Tuesday, March 26, 2013

NGUMI ZITAPIGWA BUNGENI: NDESAMBURO

MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, (CHADEMA), amewataka Watanzania watarajie mapanbano makubwa zaidi bungeni, hata ikibidi ngumi kupigwa, ili kuleta ustaarabu na kutetea haki ya kidemokrasia katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Ndesamburo ambaye amekuwa bungeni tangu mwaka 2000, alisema hayo jana katika mahojiano mafupi na gazeti hili, ofisini kwake Moshi Mjini.
Alisema nyakati zimebadilika na wabunge wa mwaka 2013 si sawa na wa mwaka 2000; kwani hawa wa sasa hawako tayari kuona kanuni zinavunjwa waziwazi.
Ndesamburo alikuwa akizungumzia kauli ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, na Naibu wake, Job Ndugai, ambao wanadai kuwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA ni vinara wa fujo bungeni.
Alisema siasa za sasa ni za vijana, si za wazee kama ilivyokuwa huko nyuma na kwamba wazee wanapaswa kuelewa kuwa nyakati zimebadilika.
Alisema kwamba katika siasa za kuelekea mwaka 2015, CHADEMA ina nafasi kubwa ya kushinda ili kuwaletea Watanzania maendeleo waliyokosa kwa miaka zaidi ya 50.
Alisema: “Lazima tujifunze kubadilika, hizi ndizo siasa za wakati huu. Watu wasidhani vijana hawa wa CHADEMA, hata vijana wa CCM… maana yake kitu kimoja ambacho nimekiona, kama tunajaribu kufikiria sasa, watu wasidhani ni CHADEMA… lakini kule ndani mpaka vijana wa CCM wanafanya vurugu. Ukitazama ile filamu iliyoletwa na TBC ilionyesha CHADEMA tu haikuonyesha upande wa CCM walioshangilia, haikuonesha kabisa; jambo ambalo si sahihi.
“Kwa hiyo watu wajifunze kwenda na wakati. Zamani Bunge lilikuwa limetawaliwa na wazee. Sasa kuna vijana. Vijana ni tofauti na wazee. Lazima wazee waanze kujua vijana wanataka nini. Sheria na kanuni zinazoendesha Bunge, vijana wanazijua, zinapovunjwa ni rahisi kuelewa. Zamani hakuna aliyekuwa anajali hilo.
“Hizi fujo ni demokrasia. Bunge linashika hamasa, limekuwa zuri. Wala wasione haya. Hii ni mwanzo tu, tutaona mengi hata ngumi zitapigwa mle ndani. Ndiyo ustaarabu, hilo ndilo Bunge. Unaponyimwa haki yako, unataka mtu afanyeje?”
Katika Bunge la Februari, Bunge lilitawaliwa na fujo, baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, na Naibu Spika, Job Ndugai, kuliendesha Bunge kinyume cha kanuni na kusababisha kuzomewa na wabunge wa upinzani waliodai Spika na naibu wake wanapinda kanuni.
Mjadala mkali ulianza wakati wa kujadili hoja binafsi za mbunge wa Ubungo, John Mnyika, mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia. Uongozi wa Bunge uliahirisha shughuli za Bunge mara kadhaa baada ya hali ya kutoelewana na ubishi mkali kutokea ndani ya Bunge.
Akizungumzia hali hiyo, Makinda alinukuliwa akisema, “Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza heshima yake ya kibunge.”
Alisema hoja binafsi za wabunge zinaongozwa na kanuni za Bunge kuanzia kanuni ya 53 hadi 58, na kanuni za majadiliano zinaongozwa na kanuni kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa vurugu haiwezi kutokea bungeni.
Makinda ambaye alionekana kuzungumza kwa jazba, alisema katika mkutano huu imeonyesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya kupotosha wananchi wanatumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya kanuni hizi hawazifahamu.
Ubabe huo wa Spika na naibu wake ulisababisha kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2010, wabunge wa vyama vya upinzani kuungana kumsusa Spika na Naibu Spika, wakipinga hatua yake ya kupindisha hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani.
Wabunge wa vyama vya upinzani waliotoka kupinga ubabe wa Spika kinyume cha kanuni ni wa vyama vya CHADEMA, CUF, UDP, TLP na NCCR-Mageuzi ambao waliungana kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, kupinga hatua ya Ndugai kuwaburuza katika kupitisha hoja ya Mbatia.
Hoja hiyo binafsi iliyoainisha udhaifu katika mfumo wa elimu nchini, iliwasilishwa na kuibua mjadala mzito bungeni, huku kambi ya upinzani ikikubali hoja ya Mbatia kutaka kuunda kamati teule wakati wabunge wa CCM wakipinga, hoja iliyosababisha hadi sasa Wazairi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda tume inayotafuja tatizo la kufeli kwa wanafunzi wa mwaka 2012.
SOURCE TANZANIA DAIMA

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...