Msichana mdogo ameomba hifadhi ya ukimbizi nchini Uingereza baada ya kukataa kwa dharau harakati za ndoa za wake wengi za Mfalme Mswati III wa Swaziland na kugoma kujiunga kwenye nyumba harimu ya wake 13.
Tintswalo Ngobeni, mwenye umri wa miaka 22, alitimkia Uingereza kutoka taifa hilo la kusini mwa Afrika akiwa na umri wa chini ya miaka 18 baada ya kuvuta hisia za mfalme huyo milionea, mtawala maarufu mkandamizaji kwa maisha yake ya anasa.
Ikiwa ni sehemu ya mila za Swazi, Mfalme Mswati III, mwenye umri wa miaka 45, anaruhusiwa kuchagua mke mpya kila mwaka.
Tintswalo, ambaye sasa anaishi mjini Birmingham, alikuwa na umri wa miaka 15 tu wakati Mfalme huyo alipofanya harakati zake baada kumuona kwenye jumba la kifalme la mke wake wa nne, LaNgangaza. Binti huyo alisema 'alitishika' pale alipogundua dhamira zake za ndoa.
Aliongeza: "Alianza kunipigia simu kwenye shule ya bweni. Aliniuliza kama ningetaka kuwa sehemu ya familia ya kifalme. Ilinibidi kukaa kimya kuhusu mashaka yangu lakini nilifahamu sikutaka kuolewa naye na kujitolea maisha yangu kwa mfalme huyo.
"Wake zake wamewekwa kwenye majumba yao, wakizingirwa na walinzi, na hakika hawawezi kwenda kokote isipokuwa tu mfalme akisema hivyo. Kitu pekee wanachofanya ni kwenda Marekani mara moja kwa mwaka, wakati mfalme huyo anapowapatia posho kwa ajili ya manunuzi."
Tintswalo alikuwa amelazimishwa kuachana na maisha ya starehe kwenye shule moja ya bweni huku shangazi yake, ambaye alikuwa mlezi wake mkuu, akisuka mipango ya kutorokea Uingereza kuungana na mama yake, ambaye alihamia mjini Birmingham miaka mitano kabla, akimtoroka mume wake mnyanyasaji.
"Sikuwa na jinsi," alisema. "Hakuna aliyewahi kumwangusha mfalme huyo au kuthubutu kumdharau, hivyo nikatoweka tu."