Baadhi ya watoto 18 katika tukio la kwanza walikuwa wakihifadhiwa kwenye
nyumba iliyopo Kata ya Pasua kwa lengo la kuwafundisha dini ya
Kiislamu, mkoani Kilimanjaro.
Mambo mazito zaidi yamezidi kubainika
mkoani Kilimanjaro baada ya polisi kugundua nyumba nyingine yenye watoto
kumi na mmoja waliokusanywa kutoka mikoa mbalimbali kwa ajili ya
kufundishwa dini.
Hii ni mara ya pili katika muda usiozidi wiki moja
baada ya polisi kubaini nyumba iliyohifadhi watoto 18 kwa lengo kama
hilo Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela
alisema tukio hilo linafanya wapelelezi kuumiza vichwa kwa kuwa mikoa
waliyotoka ndio ile ile waliyotoka watoto 18 waliokutwa kwenye nyumba
moja mjini Moshi.
Nyumba
hiyo imebainika wakati kukiwa na madai
kwamba baadhi ya misikiti katika maeneo ya Pasua, Njoro na Kibosho
yanaendesha mafunzo ya judo na karate. Tangaza biashara yako hapa kwa
bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa
Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Kamanda Kamwela alieleza kuwa kama ilivyokuwa
awali, watoto waliobainika juzi wanatoka katika mikoa ya Tanga, Dodoma,
Singida, Tabora na Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, watoto hao waligunduka
katika nyumba iliyoko eneo la Lyamungo wilayani Hai. Alisema umri wao
ni kati ya miaka 14 na 17 na walikuwa wanafundishwa dini na ushonaji.
Alisema kituo hicho ambacho hakijasajiliwa,
kinaitwa Umm Sukhail na kinamilikiwa na mwalimu mstaafu, Abubakar Juma
(64) mkazi wa Tanga ambaye kwa sasa anaishi maeneo ya Kibosho Mweka.
Kamwela alisema watoto hao wamechukuliwa na polisi
kwa uchunguzi zaidi ili kujua sababu za wao kuishi katika eneo hilo pia
kubaini ukweli wa mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.
“Kutokana na kugundulika kwa mafunzo haya yasiyo
rasmi yanayotolewa na walimu ambao pia si rasmi, lazima tuchunguze kama
baada ya kuhitimu wanapewa vyeti na wanafanya kazi wapi,” alisema.
Kamwela pia alisema polisi wanafanya uchunguzi ili
kubaini kama watoto hao walipata elimu ya msingi kama sheria
inavyoelekeza na kama walifaulu ama la na kwanini hawakuendelea na
masomo. Kamanda alisema upo uwezekano wa watoto 18 waliokutwa Pasua
kuhamishiwa kituo cha Narumu na kwamba jeshi hilo linaendelea na
uchunguzi kubaini kama wenye vituo hivyo wanafanya kazi pamoja.
Kuhusu watoto 18 wa Pasua, Kamanda Kamwela alisema
wametambuliwa na wazazi wao na kuchukuliwa, lakini bado uchunguzi
unaendelea kujua uhusiano wao na mmiliki wa nyumba hiyo.
“Tunachunguza kujua kama wazazi walikuwa
wakifahamu maisha wanayoishi na sababu za kuwatoa kwenye shule za
Serikali na kuwapeleka kwenye shule za dini wakati elimu ya msingi ni ya
lazima,” alisema.
Pamoja na wazazi wo kudai waliridhia watoto wao kwenda kupatiwa
masomo hayo, kamanda alisema uchunguzi umebaini watoto hao walikuwa
wanaishi kwenye mazingira magumu kutokana na ufinyu wa eneo na hivyo
hulazimika kulala chini.
“Upelelezi kuhusu tukio hili bado unaendelea kwa
sababu kuna maswali mengi yanayohitaji majibu kwa kuwa watoto hawa bado
ni wadogo na walitakiwa wawe wanasoma shule ya msingi,” alisema.
“Lakini wakawa wanaishi kwenye nyumba hii lazima
tujue uhalali wa wao kuacha shule na kwenda kujifunza dini kwenye nyumba
ambayo haijasajiliwa na nyumba ambayo huduma za kijamii sio rafiki.”
Kamanda alisema: “Elimu inayotolewa kwa siri
ambayo hata Serikali haijui na majirani hawajui inatia shaka na ndio
maana polisi wanafanya uchunguzi kujua ni siri gani imejificha.”
Kuhusu Jeshi la Polisi kuwa na taarifa ya kuwapo
mafunzo ya judo na karate kwenye baadhi ya nyumba za ibada, alisema
watachunguza madai hayo.
Inadaiwa mafunzo hayo hutolewa usiku katika baadhi maeneo ya Pasua, Njoro, Kibosho, na wilaya za Mwanga na Same.
Aprili mwaka jana, raia 20 wa Yemen walikutwa
vichakani alfajiri wilayani Same na walipohojiwa na kiongozi mmoja wa
kisiasa, walidai wamekuja kufundisha dini.
Habari zinadai miezi kadhaa iliyopita, polisi
mjini Moshi walivamia msikiti mmoja uliopo Kibosho na kukuta vijana
wadogo kutoka Singida, Babati na Kondoa wakifundishwa mbinu hizo za
kupigana.
Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) wa
Kilimanjaro, Rashid Mallya aliliambia gazeti hili juzi kuwa wamestushwa
na wimbi hilo la watoto kuletwa mkoani hapa kwa mafunzo ambayo
aliyaelezea kuwa hayafahamika.
“Tumeshtushwa
na hatuliungi mkono hili kwa sababu
maeneo ya kufundishia dini yetu yanajulikana na si nyumbani kwa mtu.
Vyombo vyetu vichunguze jambo hili kwa uzito,”alisema. Tangaza biashara
yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa
Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment