Rais Jakaya
Kikwete jana aliwafukuza makada wa CCM waliokuwa wakimsubiri kwenye
kituo cha dharura cha ebola alipokitembelea kwa kushtukiza katika
Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Makada hao ambao baadhi yao walivalia sare za CCM,
kinyume na matarajio yao, kiongozi huyo alipofika hospitalini hapo
alionyesha kuwashangaa kabla ya kuwataka waondoke kwa kuwa hakuhitaji
kuzungumza nao, bali wasimamizi wa kituo hicho.
“Hawa watu wote wanafanya nini hapa! Sijaja
kuhutubia hapa mimi. Ndugu zangu hawa waliowaita wamewasumbua bure,
nawashukuruni sana kwa kuja, endeleeni na shughuli zenu,” alisema Rais
Kikwete ambaye aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky
Sadiki.
Hatua hiyo ilionekana kuwanyong’onyeza makada hao
ambao hawakuwa na jinsi isipokuwa kuondoka taratibu kwenye eneo hilo na
kumwacha Rais Kikwete na viongozi wa kituo hicho.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Ukaguzi wa kituo
Katika ukaguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete
alieleza kutoridhishwa na maandalizi na akaagiza ukarabati mkubwa
ufanywe haraka ili kiwe na hadhi inayostahili.
Alionyesha kushangazwa na miundombinu duni ikiwamo
vyoo vibovu na ukosefu wa maji katika kituo hicho na kuagiza kufanyika
marekebisho ya haraka.
“Hivi hii ni kweli? Hakuna maji, vyoo vibovu,
kituo chenyewe kikuukuu! Kwa taarifa za awali, kituo hiki kilikuwa ni
kwa ajili ya ugonjwa wa kipindupindu, hakiendani kabisa na hitaji la
sasa la kuwahudumia wagonjwa wa ebola iwapo watabainika kuingia nchini,”
alisema Rais Kikwete.
Alisema katika hali ya kawaida, kituo hicho
kinatakiwa kuwa cha kisasa na chenye mazingira yanayowezesha kutoa
huduma kwa wagonjwa hao kwa usalama.
Alisema ameamua kufanya ziara hiyo Temeke na
ukaguzi wa namna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuona
ukweli wa taarifa alizopewa na kuzizungumza katika mkutano na wazee wa
Mkoa wa Dodoma wiki iliyopita.
“Hii ndiyo fursa ya hii dharura ambayo mnatakiwa
kuitumia vyema na kupata kituo cha kisasa na kwa wakati huu. Kama kuna
matatizo ya fedha tuelezane tutajua namna ya kufanya,” alisema Rais
Kikwete.
Alisema ni vyema kuhakikisha kunakuwa na kituo
maalumu cha kuwapokea na kuwahifadhi waathirika wa magonjwa ya mlipuko
ambacho ni cha kipekee na cha aina yake nchini.
Na Mwananchi
Mratibu wa Huduma za Dharura wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Christopher Mnzava alisema kituo hicho kimeandaliwa na manispaa zote
tatu za Jiji la Dar es Salaam; Temeke, Ilala na Kinondoni.
Alisema tayari kamati maalumu iliyoundwa Agosti 5,
mwaka huu chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa imeangalia maeneo muhimu
ya kufanyia kazi, ambayo ni suala la tiba, namna ya kuwahifadhi
wagonjwa, usafiri wa wagonjwa, utoaji wa mafunzo kwa watumishi na jamii
ya Mkoa wa Dar es Salaam
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid
alisema wizara yake inasimamia pia uanzishwaji wa vituo vya aina hiyo
kwa ajili ya dharura katika kila mkoa ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema pia inafanya mpango wa kuimarisha maabara
ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Tiba (NIMR) ili iwe na uwezo mkubwa wa
kupima magonjwa mengi ikiwamo ebola. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment