Tuesday, December 23, 2014

RAIS KIKWETE ATENGUA UTEUZI WA PROFESA TIBAIJUKA

Rais Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete, ametengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, huku pia akitengua kitendawili cha nani mmiliki wa fedha za akaunti ya Escrow na kusema sio za umma bali ni za IPTL.
Aidha, Serikali kupitia Kamati ya Maadili inaendelea kumfanyia uchunguzi kwani kuna upungufu wa kimaadili umeonekana kutendeka.
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa anahutubia taifa kupitia wazee na wakazi wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, lengo likiwa kuzungumzia mambo mbalimbali ya kitaifa, yakiwemo yale yaliyokuwa yakisubiri uamuzi wake, kubwa likitajwa la sakata la Akaunti ya Escrow.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.

Baada ya kutoa historia ndefu ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), tangu kuanza kwake hadi sakata la Escrow, Rais Kikwete alianza kujibu na kutolea maamuzi maazimio nane ya Bunge, huku lililokuna wengi likiwa la kuwajibisha viongozi waandamizi, wakiwemo mawaziri katika serikali yake na pia Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.
Akizungumzia hilo, alisema Bodi ya Tanesco imeshamaliza muda wake, hivyo ni kama imeshajifuta, aidha, suala la kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, amezitaka mamlaka zinazohusika zianze uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na endapo zitathibitika, atawajibishwa.
“Nimeagiza mamlaka husika zifanye uchunguzi na iwapo tuhuma dhidi yake zitabainika hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwepo kumwajibisha,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, alisema tayari Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema ameshajiuzulu ingawa amekuwa akisisitiza kuwa, hakuna kosa alilolifanya bali amewajibika ili kubeba `msalaba’ wa wengine aliokuwa anawashauri, hivyo amejiwajibisha huku akiongeza kuwa, kuhusu Profesa Tibaijuka amezungumza naye na kukubaliana aachie ngazi.
Muhongo awekwa kiporo
Wakati akichukua uamuzi huo dhidi ya Profesa Tibaijuka, Rais Kikwete alitangaza kumweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kwani suala lake liko katika hatua za kiuchunguzi.
“Kuhusu Muhongo tumemuweka kiporo, kuna uchunguzi nimeagiza ufanywe na matokeo yake yanaweza kuja baada ya siku mbili na nitafanya maamuzi kwa haki,” alisema Rais Kikwete.
Maswi na Muhongo walikuwepo ukumbini wakati Rais anahutubia, ilhali Profesa Tibaijuka hakuwepo.
Tuhuma za Tibaijuka
Akizungumzia tuhuma za Tibaijuka, Rais alisema: “Tumezungumza naye na Kamati ya Maadili inaendelea kuzungumza naye, na msingi wa mazungumzo yetu ni fedha alizopewa ni za nini na alisema ni za kuendesha shule, ila kwa nini hazikuenda moja kwa moja kwenye akaunti ya shule?
Ila akasema masharti ya watoaji (VIP Engineering), ndio yalitaka hivyo, ila kimsingi kuna upungufu wa kimaadili hapa na sina hakika kama hawa wanaopitapita kwenye akaunti wanaona nini. Tumekubaliana atupe nafasi tumteue mwingine.“ alisema Rais Kikwete.
Maazimio mengine ya Bunge aliyoyatolea uamuzi ni la kutaifisha mitambo ya IPTL na kuipa Tanesco, ambapo alisema; “Ni jambo linalojadilika na Serikali imelipokea na kulijadili, ila kutaifisha mitambo wakati huu wa kuwavutia wawekezaji si jambo sahihi na litaleta picha mbaya kwa wawekezaji. Tulishaacha hayo masuala ya kutaifisha.”
Aidha, alisema Mahakama iliagiza IPTL, kushusha bei ya umeme na kampuni hiyo ikaagizwa kubadilisha mitambo yake ya kufua umeme kutoka ya dizeli kuwa ya gesi na kwamba maagizo hayo ni mazuri, kwani umeme utakuwa ukinunuliwa kwa bei ndogo.
Kuhusu uwazi wa mikataba, alisema serikali itafanya mapitio ya mikataba, na kuongeza kuna haja ya Serikali na Bunge kukaa pamoja na kuzungumza jinsi ya kwenda na jambo hilo kwani kuna makampuni yanataka usiri wa mikataba .
Aidha, akizungumzia azimio la kuwavua vyeo wenyeviti wa Kamati za Bunge, alisema suala hilo lipo katika mamlaka za Bunge husika. Kuhusu kuundwa kwa Tume ya Kijaji kuwachunguza majaji waliohusika na sakata la Escrow, alisema itabidi kuzingatia utaratibu wa kikatiba na sheria.
Alisema suala hili linatakiwa kuanzia kwenye mahakama, badala ya kuanzia kwa Rais au bungeni, hivyo amemwachia Jaji Mkuu alishughulikie suala hilo na kwamba anachosubiri ni mapendekezo ya hatua za kuchukua.
“Tume ya Majaji ndio wanapaswa kujadili jambo hili na sio lianzie kwangu, ila nimemwambia Jaji Mkuu alishughulikie hili na wakiona majaji hao wamepoteza sifa na wakaleta uamuzi kwangu kwani mimi ndiye ninapewa majina ya kuteua, nitafanya maamuzi ,” alisisitiza Rais.
Akizungumzia azimio la kutaka mamlaka husika za kifedha na kiuchunguzi ziitaje Benki ya Stanbic na nyingine zilizohusika katika sakata la Escrow zitangazwe kuwa taasisi zinazotakatisha fedha alisema ni pendekezo zuri ila uchunguzi ufanywe.
“Ni jambo zuri na uchunguzi ufanywe,tunavyo vyombo vya uchunguzi vya ndani watafanya kazi hiyo”, alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete pia alizungumzia uundwaji wa mamlaka za kushughulikia rushwa kubwa na ndogo, akisema serikali iandae na kuwasilisha marekebisho ya sheria ya uundwaji wa vyombo hivyo.
Alisema ni wazo zuri, na serikali imekuwa inaifanyia marekebisho Taasisi ya Kuzuia Rushwa tangu mwaka 2008. Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Akaunti ya Escrow
Kuhusu nani ni mmiliki wa akaunti ya Escrow na iwapo fedha ni za umma au hapana, Rais alifafanua kuwa umiliki wa akaunti hiyo ni tofaati na akaunti nyingine na kwamba akaunti hiyo ilifunguliwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo ilikuwa ni kuweka fedha za IPTL kutoka Tanesco.
“Baada ya kuwa na mzozo baina ya Tanesco na IPTL, waliamua kufungua akaunti ambayo fedha zitakuwa zinahifadhiwa huko wakati mzozo wao wakiendelea kuutafutia suluhu na akaunti hiyo waliifungua Julai 5,mwaka 2006,” alisema Rais Kikwete.
Na Kwamba fedha zilizokuwa zikiwekwa humo ni za madai ya tozo la uwekezaji ambalo kampuni ya IPTL iliidai Tanesco hivyo, fedha hizo ni za IPTL na sio za Umma na kwamba Mamlaka ya Mapato nchini TRA, ilishapeleka madai ya kodi ya serikali ya ongezeko la thamani kwa IPTL na wamekubali kulilipa.
“Kwa mantiki hiyo fedha sio za umma ni za IPTL ambaye ndiye mlipwaji madai yake kutoka Tanesco,” alisema Rais Kikwete na kuongeza tangu akaunti hiyo ifunguliwe miaka saba sasa kwa bahati mbaya Tanesco haikufanikiwa kufikia suluhu na IPTL hadi kampuni hiyo ikapewa malipo yake.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete, imefuta hisia kwamba fedha za IPTL zilizoibua mjadala mkali bungeni zilikuwa za umma.
Ndani ya Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliomalizika Novemba 28 mwaka huu, wabunge walichachamaa na kutaka serikali iwawajibishe wote waliohusika na kutafuna fedha za IPTL zaidi ya Sh bilioni 300, huku ikisisitizwa kuwa ni za umma, jambo ambalo Rais Kikwete amethibitisha kuwa ulikuwa upotoshaji.
Wakati Rais Kikwete akizungumzia suala hilo, Profesa Muhongo alikuwa ni miongoni mwa mawaziri waliohudhuria akiwamo pia Maswi. Wengine ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na wengineo. Hata hivyo, Profesa Tibaijuka hakuhudhuria mkutano huo.
Kauli ya Zitto
Akizungumzia uamuzi wa Rais Kikwete, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto alisema: “Nimemsikiliza Mheshimiwa Rais. Ninachoweza kusema ni kwamba maazimio yale hayakuwa ya Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni maamuzi ya Bunge zima. Bunge la vyama vyote kikiwamo chama cha Rais Kikwete yaani CCM.
“Sisi kama Bunge tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na bila kutaka kumuonea mtu yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi. Bunge limefanya kazi yake na Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi wataamua wenyewe”.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz, ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715 221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Na Habari Leo 

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...