Mtuhumiwa wa makosa ya uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Jenerali Bosco Ntaganda, amejisalimisha katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali nchini Rwanda.
 Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa Ntaganda aliomba apelekwe katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, iliyoko mjini The Hague, nchini Uholanzi.
Mahakama hiyo ya ICC ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Jenerali Ntaganda mwaka 2006.
Lakini mwenyewe amekanusha tuhuma za kuwatumikisha watoto jeshini, kufanya mauaji ya kikabila na ubakaji.
Mashtaka dhidi yake yanahusiana na wakati alipokuwa kiongozi wa wanamgambo kaskazini-mashariki mwa Kongo, kati ya mwaka 2002 na 2003.
Ntaganda pia anaaminika kuwa kiongozi wa kundi la waasi la M23, ambalo linapambana na vikosi vya serikali mashariki mwa nchi hiyo.