Friday, September 05, 2014

BUNGE LA KATIBA LAKATAA ELIMU YA KIDATO CHA NNE KWA WABUNGE


Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Amir Kificho (kulia) akiwaeleza jambo wajumbe wa bunge hilo walipohudhuria kikao cha 32 cha Bunge mjini Dodoma jana.

Pendekezo la Rasimu ya Katiba kuwa wabunge walau wawe na elimu ya kidato cha nne limetupiliwa mbali na wajumbe wa Bunge Maalumu, baada ya Kamati karibu zote kulikataa.
Kamati hizo zimependekeza kigezo cha elimu kuanzia walau kidato cha nne kama sharti muhimu la mtu anayetaka kugombea Ubunge kiondolewe, badala yake mgombea ama ajue tu kusoma na kuandika, au ajue kusoma na kuandika Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama ilivyo kwenye Katiba ya sasa.Mbali na pendekezo hilo, kamati hizo zimegawanyika kuhusu Ibara ya 129 ya Rasimu ya Katiba inayowapa wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao madarakani kabla ya miaka mitano kumalizika.
Hayo yalijitokeza bungeni Dodoma jana, wakati kamati hizo zikiwasilisha taarifa zake kuhusu Sura ya 9 na 10 ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Akiwasilisha maoni ya Kamati Namba 10, Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu alisema suala la kugombea nafasi yoyote ni la kidemokrasia, hivyo haipaswi mtu yeyote kuzuiwa kwa kigezo cha elimu.
“Haki ya kuamua iwapo mgombea anafaa au hafai ni ya wapigakura. Wasizuiwe kikatiba kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua mtu wanayemtaka,”alisema na kuongeza: “Utaratibu huu haupo duniani kote hata nchi zilizo na demokrasia iliyokomaa. Hivyo ibara hiyo isomeke tu ajue kusoma na kuandika na si kiwango cha elimu kama sifa ya msingi.”
Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na Kamati Namba 8 kupitia kwa Mjumbe wake, Juma Alawi aliyesema kuweka kiwango cha elimu kwa wagombea ubunge ni ubaguzi.
Kuondolewa kwa kigezo cha elimu ya kidato cha nne pia kumeungwa mkono na kamati namba 10, 4, 12, 9 na 12 za Bunge hilo zilizowasilisha taarifa zake jana asubuhi.
Kamati namba 12 ndiyo iliyokwenda mbali zaidi na kudai kuwa ibara hiyo itasababisha ubaguzi kulingana na elimu wakati kiwango cha chini cha elimu kwa Tanzania Bara ni darasa la saba na Zanzibar ni darasa la 10.
Hata hivyo, ni Kamati Namba 2 tu inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha iliyokubali pendekezo la Rasimu la kutaka kuwapo kigezo cha elimu. Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Vuai alitaka ibara hiyo ifanyiwe marekebisho na kufuta maneno “anajua kusoma na kuandika Kiingereza na Kiswahili” na badala yake isomeke, “ana elimu isiyopungua kidato cha nne”.
Wakati kamati karibu zote zikikubaliana kuhusu kuondoa kigezo cha elimu katika kuwania ubunge, zimetofautiana kuhusu Ibara ya 129 ya inayowapa wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao asiyewajibika kwao.
Mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba yalitaka wananchi wawe na haki ya kumuondoa mbunge, endapo ataunga mkono sera zinazokwenda kinyume na masilahi ya wapigakura wake au iwapo atashindwa kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero zao au ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka jimbo lake kwa miezi sita bila sababu.
Kamati Namba 12 iliafiki wananchi kupata nguvu hiyo ya kumuondoa mbunge endapo tu atakuwa ameunga mkono sera ambazo zinakwenda kinyume na masilahi ya taifa na si ya wapiga kura waliomchagua. 
“Kimsingi hakuna namna bora ya kumtathmini mbunge kuwa ameshindwa kutekeleza na kutetea hoja na kero za wapigakura,” alisema Jaffo kwa niaba ya kamati.
Kamati namba 8, 2, 10, 4 na 9 zilipendekeza ibara hiyo ifutwe isipokuwa kamati namba 9 iliyoenda mbali zaidi na kupendekeza kutungwa kwa sheria ya kumdhibiti mbunge anayeshindwa kutekeleza majukumu yake.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walio wachache katika kamati zao walipendekeza ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye Rasimu. Maoni ya kamati mbalimbali za walio wachache waliounga mkono kubaki kwa ibara hiyo yalisomwa na Dk Tulia Ackson na Elizabeth Minde  ambao wote ni wanasheria kitaaluma.
Wakati huo huo, suala la kuwapo au kutokuwapo kwa Mahakama ya Kadhi katika Katiba Mpya jana liliibuka tena Bungeni baada ya wajumbe walio wachache kutaka liingizwe kwenye Katiba. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...