Wakati tume ya kuchunguza
matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 ikiendelea na kazi,
imebainika kuwa wanafunzi waliokata rufaa kutaka mitihani yao
isahihishwe upya wamefeli zaidi baada ya
kusahihishiwa.Kwa mujibu wa
taarifa kutoka ndani ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zimethibitishwa na baadhi ya maofisa,
wanafunzi waliokata rufaa wamefeli zaidi na hata walioongezewa alama
matokeo hayakubadilisha madaraja waliyopata awali.Habari zinaeleza kuwa,
wanafunzi waliokata rufaa NECTA kutaka mitihani yao isahihishwe upya ni
takribani 10,000 na kwamba baraza bado limetoa muda zaidi kwa wengine
wanaotaka kukata rufaa.
Vyanzo vya habari kutoka ndani
ya NECTA viliieleza NIPASHE kuwa mitihani kwa wanafunzi waliokata rufaa
ilianza kusahihishwa Machi 12 na kuhitimishwa Machi 15, mwaka huu na
kwamba wengi wamefeli zaidi.“Baada ya wanafunzi kadhaa kukata rufaa,
NECTA iliamua kuwaita walimu waandamizi katika masomo yote na kuanza
kufanya kazi ya kusahihisha mitihani hiyo upya kwa umakini,
kilichowashangaza walimu hao ni kuona kiwango cha kufeli kimeongezeka,”
alisema ofisa mmoja wa NECTA ambaye aliomba jina lake lisiandikwe
gazetini kwa maelezo kuwa siyo msemaji wa baraza hilo.