunalihifadhi), alisema kuwa mwanafunzi
ambaye alikuwa hana fedha za kuwapatia, alikuwa anaambiwa kuweka kichwa
chini, miguu na miguu juu kisha mwalimu huyo anamchapa kwenye makalio
hadi sehemu unapopita uti wa mgongo.
“Baada ya
kuona vitendo hivyo vinaendelea, huku uongozi wa shule ukiwa umekaa
kimya, tukaamua kuwaambia viongozi wa serikali ya wanafunzi na ndiyo
waliokwenda Takukuru,” alisema.
No comments:
Post a Comment