Basi dogo aina ya Hiace likiwa limetumbukia kwenye Mto Kiwira eneo maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege, wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Msiba mwingine mzito umelikumba
taifa baada ya watu 38 kupoteza maisha katika matukio mawili tofauti,
likiwamo la ajali ya basi dogo aina ya Toyota Hiace iliyoua watu 19
wakati ikifanya safari ya wizi mkoani Mbeya.
Tukio jingine limetokea mkoani Shinyanga ambako
wachimbaji wadogo 19 wa dhahabu waliokuwa katika mgodi mdogo wa Kalole,
wilayani Kahama wamekufa baada ya kufunikwa na kifusi usiku wa kuamkia
jana kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Polisi wakiwa katika machimbo ya dhahabu ya Kalole wilayani Kahama jana baada ya machimbo hayo kuporomoka na kuua watu 19.
Polisi wakiwa katika machimbo ya dhahabu ya Kalole wilayani Kahama jana baada ya machimbo hayo kuporomoka na kuua watu 19.
Matukio hayo ni mwendelezo wa majanga ya ajali
ambazo zimekuwa zikitokea kwa takriban wiki mbili mfululizo na kuua
mamia ya watu. Zaidi ya watu 980 wamefariki dunia katika ajali za
barabara katika muda wa zaidi ya miezi mitatu. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Katika ajali ya basi iliyotokea saa 3:00 asubuhi
jana katika Barabara ya Mbeya-Kyela eneo la Kiwira ambalo ni maarufu kwa
jina la Uwanja wa Ndege kutokana na magari mengi yanayopata ajali
kuonekana kama ndege inayoelekea kutua wakati yakitumbukia kwenye bonde
ambalo Mto Kiwira unapita, watu 18 walifariki papo hapo na mwingine
mmoja alifariki dunia akiwa Hospitali ya Igogwe.
Dereva wa basi hilo, lililokuwa likipeleka
wafanyabiashara kwenye gulio la Kiwira wilayani Rungwe, alikuwa ameamua
kufanya safari hiyo badala ya ruti zake za kawaida za kuzunguka mjini
Mbeya, baada ya madereva wa mabasi aina ya Toyota Coaster kuwa na mgomo
wa kupinga wenzao kupigwa faini kubwa.
Akizungumzia ajali hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya
Rungwe, Zainab Mbiro alisema chanzo chake ni mwendo wa kasi katika eneo
lenye mteremko ambao una kona kali iliyo takriban kilomita nne kabla ya
kuingia Kiwira.
Eneo hilo linajulikana kwa ajali nyingi ambazo zimekuwa zinachukua maisha ya watu wengi kila mwaka.
“Basi dogo limetumbukia kwenye Mto Kiwira baada ya
dereva kushindwa kukata kona kutokana na kuwa kwenye mwendo kasi katika
eneo la mtelemko mkali maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege,’’ alisema.
Eneo hilo la urefu wa kilometa nane za barabara ya
kuanzia Uyole kwenda Rungwe, limewekewa vibao vya alama za tahadhari
kwa madereva kuwatahadharisha kuwapo kwa miteremko na kona kali.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya, Hemed Msangi,
akiwa eneo la tukio jana, alisema ajali hiyo iliua watu 18 palepale na
mmoja alifariki dunia akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Igogwe,
Kiwira na kwamba watatu walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini hapo.
Msangi alisema maiti 18 zilipelekwa Hospitali ya
Makandana wilayani Rungwe na mmoja alibaki Igogwe. Hata hivyo alishindwa
kutaja majina akisema karibu wote hawana vitambulisho.
“Kibaya zaidi ni kwamba gari lililopata ajali ni
daladala linalosafiri kati ya Igawilo na Majengo na wafanyakazi wake
waliamua kuwachukua wafanyabiashara waliokuwa wakienda kwenye gulio la
Kiwira wilayani Rungwe baada ya (Toyota) Coaster kugoma,” alisema.
Mabasi hayo aina ya Toyota Coaster ndiyo yanayofanya safari kati ya mji wa Uyole na Tukuyu. Ajali hiyo inafanya idadi ya waliokufa kati ya
Januari Mosi na Aprili 12 mwaka huu kufikia 988, kwa mujibu wa taarifa
aliyoitoa Kamanda Mpinga hivi karibuni.
Kamanda Mpinga alisema watu 866 walikufa na
wengine 2,363 kujeruhiwa kati ya Januari na Machi, wakati wengine 103
wamepoteza maisha na 138 kujeruhiwa kati ya Machi 11 na Aprili 12 mwaka
huu.
Kuhusu mgomo wa mabasi aina ya Toyota Coaster,
Kamanda Msangi alisema chanzo ni madereva kupinga faini ya Sh250,000
iliyotolewa na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na
Nchikavu (Sumatra) kwa madereva wawili baada ya kukiuka taratibu za
usafirishaji.
Tukio la kugoma kwa madereva hao ni la pili kwa
wiki hii, la kwanza likiwa limetokea Jumatatu ambalo lilisuluhishwa
baada ya viongozi wa Sumatra kukutana na wadau hao pamoja na polisi na
kuafikiana kwamba mabasi yaliyokamatwa yaachiwe.
Mwenyekiti wa madereva hao, Damdam Mwandubya
hakuweza kupatikana, lakini dereva aliyejitambulisha kwa jina la Geofrey
Masanja alisema waligoma ili kushinikiza mabasi yaliyopigwa faini,
yaachiwe.
Maafa Shinyanga
Mkoani Shinyanga wachimbaji wadogo 19 walifukiwa
na kifusi wakiwa ndani ya mgodi mdogo wa Kalole kutokana na mvua kubwa
zinazoendelea kunyesha.
Wachimbaji hao walikuwa wameingia kwenye mashimo
nane ambayo baadaye yalibomoka kutokana na kufunikwa na udongo, jambo
lililosababisha vifo vyao.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema
vijana hao waliingia katika mashimo hayo saa 12:00 jioni kwa lengo la
kuiba mawe baada ya muda wa kufanya kazi kumalizika.
“Unajua hawa ndugu zetu ni wale wachimbaji
wasiokuwa na mashimo ambao muda ukiisha wa kazi huingia kwenye mashimo
hayo bila kuangalia usalama na ndivyo ilivyotokea kwa wachimbaji hao,”
alisema Mpesya.
Mpesya alisema kazi ya kufukua maiti hizo
lilianza, lakini lilikwama kutokana na hali ya unyevunyevu kwenye
mashimo hayo ambayo bado yanaendelea kutitia.
“Kati ya maiti 19, saba tayari zimeshatambuliwa na ndugu zao
huku nyingine mbili zikiwa bado hazijatambuliwa na tayari tumeomba
mashine ya kufukua na ya kunyonya maji kutoka mgodi wa Bulyanhulu ili
itusaidie,” alisema
Hata hivyo, Mpesya alisema idadi hiyo inaweza
kuongezeka baada ya kazi ya kufukua kukamilika kwa kuwa hawawezi kujua
kama maiti hizo 19 ndio idadi pekee ya watu waliokuwemo ndani ya mashimo
hayo.
“Tunasubiri wenzetu kutoka mgodi wa Bulyanhulu
waje waone kwanza mitambo ipi ambayo inaweza kutumika kuyafukua mashimo
hayo kwa kuwa ufukuaji wa kienyeji tuliokuwa tukitumia tumeusimamisha
kutokana na mashimo hayo kuendelea kutitia,” alisema Mpesya.
Machimbo hayo yaliyoko katika kijiji cha Kalole
katika kata ya Lunguya Halmashauri ya Msalala, ni moja kati ya migodi ya
wachimbaji wadogo wanaokisiwa kufikia 30,000 na tayari wengi wao
wamejipatia mamilioni ya pesa kwa uchimbaji huo wa kienyeji hali ambao
si salama. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment