SPIKA
wa Bunge, Anne Makinda amekiri kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike katika Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM) na hivyo kukataa mwongozo wa mbunge akisema hali iko
hivyo.

Makinda
alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati Bunge likiwachagua
wawakilishi wake katika mabaraza ya vyuo na SADC-PF, ambapo Naibu
Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliuliza swali hilo la
uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono.
Mwalimu
alimuuliza mmoja wa wagombea, Murtaza Mangungu (CCM) kuwa UDOM
imekithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi wa
kike kuombwa rushwa ya ngono na baadhi ya wahadhiri wasio waadilifu.
Naibu waziri huyo alitaka kujua, Mangungu ataondoshaje kero hiyo kwa
wanafunzi wa kike chuoni hapo, endapo atachaguliwa kuwa mjumbe wa
baraza.
Katika
majibu yake, Mangungu alisema kuwa atashirikiana na wenzake
kuhakikisha wanaondosha kero hiyo kwa wanafunzi wanaofanyiwa vitendo
hivyo.































