Nelson Mandela ‘Madiba’.
Habari hizo ambazo awali zilifanywa siri kabla ya kuvuja wikiendi iliyopita, zinasema kuwa Ikulu ya Afrika Kusini ilikosa umakini, hivyo ikaacha gari bovu limbembe Mzee Mandela na matokeo yake lilizimika kwenye barabara kuu (high way).Kuzimika kwa gari hilo, kulisababisha hekaheka lakini ufumbuzi wa haraka ulikosekana mpaka dakika 40 baadaye ndipo ‘ambulance’ nyingine ilipofika eneo la tukio, ikambeba Mzee Mandela na kumuwahisha hospitali.
Ikulu ya Afrika Kusini imelazimika kutoa tamko, baada ya wachambuzi kuelezea tukio hilo kwamba zilikuwa dakika 40 za hatari za Mzee Mandela, kwa maana nusura zichukue uhai wa kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, miaka ya 1900 nchini humo.
Tukio lenyewe, lilijiri Juni 8, mwaka huu (zaidi ya wiki mbili zilizopita) lakini ikawa kimya katika vyombo vya habari, japo minong’ono iliendelea kushamiri, kabla ya mambo kuwekwa hadharani wikiendi iliyopita.
KIVIPI DAKIKA 40 ZA HATARI?
Kwa mujibu wa habari pamoja na makala za wachambuzi mbalimbali wa kisiasa nchini Afrika Kusini, muda mfupi baada ya Mzee Mandela kuondolewa barabarani pale gari lilipomzimikia na kuwahishwa katika Hospitali ya Mediclinic Heart, Pretoria, uvumi ulienea kuwa ameshafariki dunia.