Sasa ni dhahiri
kuwa maisha ya kiongozi wa zamani wa nchi hii, Nelson Mandela yamo
hatarini kutokana na kwamba anaishi kwa msaada wa mashine,
imethibitishwa na mmoja wa wazee wa ukoo wa kiongozi huyo.
Binti yake mkubwa Makaziwe naye
amethibitisha hilo, akisema hali ni mbaya na chochote chaweza kutokea.
"Naweza kusisitiza hilo, kwamba Tata
(baba) hali yake ni mbaya sana, chochote chaweza kutokea, lakini nataka
nisisitize tena, kwamba ni Mungu tu ndiye anajua muda wa kuondoka,”
alikiambia kituo cha utangazaji cha SAFM jana.
Hali
hiyo inayotia mashaka imesababisha hata Rais Jacob Zuma afute safari
yake ya Msumbiji ambako alipanga kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Ndiyo, anatumia mashine kupumua,” Mzee Napilisi Mandela
aliiambia AFP muda mfupi baada ya kumtembelea Mandela hospitalini juzi.
“Hali ni mbaya, lakini tutafanyaje.”
Zuma alifuta safari yake iliyokuwa ifanyike jana baada ya
“kubaini, kwamba kiongozi huyo wa zamani hali yake bado ni mbaya,”
taarifa kutoka Ofisi ya Rais ilisema.
Wakati huo huo, kiongozi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu
Ban Ki-moon alisema juzi kwamba dunia yote inamwombea Mandela wakati huu
ambapo anapigania maisha yake.
Ban alimwita Mandela “mmoja wa mashujaa wa karne ya 20”
katika hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika,
OAU (sasa Umoja wa Afrika-AU) iliyofanyika New York, Marekani, ambao
uliongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
“Najua fikra na maombi yetu viko na
Nelson Mandela, familia yake na wanaompenda, Waafrika Kusini wote na
watu wote duniani ambao wamekuwa wakivutiwa na matendo yake maishani na
kuwa mfano wa kuigwa,” alisema Ban.
“Hebu nasi leo tuoneshe dhamira ya uwajibikaji wa dhati
katika kuhakikisha tunaboresha maisha na fursa za Waafrika wote,”
alisema Katibu Mkuu wa UN.
Zuma
alimtembelea Mandela hospitalini juzi saa nne usiku na kumkuta akiwa
bado na hali mbaya, msemaji wa Rais, Mac Maharaj alisema.
“Rais Zuma alizungumza na madaktari ambao bado wanaendelea
kufanya kila linalowezekana kuokoa maisha yake ... ameamua kufuta safari
yake ya Maputo kesho (jana), ambako alitakiwa kuhudhuria Mkutano wa
Uwekezaji katika miundombinu kwa nchi za Kusini mwa Afrika wanachama wa
SADC.”
Mandela (94)
alilazwa katika hospitali ya moyo ya Medi-Clinic iliyoko hapa Juni 8
kutokana na kuibuka upya kwa matatizo ya mapafu yake.
Katika hatua nyingine, mjukuu wake,
Mandla Mandela, amekanusha kuwapo kwa mvutano kati yake na shangazi
yake, Makaziwe, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana.
Magazeti yaliripoti juzi kwamba anadaiwa
alijitoa kwenye kikao cha familia kilichofanyika Qunu Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, anadaiwa
kuhamisha makaburi ya watoto watatu wa Mandela kutoka Qunu hadi Mvezo
mwaka 2011, bila hata kushauriana na familia.
Iliripotiwa pia kuwa familia hiyo ilikuwa
ikitaka watoto hao, Makgatho, Thembekile na Makaziwe, warudishwe Qunu.
“Chifu Zwelivelile (Mandla) hana suala
lolote na mtu mwenye mamlaka ya kurudisha Qunu kaburi lolote au makaburi
yote,” msemaji wa Mandla, Freddy Pilusa alikaririwa akiiambia The Star
jana.
“Mvezo ndiko mahali
ilikozaliwa familia ya Mandela na kimila ndiko nyumbani kwao, na hivyo
ndiko iliko historia ya familia hiyo.” Alisema Mandla hawezi sasa
kuzungumzia lolote kuhusu mipango ya maziko ya babu yake.
Waganga wa jadi wa Limpopo jana
walifanya matambiko katika ofisi za ANC zilizoko Polokwane kumwombea
Mandela.
Mwenyekiti wa Timu
kazi ya ANC Limpopo, Falaza Mdaka, alisema waganga hao waliomba
kufanyia tambiko lao katika ofisi hizo wakisema ndiko kulikuwa
‘nyumbani’ kwa Mandela na kuongeza kuwa alikuwa mtu wa aina yake na
dunia bado inamhitaji.
Waganga
hao waliimba nyimbo za mapambano na kuchoma ubani, wakiwaomba wahenga
kumponesha kiongozi huyo anayependwa na nchi nzima. “Mandela anahitaji
msaada wa wahenga,” alisema mmoja wa waganga hao, Sylvester Hlathi.
No comments:
Post a Comment