UWANJA wa Azam Complex
unaomilikiwa na mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam
fc umezidi kuwa mgumu kwa timu za ligi kuu.
Timu pinzani zinapofika maeneo ya Chamazi zinaanza kupata harufu ya kipigo kutoka kwa wenyeji wao.
Chamazi si sehemu salama kwa timu za ligi kuu isipokuwa kwa Simba na Yanga ambao hawajawahi kucheza katika uwanja huo.
Azam fc wakiendelea kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani, jana walishinda mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Mkoani Pwani.
Kabla ya mechi hii, niliandika
kupitia mtandao huu nikisema Azam fc wataifunga Ruvu Shooting kwasababu
mazingira ya Chamazi ni rafiki kwao na wana kikosi kilichojaa. Nilisema
sio rahisi kuifunga Azam katika uwanja wake, hata rekodi zinaonesha
hivyo.
Azam walikwenda kupumzika wakiwa mbele kwa bao 1-0 liliofungwa na Mrundi, Didier Kavumnagu katika dakika ya 40. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kavumbagu alifunga goli hilo
baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Ruvu Shooting,
Abdallah Abdallah kufuatia shuti la Kipre Tchetche aliyeunganisha krosi
murua ya Shomari Salum Kapombe.
Lilikuwa bao jepesi kabisa kwa
Didier, lakini lilitosha kufikisha mabao 3 katika mechi mbili, baada ya
kufunga mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro katika
mechi ya ufunguzi.
Dakika ya 50, Himid Mao Mkami alipiga krosi safi iliyomaliziwa kiufundi na Didier Kavumbagu na kuiandikia Azam bao la pili.
Hilo lilikuwa bao la nne kwa
Kavumbagu katika mechi mbili na inaonekana safari hii amedhamiria kupata
kiatu cha dhahabu anachomiliki Amissi Tambwe wa Simba. Hata hivyo,
Kavumbagu alikosa baadhi ya nafasi kadhaa za kufunga.
Mabeki wa kati wa Ruvu Shooting,
Salvatory Ntebe na Hamisi Kasanga walishindwa kuhimili makali ya
washambuliaji wa Azam fc na mara nyingi waliruhusu mashambulizi langoni
mwao.
Katika dakika ya 70, Salum
Abubakary ‘Sure Boy’ alikaribia kufunga, lakini alikosa umakini wa
kuunganisha krosi ya Kavumbagu na dakika tano baadaye, Mrundi huyo
alishindwa kufunga ‘Hat-trick’ ya kwanza msimu huu kufuatia
kutengenezewa mpira safi na Tchetche.
Kipre Balou, Mudathir Yahya
walishika barabara sehemu ya kati, huku Salum Abubakar aliyecheza nyuma
ya Didier Kavumbagu akifanya kazi nzuri.
Tchetche aliyeshambulia kutoka
kushoto na Himid Mao kutoka kulia, waliisaidia Azam kufika mara nyingi
zaidi langoni kwa Shooting, wakipiga krosi na kutoa pasi kwa
washambuliaji wa kati.
Azam fc wamekuwa wakiutendea haki uwanja wa nyumbani. Inafahamika kuwa kucheza nyumbani ni moja ya sababu ya kushinda mechi.
Uwanja wa nyumbani huwa ni rafiki kwa wachezaji. Wanakuwa huru na wanacheza mbele ya mashabiki wao wengi.
Azam fc haina mashabiki wengi
kivile ukilinganisha na Simba au Yanga, hata uwanja wa Chamazi huwa
haujai. Lakini haiwapi shida kufanya vizuri.
Lakini mbele ya mashabiki wao
wachache huko Chamazi, wamekuwa wakitandaza soka safi na kuiadhibu
karibia kila timu inayogusa uwanja wao.
Kwa bahati mbaya watu hawapati
nafasi ya kuwaona Azam fc hasa wanapocheza siku ambayo Simba au Yanga
inacheza pia. Lakini hawa vijana wanaonekana kuwa na mipango sahihi na
morali kubwa ya ushindi.
Kwa asimilia kubwa wachezaji wa
Azam wana utimamu mzuri wa mwili, wako fiti kimbinu, kiufundi na
kisaikolojia. Mazingira haya yamewafanya wacheze mpira vizuri na kwa
utulivu.
Kwa jinsi wanavyocheza mpira Chamazi, watu wengi nikiwemo mimi ningetamani kuona Simba na Yanga wakigusa dimba hilo.
Naamini hali ingekuwa ngumu kwa
wakongwe hao. Wangehangaika kupata matokeo kama inavyowatokea kwenye
baadhi ya viwanja kama vile Sokoine Mbeya, Jamhuri Morogoro na Mkwakwani
Tanga.
Kwa bahati mbaya zaidi wangekutana na timu bora ikiwa nyumbani kwake. Lakini kwasababu haiwezekani ndio basi tena.
Simba na Yanga zina mashabiki
wengi mno, uwanja wa Chamazi unachukua watazamaji wachache, hivyo
inalazimu mechi zote zinazowakutanisha Azam dhidi ya Simba au Yanga
kuchezwa uwanja wa Taifa.
Lakini sifa lazima ziwaendee Azam fc, wamekuwa bora wanapocheza nyumbani kwao na ndivyo inatakiwa kuwa.
Usifanye makosa nyumbani, najua
mpira umebadilika siku hizi, timu inaweza kushinda nyumbani na ugenini,
lakini bado uwanja wa nyumbani una faida nyingi.
Hata ulaya, ni ngumu sana kushinda ugenini kwasababu wenyeji wanakuwa na faida nyingi ikiwemo idadi ya mashabiki.
Kwa jinsi Azam walivyo na kikosi
kikubwa, wanavyojiamini nyumbani kwao, wataendelea kuzichapa timu za
ligi kuu mpaka pale zitakapojipanga kimbinu zaidi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Baraka Mpenja
No comments:
Post a Comment