Saturday, June 08, 2013

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amekiri kuwepo kwa vitendo ngono UDOM.

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amekiri kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na hivyo kukataa mwongozo wa mbunge akisema hali iko hivyo.


Makinda alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati Bunge likiwachagua wawakilishi wake katika mabaraza ya vyuo na SADC-PF, ambapo Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliuliza swali hilo la uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono.


Mwalimu alimuuliza mmoja wa wagombea, Murtaza Mangungu (CCM) kuwa UDOM imekithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi wa kike kuombwa rushwa ya ngono na baadhi ya wahadhiri wasio waadilifu.

Naibu waziri huyo alitaka kujua, Mangungu ataondoshaje kero hiyo kwa wanafunzi wa kike chuoni hapo, endapo atachaguliwa kuwa mjumbe wa baraza.

Katika majibu yake, Mangungu alisema kuwa atashirikiana na wenzake kuhakikisha wanaondosha kero hiyo kwa wanafunzi wanaofanyiwa vitendo hivyo.

Baada ya majibu hayo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo (CUF), aliomba mwongozo wa spika, akitaka swali na jibu hilo vifutwe akidai italeta picha mbaya kwa UDOM.


“Mheshimia Spika, aliyeuliza swali ni kiongozi wa serikali, naibu waziri, sasa jibu hili likibakia hivyo italeta sifa mbaya kwa UDOM kuwa kuna vitendo vya rushwa ya ngono, naomba swali na jibu vifutwe,” alisema.


Hata hivyo, katika kujibu mwongozo huo, Spika Makinda alisema kwa kifupi: “Hakifutwi kitu hapa, hali ndivyo ilivyo.”

Kwa miaka ya karibuni, UDOM imekuwa ikitajwa kwa sifa mbaya ya baadhi ya wahadhiri wake kuwaomba wanafunzi wa kike rushwa ya ngono ili wawape upendeleo katika ufaulu wao.


Inaelezwa kuwa wako baadhi ya wanafunzi wa kike waliofelishwa mitihani na kutakiwa kurudia masomo au mwaka baada ya kugoma kutimiza matakwa hayo ya rushwa ya ngono.

Pia wanafunzi kadhaa wa kike wa chuo hicho, wamekuwa wakihusishwa na matukio ya biashara ya ukahaba katika maeneo mbalimbali ya starehe mjini hapa, hasa wakati wa vikao vya Bunge.


Katika hatua nyingine, Spika Makinda alitangaza washindi wa uchaguzi huo wa wawakilishi wa Bunge kwenye mabaraza ya vyuo na SADC-PF.

Alisema kuwa Mangungu anakuwa mjumbe wa baraza UDOM baada ya kumshinda Pudenciana Kikwembe wa Viti Maalum (CCM), huku Jitu Vrajlal Soni akipita bila kupingwa kuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Morogoro (SUA) baada ya mshindani wake, Dk. Peter Kafumu kujitoa.


Wengine ni Pindi Chana wa Viti Maalum (CCM) ambaye alipita bila kupingwa kuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Spika aliongeza kuwa Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) atakuwa mjumbe katika Jukwaa la Kibunge la nchi Wanachama Kusini mwa Afrika (SADC-PF).

Katika mchuano huo, Jafo aliwashinda Leticia Nyerere wa viti maalum (CHADEMA) na Lolesia Bukwimba wa Busanda (CCM).
Via Tanzania Daima

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...