Uongozi wa Yanga umepanga
kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuishtaki TFF kwa
kukiuka Kanuni ya 19 ya usajili katika kufanya uamuzi wa utata wa
usajili wa mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi.
Kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya TFF kilichofanyika jijini Dar es salaam juzi, kiliamua kumtangaza
Okwi kuwa mchezaji huru baada ya kubaini kuwa Yanga ilivunja mkataba kwa
kutomlipa stahiki zake za usajili na pia kuandika barua TFF kutaka
mkataba wake na Mganda huyo uvunjwe, uamuzi ambao umeinufaisha Simba
ambayo imemsajili.
Mkataba wa mchezaji huyo ulipitiwa na kamati hiyo
ikiwamo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na Yanga na kuridhika kuwa
mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Kamati hiyo ilisema ukiwa ni mkataba wa pande
mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba nane kuhusu malipo ya ada ya
usajili. Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho hadi kufikia
Juni 27 mwaka huu, ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe.
Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu
yoyote.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga jana ulisema
haukubaliani na uamuzi huo na kwamba walikuwa wameshaandika barua
kupinga baadhi ya wajumbe katika kamati ya sheria ya TFF wasisikilize
kesi yao, akiwamo mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hans Pope ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya sheria.
Akizungumza jijini jana, mwenyekiti wa Kamati ya
Sheria na Katiba wa Yanga ambaye pia aliiwakilisha Yanga juzi, Sam
Mapande alisema hawana imani na kamati iliyotoa uamuzi kwa kuwa kuna
mgongano wa kimasilahi na TFF wanajua hilo.
“Msimamo wetu ni kwamba tunatambua Okwi bado ni
mchezaji wetu kwa kuwa tuliwaandikia barua TFF ya kuvunja mkataba na
Okwi hawajafanya hivyo, kuna wajumbe tuliomba watoke, lakini hawakutoka
hivyo hatuna imani na kamati. Pia TFF ilipaswa kusaka wasuluhishi
wengine ambao si wa kamati ile kwa sababu tayari tulishaonyesha
wasiwasi, lakini TFF haikufanya hivyo,” alisema Mapande.
“Jana (juzi) tumetoka pale tukikubaliana na kamati
leo (jana) tupeleke maelezo mengine ya ziada kama tunayo, lakini
tunasikitika wametoa uamuzi wakati hatujawasilisha maelezo yetu.
“TFF walikuwa na ajenda zao binafsi kwani licha ya
kuwapelekea barua lukuki hakuna hata moja iliyofanyiwa kazi zaidi
kuandikiwa barua ya kuitwa kwenye kikao cha jana (juzi).
“Barua ya TFF ilituambia itajadili malalamiko yetu
yote ikiwamo ya Okwi kufanya mazungumzo na timu ya Misri kinyume cha
taratibu, itajadili barua ya Yanga kuomba kuvunja mkataba na Okwi na
barua ya kumlazimisha arudishe fedha zote za usajili na mishahara
aliyochukua, pia alipe Dola 200,000 kwa kuikosesha Yanga ubingwa.
“Tuliishtaki pia Simba na timu ya Misri kufanya
mazungumzo na Okwi kinyume cha taratibu. Lakini cha kushangaza
tulipoingia kwenye kikao, yule mwenyekiti (Richard Sinamtwa) alisema
wanashughulika na usajili tu na si malalamiko mengine. Hiyo ni ajabu
sana,” alisema Mapande.
Alisema: “Kamati ya Sheria ya TFF imejivika
malalamiko kwa kutolea uamuzi jambo ambalo halikuwapo mezani mwake.
Kwenye mkataba kuna kipengele kinasema mkataba unavunjwa kwa pande mbili
kuelewana kama wameshindwana kimkataba, lakini Okwi hakuwahi kupeleka
malalamiko yoyote TFF.”
Hata hivyo, Kaimu katibu mkuu wa TFF, Boniface Wambura alisema
kuwa masuala ya uhalali wa Okwi kusajiliwa Yanga au Simba yataamuliwa
Jumamosi wakati kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji itakapokutana kwa
mara nyingine kupitia masuala ya usajili.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, Zacharia Hans Pope amesema Yanga waende wanapoenda ila wataishia
kuhangaika kwani Kamati ya Sheria TFF imetoa uamuzi sahihi bila kupepesa
macho kwamba Okwi ni mchezaji huru na hivi sasa ameamua kujiunga Simba
ambayo aliwahi kuichezea kabla ya kwenda Tunisia kuitumikia klabu ya
Etoile du Sahel.
No comments:
Post a Comment