Tuesday, March 26, 2013

MCHORO WA KUMUUA ASKOFU MOKIWA


MCHORO uliosanifiwa na watu ambao inaaminika walitaka kumuua Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,  Dk. Valentino Mokiwa ni hatari.

 
Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,  Dk. Valentino Mokiwa.
Taarifa za kila upande, zinathibitisha kwamba mchoro huo ulisanifiwa kitaalam na kwamba kilichomwokoa Mokiwa ni Mungu.
Imebainika kuwa kingine kilichonusuru maisha ya Mokiwa ni muundo wa nyumba yake, kwani baada ya majambazi kumshambulia kwa mapanga mlinzi wake, iliwawia vigumu kuifikia nyumba ambayo kiongozi huyo wa kiroho alikuwemo.

MCHORO WENYEWE
Uchunguzi unaonesha kwamba uvamizi nyumbani kwa Mokiwa, Mbezi kwa Yusuf, Dar es Salaam, Machi 9, mwaka huu haukuwa wa bahati mbaya kwani uliandaliwa mapema.
Pikipiki ambayo namba zake hazikunakiliwa, inatajwa kuhusika na upangaji wa uvamizi huo kwani siku ya tukio ilikaribia nyumba ya Mokiwa takriban mara tatu.
 
“Eneo la nyumba ya askofu haina majirani wanaokaribiana useme labda alikuwa anakwenda kwenye nyumba nyingine.
“Ile pikipiki kwa mara ya kwanza ilionekana kati ya  saa 12:30 na saa 1:00 jioni. Iliondoka, nusu saa baadaye ikarejea tena, naamini yule mwendesha pikipiki na aliyepakiwa ndiyo waliokuwa wanasoma mazingira ya nyumba na uvamizi.


“Mara tatu walipokuja, nilishauriana na mwenzangu kisha nikatoka kwenda kuwauliza, wakajibu wanaangalia shamba ambalo mmiliki wake alipanga kuwauzia siku inayofuata, kwa hiyo pale walikuwa wanalikagua eneo lenyewe.
“Niliwauliza mbona ukaguzi wenyewe wanaufanya usiku? Majibu yao yakawa hayaeleweki kisha wakatoweka. Naamini wale ndiyo wachora mchoro wenyewe,” alisema mmoja wa walinzi kwa sharti la kutotajwa jina.

KIKAO SAA SABA USIKU
Habari zaidi zinaeleza kuwa mishale ya saa 7 usiku, mmoja wa walinzi wa Mokiwa aliwaona watu watatu wakiwa wamesimama gizani kama vile wanajadiliana kitu.
Imeelezwa kuwa mlinzi huyo hakuwa na wasiwasi mwingi kwa sababu hakudhani kama watu hao, walikuwa wanapanga njama za kuvamia kwenye nyumba ya Mokiwa.

MAJAMBAZI WAKATA SENG’ENGE
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, saa 8 usiku, majambazi hao waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya Mokiwa kwa kukwea ukutani.
 
“Nyumba inalindwa na mitambo maalum, kwa hiyo walikata seng’enge na kuharibu mfumo mzima wa ulinzi wa umeme kwenye nyumba hiyo.
 
“Bila kupoteza wakati, wakamwamuru mlinzi anayeitwa Fred awaoneshe mahali alipo Mokiwa, vinginevyo watamuua.
“Fred alibabaika sana, wale majambazi kwa sababu hawakutaka kupoteza wakati, wakaanza kumcharanga mapanga kichwani na miguuni kisha wakamchoma kitu chenye ncha kali mgongoni.
 
“Baada ya kuona Fred hajibu walishauriana, nadhani matarajio yao hayakuwa kama hali halisi waliyoikuta. Walidhani wakiingia tu ndani ya uzio watakutana na nyumba ya Mokiwa.
“Sasa ukiwa getini, unaiona nyumba kwa mbali, halafu kutoka pale getini hadi kwenye nyumba yenyewe ni pori, hilo likawatisha, wakakubaliana waondoke wakajipange vizuri,” kilisema chanzo chetu.
MAJIRANI WACHELEWA MCHEZO
Chanzo kilisema, utulivu wa usiku, ulisaidia kuwafanya majirani ambao wapo mbali kidogo kumsikia, hivyo wakajikusanya kwenda kutoa msaada.
“Majirani walifika usiku huo na kukuta mlinzi huyo akiwa anachuruzika damu  na baadaye akazimia, walimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Pwani, Tumbi.
“Kabla ya tukio, Askofu Mokiwa aliwatahadharisha walinzi wake kuwa makini, kwani alikuwa anapata ujumbe wa vitisho, hivyo kumfanya atoe taarifa polisi,” kilisema chanzo chetu.
MOKIWA AZUNGUMZA
Kwa upande wake Askofu Mokiwa alisema, anashangazwa na kitendo hicho cha kuvamiwa nyumbani kwake na mlinzi wake kujeruhiwa vibaya.
Alisema, hajawahi kusikia au kuona katika maeneo hayo uvamizi ukitokea,  hivyo  tukio lililotokea nyumbani kwake  ni kama mchoro wa kikundi cha watu fulani waliotaka kumuua.
“Walipofika pale hawakutaka kitu chochote, walisema wananitaka mimi, nashukuru Mungu hawakuweza kunifikia,” alisema Mokiwa.
                             CHANZO CHA HABRI NA GLOBALPUBLISHERS

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...