Saturday, April 18, 2015

ETOILE WAPIGWE TU...!!!

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao katika moja ya mechi katika uwanja wa Taifa.
Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli katika moja ya mechi walizocheza Uwanja wa Taifa.
 
WAPIGWE tu hao Etoile Sportive du Sahel. Ndio kauli ambayo wapenzi wa Yanga na wa mpira wa miguu Tanzania wanaitoa kuelekea pambano la leo la Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga, moja ya timu kongwe nchini, inashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuikabili Etoile Sportive du Sahel (ESS) ya Tunisia katika mechi ya raundi ya pili ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Vijana hao wa Jangwani ndio timu pekee iliyobaki ya Tanzania katika michuano ya kimataifa na ndio maana wapenzi wake, mashabiki wa soka nchini na Watanzania kwa ujumla, wangependa kuiona inaipiga ESS na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika marudiano Mei Mosi, mwaka huu, mjini Sousse. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm ameufananisha mchezo huu na vita ambayo wanalazimika kuishinda ili kujiweka katika mazingira ya kucheza hatua ya makundi. Pluijm alisema anawaheshimu wapinzani wao kuwa ni timu nzuri yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa kwenye mashindano hayo, lakini wamejiandaa kushinda mchezo huo.

“Najua Sahel ni timu kubwa, lakini mchezo huu ni sawa na vita kwetu, lazima tupambane ili tupate ushindi utakaotuweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.

Kocha huyo aliyewahi kupata mafanikio makubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Berekum Chelsea FC ya Ghana, alisema watatumia mfumo ule ule alioutumia katika mechi za hatua mbili za kwanza katika michuano hiyo ya kimataifa, wa mashambulizi na kasi kupata mabao mengi.

“Tutatumia mfumo wetu ule ule ambao umetufikisha hapa kwa kucheza kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi tukiwa na lengo la kupata idadi kubwa ya mabao,” aliongeza Pluijm anayesaidiwa na Charles Boniface Mkwasa. Kufika hatua hiyo, Yanga ilizitoa Botswana Defences Forces (BDF) ya Botswana na FC Platinum ya Zimbabwe.

Pluijm alisema wachezaji wake wote wapo katika hali nzuri na amekuwa akiwajenga kisaikolojia ili wacheze kwakujiamini na kupata matokeo mazuri leo.
Yanga itawategemea wachezaji wake ambao kwa msimu huu wamekuwa wakiibeba na kuiwezesha kuongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara hadi sasa ikiwa na pointi 46 baada ya mechi 21.

Hao wanaongozwa na nahodha wao, Nadir Haroub wenyewe wanamwita Cannavaro wakimfananisha na nahodha wa Italia aliyenyakua ubingwa wa dunia 2006, beki kisiki Fabio Cannavaro.

Wengine ni kipa Ally Mustapha, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Said Juma ‘Makapu,’ Simon Msuva, Mrisho Ngassa, Kpah Sherman, Amisi Tambwe, Haruna Niyonzima, Andrey Coutinho ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeraha.
Itamkosa Salum Telela ambaye aliumia dhidi ya Mbeya City wiki iliyopita na ameshindwa kupona kwa wakati. Wapinzani wa Yanga walitua jana alfajiri kwa ndege maalumu ya kukodi namba Bj4870 Nouvelair wakiwa na msafara wa watu 56.

Jana jioni walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa. Msafara huo unahusisha wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10.

ESS imepata nafasi ya kukutana na Yanga baada ya kuitoa Benifica de Luanda ya Angola kwa jumla ya ambao 2-1. Ilitoka sare ya bao 1-1 mjini Luanda, wakati katika mechi ya kwanza, Watunisia walishinda 1-0. Aidha, Yanga ilipata nafasi ya kukutana na timu hiyo baada ya kuwatoa FC Platinum Zimbabwe.

Licha ya kufungwa bao 1-0 katika mechi ya marudiano iliyochezwa Bulawayo nchini Zimbabwe, Yanga walisonga mbele kutokana na ushindi wa mabao 5-1 ambao iliupata katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam.

Rekodi zinaonesha kuwa Etoile katika kipindi cha miaka 10 tangu 2005 katika ushiriki wake wa michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, imewahi kushindwa kuvuka raundi ya kwanza kwenda ya pili mara moja tu.

Mara zote timu hiyo imekuwa ikiishia raundi ya pili au hatua ya makundi na mara nne imefanikiwa kucheza fainali, mbili za Ligi ya Mabingwa ikitwaa kombe moja na kupoteza mara moja sawa na ilivyo kwa Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa rekodi tangu 2005, Etoile ilifika fainali za Ligi ya Mabingwa na kufungwa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-0. Wakitoka sare isiyo na mabao nyumbani kabla ya kulala 3-0 ugenini.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka Msumbiji huku Kamisaa akiwa Salah Ahmed Mohamed kutoka Sudan. Kiingilio cha mchezo huo ni Sh 5,000, Sh 10,000, Sh 20,000, Sh 30,000 na Sh 40,000. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...