Thursday, July 13, 2017

WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na kukabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa.

Amesema kati ya magari hayo, moja ni kwa hospitali hiyo ya wilaya na la pili litapelekwa katika Kituo cha Afya cha Mandawa.

Alikabidhi magari hayo jana alipotembelea hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema magari hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.

“Rais wetu Dk. John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono,” alisema.

Waziri Mkuu alisema magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa  wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.

Kabla ya kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama na ya  watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na akasema kwamba ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya, alisema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.

LOWASSA ATAKIWA KURUDI KWA DCI ALHAMISI IJAYO

Nusu saa baada ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kuwasili katika ofisi ya mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, kama alivyotakiwa kufanya Juni 29, ameruhusiwa na kutakiwa kurudi tena Alhamisi ijayo.

Mwanasheria wa Lowassa, Peter Kibatala amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Lowassa ametakiwa kurudi Alhamisi bila sababu za kuahirishwa kwa mahojiano hayo kuwekwa wazi.

“Hatujaambiwa kwa nini ila tumeambiwa tuje alhamisi ijayo kwa ajili ya maelekezo na kuwasikiliza zaidi,” alisema

SERIKALI YATANGAZA AJIRA 10, 000 KUZIBA PENGO LA WALIOGHUSHI VYETI

Ofisi ya  Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa vibali vya ajira 10,184 kwa mamlaka za serikali za mitaa, sekretarieti za mikoa, wakala za serikali na taasisi na mashirika ya umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amesema hayo leo katika kikao na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Mgawo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki

Ameongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgao wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuziwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi za wazi zilizojitokeza.

Wednesday, July 12, 2017

DIWANI MWINGINE WA CHADEMA ARUSHA, AJIUZULU LEO







Hali si shwari tena ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, baada ya diwani mwingine wa chama hicho, Japhet Jackson kuandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM.

Diwani huyo ni wa saba kujiuzulu ndani ya mwezi mmoja, katika Jimbo la Arumeru Mashariki na Jimbo la Arusha mjini, majimbo ambayo wabunge wake ni Joshua Nassari na Godbless Lema.

Jackson amewasilisha barua leo mchana ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri na kueleza anamuunga mkono Rais John Magufuli.

KLABU YA EVERTON YAWASILI NCHINI, WAYNE ROONEY YUMO.

Klabu ya Everton tayari imewasili Jijini Dar es Salam asubuhi ya leo ikitokea nchini Uingereza nakupokelewa na Waziri wa Habari Dr. Harrison Mwakyembe, huku ikiwakosa wachezaji wake watatu muhimu katika kikosi hicho kutokana na majeruhi waliyokuwa nayo.

Pamoja na hayo, timu ya Everton imeongozwa na mchezaji nyota Wayne Rooney pamoja na Davy Klaassen na Michael Keane ambao pia wamejiunga na klabu hivi karibuni.

 Like page yetu ya facebook/jambotz pia tu-follow Instagram @jambotz.

Tuesday, July 11, 2017

DIWANI WA CHADEMA ARUSHA AJIUZULU NA KUMUUNGA MKONO MAGUFULI

Diwani wa Ngabobo (Chadema), Solomon Laizer ameandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM kwa maelezo anamuunga mkono Rais John Magufuli.

Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu kwa kutoa sababu kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri amethibitisha leo (Julai 11) kupata taarifa za kujiuzulu kwa Ngabobo.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema kujiuzulu kwa diwani huyo ni mchezo mchafu akidai  amenunuliwa.

Wednesday, July 05, 2017

MSHINDI WA KUCHORA NEMBO YA EAC KUNYAKUA KITITA CHA DOLA 25,000

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, imewataka vijana wenye uwezo wa kubuni na kuchora kujitokeza kushiriki shindano la kubuni nembo mpya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Msemaji wa wizara hiyo,  Mindi Kasiga amesema shindano hilo ni fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao, pia kujipatia kipato iwapo watashinda. 

Shindano hilo limeanza Juni Mosi na mwisho ni Agosti 31.

Tuesday, July 04, 2017

MAGUFULI AZITAKA NGO'S ZINAZOTETEA WANAFUNZI WENYE MIMBA WAFUNGUE SHULE ZAO

Rais John Magufuli amezitaka Asasi za Kiraia (NGO’s) kufungua shule kwa wanafunzi wanaopata mimba shuleni kama kweli zinawapenda wanafunzi hao.

Rais ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 4) alipokuwa akihutubia wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Sengerema.

“Si kwamba nawachukia wenye mimba, hata kwa bahati mbaya akapata mimba, kama hizo NGO zinawatetea sana, zifungue shule za wenye mimba, kwa sababu zinawapenda wenye mimba, wafungue shule zao,”amesema Rais leo.

Amesema hata hao wanaofanya makongamano ya kuhamasisha watu wapate mimba wafungue shule zao kwa ajili ya wanafunzi hao.

“ Haiwezekani fedha za walipa kodi, Sh 17 bilioni kila mwaka za kusomesha watoto wetu, kwenda kusomesha wakinamama, wazunguke, waimbe, waseme nini mimi ndiyo Rais, huo ndio ukweli,” amesema.

Amesema tatizo si wanaopata mimba, kwani wapo waliopata matatizo, kama kuugua kwa muda mrefu wakashindwa kwenda shule lakini ulianzishwa mpango maalum wa kuwasomesha katika mfumo usio rasmi.

KINGA YA UKIMWI YAANZA KUONESHA MAFANIKIO

Utafiti wa kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya  Ukimwi, ulioanza kufanywa nchini miaka kadhaa iliyopita umeana kuonyesha mafanikio.

Lakini watafiti wamesema Watanzania watahitaji kuwa uvumilivu wa miaka michache ijayo kusubiri hatua za mwisho za ukamilishaji utafiti wa kinga hiyo kabla haijaanza kutimika rasmi.

Taarifa hizo zinakuja ikiwa wiki moja baada ya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutumia dawa ya ugonjwa wa Ukimwi ambayo inaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu ambao wanasumbuliwa na magonjwa nyemelezi na ambayo hayakubali tiba nyingine.

Kwa miaka kadhaa  Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS) imekuwa ikiendesha utafiti kuhusiana na chanjo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na katika hatua ya awali utafiti huo uliwahusisha baadhi ya watu wanaishi na virusi hivyo.

TIMU YA SINGIDA UNITED YAONESHA JEURI YA PESA, YANUNUA BASI LA MILLION 350/-

Baada ya kupata udhamini mnono kutoka katika kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa hatimaye klabu ya Singida United inazidi kutanua misuli yake katika ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kutambulisha usafiri wao utakao tumika katika kusafirishia wachezaji.
 Akizungumza na waandishi wa habari jana katibu Mwenezi wa klabu hiyo Festo Sanga amethibitisha Singida United kununua Basi jipya lenye gharama ya shilling milioni 350.

Sunday, July 02, 2017

MTANGAZAJI WA AZAM TV ALIEPOTEA APATIKANA

Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Azam, Fatna Ramole amepatikana ikiwa ni saa 48 baada ya kudaiwa kutoweka.

Ndugu yake, Lulu Ramole amezungumza na mwandishi wa habari hii jana (Julai mosi) na kueleza kuwa kwa sasa yeye na Fatna wapo kituo cha Polisi, Kinondoni.

Lulu aliandika katika ukurasa wake wa twitter leo saa nane mchana akiwashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompa hadi dada yake kupatikana.

“Msamaria alitupigia simu amepatikana Makongo, nipo naye lakini siwezi kueleza kwa undani alivyopatikana, uchunguzi unaendelea,” amejibu kwa kifupi Lulu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda amethibitisha kupatikana kwa Fatna, lakini kwa maelezo na ufafanuzi zaidi alishauri familia ya mwanahabari huyo iulizwe.

“Lakini tutawaita hapa kwa mahojiano zaidi,” amesema

WABUNGE UJERUMANI WAIDHINISHA NDOA YA JINSIA MOJA

Wabunge nchini Ujerumani wameidhinishwa, kwa wingi wa kura, sheria ya kuhalalisha ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Wamefanya hivyos iku chache baada ya Kansela Angela Merkel kuondoa upinzani wake dhidi ya mpango huo.

Chini ya mabadiliko hayo sasa, wapenzi wanaotaka kuoana ambao awali walikubaliwa tu kuwa na ushirika, hadhi ya ndoa kamili na wana haki ya kuasili watoto.

TRUMP: TUMECHOKA KUIVUMILIA KOREA KASKAZINI

Rais wa Marekani, Donald Trump amesisitiza kwamba muda wa kimkakati wa uvumilivu kwa Korea Kaskazini umekwisha.

Katika hotuba ya pamoja juzi, akiwa na mwenzake wa Korea Kusini, Moon Jae katika bustani ya Rose kwenye Ikulu ya White house, Trump aliahidi ‘kuchukua hatua madhubuti’ dhidi ya programu ya nyuklia na makombora ya Korea Kusini akisema vitisho vyake vinafaa kupatiwa majibu ya kijasiri.

“Hizi si zama za kuvuta subira juu ya Serikali ya Korea Kusini ambayo imeshindwa kutekeleza wajibu wake,” alisema Trump.

Tuesday, June 27, 2017

'MARUFUKU CHAKULA KUSAFIRISHWA NJE YA NCHI' MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula nje ya nchi bila kibali na kuwataka wafanyabiashara kuuza chakula kwenye maeneo yenye uhaba nchini.

Majaliwa ametoa agizo hilo jana, Jumatatu wakati akihutubia Baraza la Eid katika Msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu huyo amesema kuwa kuna maeneo ambayo wananchi hawakupata chakula vizuri kutokana na uhaba wa mvua hivyo wafanyabiashara wapeleke chakula kwenye maeneo hayo.

“Serikali bado haijatoa kibali cha kutoa chakula nje ya nchi, kama unaona kuna umuhimu kaombe kibali, lakini utapewa kibali cha kusaga upeleke unga na siyo mahindi,”amesisitiza  Majaliwa.

Majaliwa ameonya kuwa kwa wale watakao kamatwa wakisafirisha mahindi nje ya nchi kinyume na utaratibu, mahindi hayo yatataifishwa na kupelekwa kwenye ghala la Taifa na magari yatapelekwa polisi.

Amesema kuwa Serikali imepokea barua za maombi ya kupeleka chakula nchi jirani, lakini bado haijatoa ruhusa.

Monday, June 26, 2017

JAMBO TZ INAWATAKIA EID MUBARAK WAISLAMU WOTE DUNIANI

Uongozi na wafanyakazi wote wa Jambo Tz Blog wanawatakia watanzania wote kwa ujumla Eid Mubarak na mapumziko mema katika sikukuu ya Eid El Fitr.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...